Serikali za EAC zashinikizwa kugawa pedi bure, kuondoa tozo

Dar es Salaam. Serikali za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimetakiwa kupitia upya sera na mifumo ya kodi ili kuhakikisha upatikanaji wa taulo za kike (pedi) unakuwa rahisi au bure, hatua itakayosaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wasichana hasa walioko vijijini na familia zenye kipato duni.

Kukosekana kwa taulo za kike, imesababisha baadhi ya wasichana kutumia pedi moja kutwa au zaidi ya siku moja, migomba au hata soksi ili kujisitiri, huku wengine wakifanya maamuzi ya kubeba ujauzito ili wasione hedhi kwa miezi tisa.

Hayo yamezungumzwa jana Alhamisi, Machi 19 na wabunge wa EALA, viongozi wa vijana, mashirika ya kiraia, wadau wa afya na wanaharakati wakati wa kufunga mkutano wa siku mbili wa maboresho ya Sera ya Vijana 2025-2030.

Suala hilo alipoulizwa Mganga Mkuu wa Serikali amesema, “Suala la kodi liko Wizara ya Fedha kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) watakapokamilisha taratibu zao ndio watatujulisha sisi.”

Katika mjadala huo, Wakili Denis Bwana kutoka Shirika la Eannaso, amesema ipo haja ya kubadili mtazamo wa sera za kodi kwa bidhaa za hedhi, akisisitiza kuwa hedhi si jambo la hiari hivyo haipaswi kubeba mzigo wa kifedha kwa msichana.

“Mtoto wa kike hawezi kuchagua kupata hedhi. Ni hali ya kibaolojia. Kwa nini basi alazimike kulipia jambo ambalo haliko chini ya uamuzi wake? Wakati huohuo, bidhaa kama kondomu zinatolewa bure ilhali matumizi yake ni ya hiari,” amesema.

Ameongeza kuwa sera mpya zinapaswa kulenga kumsaidia msichana wa pembezoni asiingie kwenye vitendo hatarishi kama ngono za mapema au mimba za utotoni kwa ajili ya kujikimu kupata fedha za kununua pedi.

Kwa mujibu wa Bwana, nchi za EAC zinapaswa pia kuhamasisha uwekezaji wa ndani katika uzalishaji wa pedi ili kupunguza gharama, akitoa mfano wa jinsi bei za barakoa zilivyoshuka wakati wa janga la UVIKO-19 baada ya uzalishaji kuongezeka.

“Serikali zinaweza kutoa vivutio kwa wawekezaji kama ilivyo kwenye sekta nyingine. Tukizalisha pedi ndani ya nchi, bei zitashuka na upatikanaji utaongezeka,” amesema.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Vijana kuhusu Afya ya Uzazi Leticia Mswaki amesema uzoefu wa moja kwa moja unaonyesha ukubwa wa changamoto hiyo, akieleza kuwa wasichana wengi hulazimika kutumia njia zisizo salama wakati wa hedhi kutokana na kukosa pedi.

“Kuna wanaotumia pedi moja kwa siku nne, wengine hutumia migomba au hata soksi ili kujisitiri. Hili si jambo la kawaida, linapaswa kupewa uzito wake,” amesema.

Ameshauri serikali kuanza kwa kugawa bure taulo za kike mashuleni, ambako kuna idadi kubwa ya wasichana, huku ikitengeneza mifumo ya kuwafikia wale walio nje ya mfumo wa elimu.

“Wasichana wengi hukosa vipindi au kuacha shule kabisa kwa sababu ya aibu na ukosefu wa pedi. Tukizitoa bure mashuleni, tutasaidia kuongeza utulivu darasani na usawa wa kielimu kati ya wasichana na wavulana,” ameongeza.

Mwakilishi wa vijana kutoka Kenya, Amina Boru, amesema changamoto hiyo si ya nchi moja bali ni ya kikanda, akieleza kuwa baadhi ya wasichana nchini kwake hulazimika kutumia vitambaa au njia hatarishi kama kuchimba mashimo ardhini ili kujisitiri.

Ameeleza kuwa ingawa jitihada zimefanyika kuhamasisha matumizi ya pedi zinazofuliwa, bado kuna changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mengi, hali inayoweza kuongeza hatari ya maambukizi.

“Bila maji ya kutosha, hata hizi pedi za kufua zinakuwa changamoto. Ndiyo maana tunasisitiza serikali kufadhili upatikanaji wa pedi mashuleni kama kipaumbele cha haraka,” amesema.

Mratibu wa EA Youth Alliance, Elizabeth Kiburo amesema umasikini ni chanzo kikuu kinachochochea wasichana kuingia kwenye ndoa au mahusiano ya mapema wakikimbia gharama za kujisitiri wakati wa hedhi.

“Tatizo hili lina mizizi ya kiuchumi. Msichana anapokosa pedi, anaweza kuona ndoa au mahusiano kama njia ya kujikimu. Serikali lazima iingilie kati,” amesema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Vijana wa Afrika Mashariki, Irene Kitoti, amesisitiza umuhimu wa sera za kikanda kuhakikisha taulo za kike zinapatikana bure kwa wasichana wote, hasa wa vijijini.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza mahudhurio shuleni, kuimarisha kujiamini kwa wasichana na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa muda mrefu.

“Msichana akiwa na uhakika wa kupata pedi, anakuwa na utulivu wa kusoma na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo,” amesema.

Aidha, amependekeza kuwepo kwa sera rafiki za mazingira ya kazi na elimu, ikiwamo uwezekano wa mapumziko maalumu kwa wanawake wanaopata maumivu makali wakati wa hedhi, akitoa mfano wa baadhi ya nchi zilizoanza kutekeleza utaratibu huo.

Wadau hao pia wametoa wito kwa vijana kushiriki kikamilifu katika kufuatilia na kuchambua sera za EAC ili kuhakikisha mahitaji yao yanazingatiwa.

Wamesema ni muhimu kwa vijana kuvuka mipaka ya kitaifa na kushirikiana kikanda katika kutoa mawazo na kushinikiza utekelezaji wa sera zinazolenga kuboresha afya ya uzazi na haki za wasichana.

Mapendekezo hayo yanaibuka wakati Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiendelea kuandaa na kutekeleza sera za vijana na afya ya uzazi kwa kipindi cha 2025–2030, zikilenga kupunguza changamoto za kiafya na kijamii zinazowakabili vijana, hususan wasichana.

Iwapo yatatekelezwa, wadau wanaamini hatua hizo zitasaidia si tu kulinda heshima ya mtoto wa kike, bali pia kuongeza usawa wa kijinsia, kuboresha elimu na kuchochea maendeleo endelevu katika ukanda wa Afrika Mashariki.