Morogoro. Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM), Hussein Rashid Omary (23) amekutwa amefariki dunia ndani ya chumba chake katika tukio lililoibua taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo ambalo akiishi Kihonda Maghorofani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 20.2026 , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema mwanafunzi huyo alikuwa akisoma kozi ya ualimu mwaka wa tatu na alibainika kufariki asubuhi ya Machi leo katika nyumba aliyokuwa akiishi katika mtaa wa Mbuyuni, huku mwili wake ukiwa umeharibika.
Kamanda Mkama amesema taarifa za awali zinaeleza kuwa marehemu alianza kuugua tangu Machi 17, 2026 alipokuwa darasani, huku uchunguzi wa mwanzo ukionyesha kuwa huenda kifo chake kilitokana na maradhi ya kawaida ambapo mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri ndugu na jamaa kwa taratibu zaidi.
“Uchunguzi wa awali kifo cha Hussein kimetokana na maradhi ya kawaida na tumepata taarifa kuwa marehemu alianza kuugua tangu Machi 17, 2026 alipokuwa darasani,”amesema Kamanda Mkama.
Katika tukio lingine, Kamanda Mkama amesema Jeshi la Polisi limewakamata watuhumiwa wanane wanaodaiwa kujihusisha na mtandao wa wizi wa mifugo na biashara haramu ya nyama baada ya kukamatwa wakiwa na kilo 240 za nyama iliyokaushwa pamoja na vipande 10 vya mifugo.
Ameongeza Kamanda Mkama kwa kusema kuwa katika operesheni iliyofanyika kati ya Februari 17 na 19, 2026 ya kudhibiti uhalifu, hususan wizi wa mifugo na usambazaji wa bidhaa zisizokaguliwa kiwanda watuhumiwa hao.
Aliwataja baadhi ya watuhumiwa hao kuwa ni Baraka Melkiori (37), Charles Eliya Juma (22), Paschal Shimba (29), Omari Mohamed Ally (35), George Jafet Mamkwe (32) na Janet Thobias (26), wote wakazi wa Wilaya ya Kilosa.
Kwa mujibu wa Kamanda Mkama amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakishirikiana na wezi wa mifugo kwa kuchinja mifugo nyakati za usiku kinyume cha sheria, kisha kusambaza nyama hiyo katika maeneo yasiyo rasmi, ikiwemo mabucha yasiyotambulika.
“Tunatoa wito kwa wananchi kuhakikisha wananunua nyama katika machinjio yanayotambulika ili kuepuka madhara ya kiafya yatokanayo na ulaji wa nyama isiyokaguliwa,” amesema Mkama.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha doria na operesheni maalum katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu, huku akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Aidha, aliwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu, pamoja na kuepuka kununua nyama katika mabucha yasiyo rasmi.
Katika hatua nyingine, aliwatakia Waislamu na wananchi wote kwa ujumla sikukuu njema ya Eid el-Fitri.