Profesa Kitila anadi uwekezaji wa kimkakati China

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ameitangaza Tanzania nchini China kama kitovu cha uwekezaji wa kimkakati, akisema nchi hiyo imejipanga kuwa lango la biashara, uzalishaji na usafirishaji kwa soko la kikanda na bara la Afrika.

Akihutubia jukwaa la kibiashara kati ya jimbo la Shandong (Weihai) na Tanzania, Profesa Kitila alisema Tanzania inaingia kwenye ushindani wa kimataifa wa kuvutia mitaji ikiwa na faida ya utulivu wa kisiasa, nafasi ya kijiografia, soko linalokua na mageuzi yanayoboreshwa kwa lengo la kuifanya sekta binafsi kuwa injini ya ukuaji wa uchumi.

“Tanzania ni moja ya maeneo yenye mustakabali mkubwa zaidi wa uwekezaji barani Afrika,” alisema Profesa Kitila katika hotuba yake mbele ya viongozi wa Serikali, wafanyabiashara na wawekezaji wa China.

Jukwaa hilo lilikuwa ni sehemu ya juhudi za Tanzania kujiweka katika nafasi bora zaidi kwenye ushindani wa kimataifa wa kuvutia uwekezaji, hasa katika kipindi ambacho nchi nyingi za Afrika zinapambana kujenga mazingira bora ya biashara, kupanua wigo wa viwanda na kutumia vyema fursa ya soko la pamoja la Afrika (AfCFTA).

Profesa Kitila alisema Tanzania inaingia katika ushindani huo ikiwa na nguzo kadhaa muhimu ambazo wawekezaji wengi huzitafuta, zikiwamo utulivu wa kisiasa, idadi kubwa ya watu, ukuaji wa uchumi, nafasi ya kijiografia na upatikanaji wa soko la kikanda.

Alisema kwa sasa Tanzania ina watu zaidi ya milioni 70, jambo linaloifanya kuwa soko muhimu kwa bidhaa na huduma, lakini zaidi ni kwamba nafasi yake ya pwani ya mashariki mwa Afrika, inaifanya kuwa mlango wa biashara kwa nchi kadhaa zisizo na bandari katika ukanda huu.

“Unapowekeza Tanzania, huwekezi Tanzania pekee, bali unawekeza katika soko kubwa zaidi la kikanda,” alisema na kusisitiza kuwa kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), mwekezaji anayeingia Tanzania anapata fursa ya kufikia mamia ya mamilioni ya watu.

Katika hotuba hiyo, Profesa Kitila alisema Tanzania kwa sasa inatekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambayo inalenga kuifanya nchi kuwa uchumi wa maarifa, wa viwanda, wenye ushindani na wa kipato cha juu cha kati, ifikapo mwaka 2050.

Alisema ushirikiano na wawekezaji wa kimataifa, hasa kutoka China, utakuwa nguzo muhimu katika kufanikisha safari hiyo.

“Tanzania sasa inaanza safari yake ya mabadiliko makubwa ya kiuchumi. Tunawaalika muwe sehemu ya safari hiyo,” alisema.

Profesa Kitila alisema uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China, umejengwa katika misingi ya mshikamano wa muda mrefu lakini historia hiyo sasa inapaswa kupewa sura mpya ya kiuchumi, ambapo urafiki wa kisiasa unatafsiriwa katika miradi zaidi ya pamoja, ubia wa uzalishaji, usindikaji, teknolojia na maendeleo ya miundombinu.

Alisema Tanzania inaamini inaweza kuwavutia wawekezaji wa China katika sekta ya viwanda na kuwa Serikali inaendelea kuijenga nchi  kuwa kitovu cha uzalishaji kwa ajili ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Kwa mujibu wa waziri huyo,  nchi inaendeleza maeneo ya viwanda, maeneo maalumu ya kiuchumi na maeneo ya usindikaji kwa ajili ya mauzo ya nje, huku ikialika kampuni za China kushirikiana katika uzalishaji wa nguo, vifaa vya ujenzi, uunganishaji wa vifaa vya kielektroniki, mashine na bidhaa nyingine za viwandani.

Katika kuonyesha uzito wa uhusiano wa kiuchumi uliopo tayari kati ya Tanzania na China, Profesa Kitila alisema hadi Machi 2026, nchi hiyo ilikuwa mwekezaji mkubwa zaidi nchini ikiwa na zaidi ya kampuni 1,000 zilizowekeza mtaji wa dola za Marekani 3.4 bilioni, sawa na karibu nusu ya mtaji wa wawekezaji 10 wakubwa nchini.

Alisema uwekezaji huo pia umezalisha ajira 90,414, sawa na asilimia 76 ya ajira zilizotokana na kundi hilo la wawekezaji wakubwa.