Mashariki ya Kati inavyoadhimisha Eid katikati ya vita

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya  Waislamu wakiendelea na mfungo wa Ramadhan katika baadhi ya maeneo duniani, Mashariki ya kati katika mataifa kama Saudi Arabia wamesherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr.

Kutokana na tishio la kiusalama linalochochewa na vita vya Iran, Israel na Marekani, mataifa hayo ya Ghuba yametangaza kuwa sala za sikukuu ya Eid mwaka huu zinafanyika katika misikiti ya kawaida badala ya umati wa watu kukusanyika viwanjani kama ilivyo ada, ikiwa ni tahadhari kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Iran kwa mataifa hayo.

Taarifa kutoka ukanda huo zinasema Wapalestina katika Ukanda wa Gaza ulioharibiwa vibaya na vita leo wamekusanyika kuadhimisha sikukuu ya Iddi inayoashiria mwisho wa mwezi wa mfungo wa Ramadhan.

Wakiwa wamedhamiria kukiondoa kiwingu kilicholetwa na vita katika ukanda huo,  inaelezwa kuwa wazazi katika eneo la Khan Younis wamekusanyika kuoka biskuti kwa ajili ya watoto wao ambao maisha yao yameathiriwa na vita.

Huku sherehe hizo zikiendelea,  Israel imekuwa ikifanya mashambulizi ya hapa na pale kila kukicha katika ukanda huo ikiilenga Iran ambayo imekuwa ikijibu na kuzidisha tishio la kiusalama katika ukanda huo wenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Vyanzo vya habari barani humo vinaeleza kuwa mazingira ya maadhimisho ya Eid yamekuwa ya tofauti huku nchini Irak katika mji wa Erbil nako, maandalizi ya sherehe hizo yakiendelea huku wasiwasi wa usalama ukiwa umewagubika raia kutokana na vita hivyo vya Iran, Marekani na Israel.

Aidha, Wamiliki wa maduka katika mji huo wamenukuliwa na vyombo vya habari wakisema  mazingira ya biashara yamebadilika katika sherehe za mwaka huu ikilinganishwa na sherehe za mwaka jana.

Hata hivyo, licha ya wasiwasi ulioko, baadhi ya masoko yamesalia wazi huku familia zikiendelea kufanya manunuzi kwa tahadhari kwa ajili ya sherehe hizo za Eid.

Tangu kuanza kwa vita vya Iran mnamo Februari mwaka huu, Irak imeshuhudia mashambulizi kadhaa yakiwemo ya droni na makombora kufanywa nchini humo huku kambi za kijeshi, miundo mbinu ya mafuta na maeneo mengine yakishambuliwa.

Nako nchini Afghanistan waumini wa Kiislamu wameadhimisha sikukuu ya Iddi kwa sala katika msikiti wa Sha-Do Shamshira.

Mapema Jumatano, Afghanistan na Pakistan walitangaza usitishwaji wa mapigano yanayozidi baina ya nchi hizo mbili, siku mbili baada ya Kabul kuilaumu Islamabad kwa shambulizi la angani katika mji huo mkuu, lililosababisha vifo vya mamia ya watu.

Nchi hizo mbili zimetangaza kwa pamoja kuwa zinasitisha vita kupisha sherehe za Iddi kutokana na mwito wa Saudi Arabia, Uturuki na Qatar.

Huko Pakistan nako inaelezwa kuwa sikukuu hiyo inaadhimishwa huku maelfu ya watu wakiwa wamefurika kwenye vituo vya mabasi na treni mjini Lahore kujaribu kupata usafiri kuelekea maeneo ya vijijini kwa ajili ya kusherehekea na familia zao.

Hali hiyo inatajwa kufanana katika maeneo mengi ya Mashariki ya kati ikiwemo India na Bangaldesh ambako Waislamu wanaadhimisha sherehe hiyo ikiwa  imegubikwa na vita vinavyoendelea nchini Iran, ambavyo vimesababisha kuongezeka kwa bei za mafuta, gesi na kupanda kwa gharama za maisha.

Katika Mji Mkuu wa India New Delhi, uhaba wa mitungi ya gesi inayotumiwa na wengi kwa mapishi, inatajwa kusababisha migahawa mingi kutumia majiko ya mkaa huku Serikali ya nchi hiyo ikichukua hatua ya kuelekeza mitungi mingi zaidi ya gesi kutumika majumbani badala ya migahawa na mahotelini.

Bei za bidhaa nchini humo zimepanda, na baadhi ya migahawa imechukua hatua ya kutopika baadhi ya vyakula kutokana na matatizo hayo ya nishati, ambayo yamesababishwa pakubwa na vita vya Iran.

Hii ni kwa sababu India kwa sehemu kubwa inategemea gesi na mafuta yanayosafirishwa kupitia mlango bahari wa Hormuz.

Kwa upande wake, Iran ambayo ni moja ya mataifa yenye idadi kubwa ya Waislamu wa Kishia duniani imetangaza kuwa sherehe za Eid zitafanyika Jumamosi.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya kiongozi mkuu wa Mojtaba Khamenei ikisema Ijumaa ndiyo siku ya 30 na itakuwa pia siku ya kutazama kuandama kwa mwezi, kulingana na kalenda ya Kiislamu, huku siku ya mwisho ya Ramadhan huko nchini Iran inakuja wakati wa sherehe za mwaka mpya wa Nowruz

Aidha, Jumamosi Machi 21, imetangazwa kuwa ndiyo  siku ya Eid katika maeneo yanayosalia ikiwemo Afrika Mashariki ambapo Ijumaa ya leo ndiyo mwisho wa mfungo huo.