Polisi Dar wakazia marufuku matumizi ya njia za mwendokasi

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesisitiza marufuku kwa magari binafsi, ya serikali pamoja na pikipiki kutumia barabara maalum za mabasi yaendayo haraka (BRT), likieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuzuia ajali zinazoweza kusababisha madhara makubwa kwa abiria.

Tamko hilo linakuja kufuatia kuendelea kwa ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani licha ya juhudi za utoaji elimu kwa makundi mbalimbali ya watumiaji wa vyombo vya moto.

Mwishoni mwa Januari 2026, Jeshi hilo lilieleza kuwa pamoja na kampeni za uhamasishaji, bado baadhi ya madereva wanaendelea kukiuka sheria kwa makusudi, hususan waendesha bodaboda, madereva wa magari binafsi na ya serikali, hali inayochangia ongezeko la ajali.

Wakati Jeshi la Polisi likitoa msisitizo huo, ajali Machi 17, 2026 kuna ajali ilitokea katika eneo la Msikitini, Barabara ya Kilwa, ikihusisha basi la mwendokasi la kampuni ya Mofat lililokuwa likifanya safari kati ya Mbagala na Gerezani.

Katika ajali hiyo, basi hilo liligongwa na gari dogo aina ya Toyota Forester lililoingia kwenye njia ya mwendokasi kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani (Cap 168), ni kosa kwa dereva yeyote kutumia njia isiyoruhusiwa.

Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Machi 20, 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema wamebaini ongezeko la madereva wanaokiuka sheria kwa kutumia njia hizo bila ruhusa, jambo linalohatarisha usalama wa abiria wa mabasi ya mwendokasi pamoja na watembea kwa miguu.

Amesema kupitia operesheni zinazoendelea, tayari wamefanikiwa kukamata magari kadhaa yakiwamo ya watu binafsi, ya serikali na pikipiki zilizokuwa zikitumia njia hizo kinyume cha taratibu.

“Katika kipindi hiki tumekamata idadi ya magari madogo pamoja na pikipiki zilizokuwa zinapita kwenye barabara hizi kinyume cha sheria. Tutaendelea kukusanya na kutoa takwimu zaidi kadri operesheni zinavyoendelea,” amesema Muliro.

Kamanda huyo ametoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na mwandishi wa Mwananchi kuhusu hatua zinazochukuliwa kudhibiti matumizi holela ya njia za mwendokasi.

Ameongeza kuwa baadhi ya madereva waliokamatwa wamechukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kutozwa faini huku wengine wakifikishwa mahakamani kwa kukaidi alama na maelekezo ya usalama barabarani.

Muliro amesisitiza kuwa ni marufuku kabisa kwa magari binafsi na pikipiki kutumia njia hizo, akionya kuwa ukiukwaji huo ni hatari zaidi nyakati za usiku na unaweza kusababisha ajali kubwa kwa abiria waliopo ndani ya mabasi.

“Unapopita kwenye njia hizi unaweza kupata madhara makubwa au kusababisha madhara kwa watu wengi waliopo kwenye mabasi. Hii ni hatari kubwa,” amesisitiza.

Aidha, amekemea watumishi wa serikali wanaokiuka sheria hizo, akisema wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa wananchi katika kuzingatia sheria na kanuni za barabarani.

“Kwa mtumishi wa serikali ni mbaya zaidi kwa sababu haonyeshi taswira nzuri ya utii wa sheria. Kila mmoja anapaswa kuwajibika kwa nafasi yake,” amesema.

Ametoa wito kwa madereva, waendesha bodaboda na wananchi kwa ujumla kushirikiana na vyombo vya dola kwa kufuata sheria, ili kulinda maisha yao na ya wengine.

Jeshi la Polisi limesema litaendelea na operesheni hizo kwa lengo la kuimarisha usalama barabarani na kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.