Saa 72 zinavyoleta hatari mpya Ligi Kuu Bara, wataalamu wafafanua

AZAM, Yanga na Singida Black Stars, hatimaye zimekamilisha duru la kwanza la Ligi Kuu Bara, huku ikiiacha Simba ikiwa bado na mechi mbili nayo kufunga hesabu hizo.

Kumbuka timu hizo nne zilikuwa na viporo vingi vilivyotokana na ushiriki wao wa michuano ya CAF msimu huu na Simba na Yanga zilikuwa Ligi ya Mabingwa, wakati Azam na Singida Black Stars upande wa Kombe la Shirikisho, huku ikishuhudiwa zote zikiishia makundi.

Wakati timu hizo zinamaliza majukumu yao ya michuano ya kimataifa, Yanga, Azam na Singida Black Stars zilikuwa zimecheza mechi nane kila moja za Ligi Kuu Bara, huku Simba ikiwa na saba. Wakati JKT Tanzania ikicheza mechi 11 ambazo zilikuwa nyingi kuliko timu nyingine.

Baada ya hapo, ratiba ikaanza kukimbizana huku baadhi ya timu zikipata muda mwingi wa kupumzika ikiwamo JKT Tanzania inayokaa kwa siku 69, sawa na miezi miwili na siku kumi bila ya kucheza mechi ya ligi kutoka Februari 25 ilipocheza dhidi ya Yanga hadi Aprili 4 itakapoikabili Namungo.

Wakati huohuo, kuna timu zinakosa muda rafiki wa kupumzika kama Yanga iliyotoka kukabiliana na TRA United, Machi 18, 2026 majira ya saa 10:00 jioni, ikiwa ni chini ya saa 72 tangu ilipomalizana na Azam, Machi 15, 2026, saa 2:30 usiku. Tofauti ya muda huo ni saa 68.

Ukiachana na Yanga, timu zingine zilizokuwa na viporo kama Azam, Simba na Singida Black Stars, mechi zake hakuna iliyochezwa chini ya saa 72.

Mashabiki wa Yanga hawaelewi kipi kinaikumba timu yao ikiangusha pointi sita ndani ya mechi tano za karibuni, lakini kabla ya mambo ya ufundi ratiba ya mechi hizo inatishia hatma ya timu hiyo kutetea ubingwa wake.

Iko hivi; tuanzie pale Yanga ilipokuwa mwenyeji dhidi ya Simba Machi Mosi, 2026, baada ya mechi hiyo, Yanga ilikuwa mgeni wa Singida Black Stars, Machi 5, 2026, kisha Machi 8, 2026, ikaikaribisha Polisi Tanzania katika mechi ya Kombe la Shirikisho la CRDB.

Baada ya hapo, Yanga ilishuka uwanjani Machi 11, 2026 ikiwa mgeni dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya, mechi iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri pale Dodoma.

Mechi iliyofuata, Yanga ilirejea jijini Dar es Salaam ikiwafuata wenyeji wao Azam FC, mchezo uliopigwa Machi 15, 2026 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Ilipomalizana na Azam, Yanga ikasafiri mpaka Mkoani Arusha ikiwafuata wenyeji wao TRA United, mechi iliyopigwa Machi 18, 2026. Jumamosi Machi 21, 2026 Yanga itakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, ikirudi tena pale Jamhuri jijini Dodoma.

Katika mechi hizo, Yanga imecheza chini ya saa 72 kutoka ilipocheza dhidi ya Azam kisha kukabiliana na TRA United, lakini zingine zilikuwa ndani ya muda huo, huku changamoto pekee ikiwa ni kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine, hata hivyo, klabu hiyo inatumia usafiri wa ndege, lakini kama ingetumia usafiri wa gari, ingekuwa changamoto zaidi.

Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) linataka angalau baada ya saa 72 timu inaweza kucheza mchezo mwingine wa mashindano kutoka ule uliopita ili kutoa muda wa wachezaji kupata mapumziko ya kutosha.

Kanuni hii imeibuka kutokana na mjadala mkubwa wa kimataifa kuhusu msongamano wa ratiba za mechi na athari zake kwa afya ya wachezaji. Katika miaka ya hivi karibuni, ongezeko la mashindano ya kimataifa na ya klabu limeongeza mzigo kwa wachezaji, jambo lililolazimisha wadau wa soka kuweka viwango vya chini vya mapumziko.

Kwa mujibu wa tamko rasmi la FIFA, kanuni hii inaeleza wazi kuwa mchezaji au timu haitakiwi kucheza mechi mbili mfululizo bila kupumzika kwa angalau saa 72 ambazo ni sawa na siku tatu kamili.

Zaidi ya hilo, FIFA inaeleza kuwa kanuni hii imekubaliwa kwa pamoja kati yake na vyama vya wachezaji duniani.

Makubaliano haya yanaipa uzito mkubwa kanuni hii, kwani siyo tu pendekezo la upande mmoja bali ni mwafaka wa wadau wakuu wa mchezo.

Kwa mantiki hiyo, saa 72 zinachukuliwa kama kiwango cha chini kinachopaswa kuzingatiwa katika upangaji wa ratiba za mashindano.

Katika mwongozo huo huo, FIFA inaongeza mapumziko hayo yanapaswa kuendana na ratiba za timu husika.

Hii ina maana utekelezaji wa kanuni unaruhusu kubadilika kulingana na mazingira ya mashindano.

Kanuni ya saa 72 pia haiji peke yake, bali ni sehemu ya mfumo mpana wa kulinda wachezaji. FIFA inaelekeza pia kuwepo kwa mapumziko mengine, ikiwemo siku moja ya mapumziko kwa wiki na angalau siku 21 za mapumziko mwisho wa msimu.

Haya yote yanaonesha kuwa kanuni hii ni sehemu ya sera kubwa ya kusimamia afya na ustawi wa wachezaji katika soka la kisasa.

Katika utekelezaji wake, kanuni hii inahusisha pia kuzingatia mambo kama safari ndefu za kimataifa na hali ya hewa.

FIFA inaeleza kuwa upangaji wa ratiba unapaswa kuzingatia mazingira haya ili kuhakikisha kuwa muda wa mapumziko unakuwa na maana halisi kwa wachezaji.

Hii inaifanya kanuni ya saa 72 kuwa siyo tu namba, bali sehemu ya mfumo wa kitaalamu wa usimamizi wa mchezo.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alikiri ugumu wa ratiba hiyo ya mechi zao, akisema baada ya mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar uongozi wa klabu yao utakaa na kufanya tathimini kisha kutoa tamko rasmi.

“Kuna hiyo changamoto ya masaa kutotimia kwenye mechi za Yanga, na hii sio siasa, na hayo masaa 72 ni kwa kima cha chini na haya yote yanaletwa kwa lengo la kuwalinda wachezaji wasipate shida ya afya,” alisema Kamwe.

“Yanga kwa sasa hatutaki kulalamika, tumepanga kucheza hizi mechi licha ya hizo changamoto, tumemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi na tunakwenda kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar na tutakuwa tumemaliza mzunguko wa kwanza na kucheza mechi moja ya mzunguko wa pili, tukimaliza mchezo wa Mtibwa Sugar tutakutana na kufanya tathimini.

“Ndani ya hiyo tathimini ndiyo tutaangalia wapi tulikosea na wapi kuna shida na kuanzia hapo sasa ndiyo tutatoa tamko rasmi, niwaombe Wanayanga wakati huu tujikite kwanza kucheza hizi mechi, uongozi wa klabu yao ni makini na unafuatilia kila kitu kwa ukubwa.

“Huko nyuma wakati kama huu tulikuwa nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya waliokuwa wanaongoza ligi wakati huo Simba lakini sasa sisi ndio tupo juu kwa tofauti kama hiyo, niwaombe hili tuliache kwanza tutalizungumza hapo mbele baada ya mchezo wetu unaofuata.”€

Akizungumzia hilo, Dokta Juma Sufiani ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha madaktari wa Tiba za Wanamichezo TanzaniA (TASMA), alisema kama kuna timu inacheza mchezo mmoja kwenda mwingine chini ya saa 72, hiyo ni hatari kwa afya za wachezaji na ni rahisi kuweza kupata uchovu na baadaye kuumia.

“Unajua kanuni zetu hapa nchini tunazichukua kutoka FIFA na CAF, sasa wenzetu kule wamepiga hatua kidogo wanatumia usafiri wa kisasa zaidi, huku kwetu ni tofauti miundombinu yetu ni migumu kidogo sasa kama kuna timu kama ambavyo unasema inacheza mechi moja kwenda nyingine chini ya saa 72 hiyo ni hatari kwa wachezaji,” alisema Sufian ambaye ni daktari mkongwe wa tiba za wanamichezo nchini.

“Unaweza kuangalia timu imecheza kule Namungo mkoani Lindi, baada ya mchezo inasafiri kwa basi inakwenda Kigoma kucheza mchezo mwingine, vipi kama inakutana na ratiba ya muda kutotimia saa 72 hali itakuwaje, hata kama inatumia ndege italazimika kukaa uwanja wa ndege masaa mawili kusubiri safari bado kuna muda wa safari yenyewe, ni gharama sana kuwa na ndege ya kukodi, timu nyingi zinatumia ndege za biashara.

“Madhara yake ni makubwa sana hasa kwa wachezaji ambao kwa ratiba ya namna hiyo baadhi yao watapata uchovu wa misuli, utaona mchezaji umakini wake unapungua uwanjani anaweza kuingia sehemu ambayo hakutakiwa kufanya na baadaye anaumia, kwahiyo waathirika wakubwa wanakuwa wachezaji.”

Akizungumzia idadi kubwa ya majeruhi inayoikumba Yanga na suluhisho lake, Dr. Robert Kamau ambaye amewahi kufanya kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na sasa makazi yake Hispania, alisema:

“Kwanza kabisa, ni muhimu kuelewa kuwa mlipuko huu wa majeraha hautokei kwa bahati mbaya tu. Kuna sababu nyingi zinazochangia wachezaji kukumbwa na majeraha mara kwa mara.

“Sababu za ndani ni muhimu. Wachezaji wanapofanya mazoezi kupita kiasi au kushiriki mechi nyingi bila muda wa kutosha wa kupumzika, misuli na ‘tendon’ zinabeba mzigo mkubwa zaidi, jambo linalosababisha kuvunjika kwa nyuzi za misuli. Wengine wana historia ya majeraha ya zamani na pale wanapokumbana na mazoezi mengi au mechi mfululizo huwa kunakuwa na hatari kubwa sana.”

Kwa sasa Yanga ina wachezaji nane watakaokosekana katika mechi ijayo dhidi ya Mtibwa Sugar kutokana na majeraha na wapo walioumia hivi karibuni ikihusishwa na kucheza mfululizo ambao ni Ibrahim Abdullah ‘Bacca’, Dickson Job, Chadrack Boka, Laurindo Aurelio ‘Depu’, Edmund John, Israel Mwenda na Prince Dube, huku Clement Mzize akiumia muda mrefu.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Cornel Barnabas, alipotafutwa kuzungumzia hilo, alisema: “Hayo mambo kuhusu ratiba ningeomba umtafute Boimanda (Karim), yeye ndiye anatakiwa kuyazungumzia.”€

Alipotafutwa Karim Boimanda ambaye ni Ofisa Habari wa TPLB, simu yake ya mkononi iliita bila ya kupokewa.