MKUTANO WA HALI YA WANAWAKE DUNIANI (CSW 70 WAHITIMISHWA NEW YORK, MAREKANI.

-WAZIRI DKT. GWAJIMA KUANZISHA JUKWAA LA MAJADILIANO ENDELEVU YA KISEKTA KUHUSU MIKUTANO YA WIZARA KIMATAIFA.

Na WMJJWM New York Marekani

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema, Serikali kupitia Wizara anayoiongoza itaanzisha Jukwaa endelevu la majadiliano ya Kisekta litakaosaidia kuongeza ufanisi wa ushiriki wa Nchi katika Mikutano ya kimataifa inayogusa maendeleo ya Wanawake na Jinsia.

Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo jijini New York nchini Marekani mara baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa 70 wa Hali ya Wanawake Duniani (CSW 70) ambapo, Tanzania ilishiriki na kueleza mafanikio iliyopata katika kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana.

Waziri Dkt. Gwajima amesema jukwaa hilo litasaidia kuwepo kwa uelewe wa pamoja kati ya Serikali na wadau wengine wote katika kuratibu ushiriki wa nchi katika mikutano mbalimbali ya kimataifa hasa inayogusa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili kuongeza ufanisi zaidi.

“Ni muhimu tuwe na Jukwaa hili ambalo litasaidia kuturatibu Serikali na wadau wetu wote ili, tunapotaka kushiriki katika Mikutano ya Kimataifa tuwe na uelewa wa pamoja na maandalizi ya pamoja ya kwenda kuitangaza nchi kimataifa” amesisitiza Waziri Dkt. Gwajima

Ameeleza kuwa, Tanzania imeshiriki mikutano mbalimbali iliyoandaa na iliyoalikwa ikiwa na lengo la kueleza mafanikio ya nchi katika suala la upatikanaji wa haki kwa wanawake na watoto wa kike na pia kujifunza namna mataifa mengine wanavyotekeleza suala hilo.

Aidha ameongeza kuwa, taarifa ya ushiriki wa Nchi katika Mkutano wa 70 wa Hali ya Wanawake Duniani itatolewa mara baada ya ujumbe ulioshiriki Mkutano huo kuwasili nchini.

Mkutano huo uliofunguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres Machi 09, 2026 uliongozwa na Kaulimbiu isemayo “Kuhakikisha na Kuimarisha upatikanaji wa Haki kwa Wanawake na Wasichana wote, ikiwa ni pamoja na kukuza mifumo ya kisheria nyenye usawa na jumuishi, kuondoa sheria, sera, na desturi za kibaguzi na kushughulikia vikwazo vya kimuundo”, (Ensuring and Strengthening access to justice for all Women and Girls, including by promoting inclusive and equitable legal system, eliminating discriminatory laws, policies, and practices and addressing structural barriers”).