WAKATI za Yanga na Simba zikiwa miongoni mwa timu shiriki za Kombe La Muungano 2026, imeelezwa uwepo wao utaleta ushindani na kuongeza hadhi kwa mashindano hayo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Hussein Ahmada Vuai alisema ushiriki wa timu hizo utazidi kuleta hamasa kwa mashabiki kufika viwanjani kushuhudia burudani ya watani ya wa jadi.
Michuano hiyo iliyopangwa kuanza Aprili 21 hadi 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, itashirikisha timu nane ambazo ni bingwa mtetezi Yanga, Simba, Azam na Singida Black Stars zote kutoka Tanzania Bara. Kwa upande wa Zanzibar ni KVZ, Muembe Makumbi, Mlandege na Mafunzo.
Ikumbukwe, wakati Simba inachukua ubingwa wa michuano hiyo mwaka 2024, Yanga haikushikiri, huku pia Yanga ilipotwaa ubingwa mwaka 2025, Simba haikushiriki.
Kwa msimu huu, timu hizo zote zinakwenda kushiriki.
Ahmada alisema sababu ya Simba na Yanga kupishana ushiriki katika misimu miwili iliyopita, haikuwa uamuzi wao binafsi kwani zilikuwa na uwakilishi wa mashindano ya kimataifa, hivyo hawakutaka kuzipa ugumu.
Aliongeza, kwa msimu huu baada ya timu hizo kuishia makundi katika mashindano ya kimataifa, imetoa nafasi ya kushiriki kwenye mashindano haya moja kwa moja.
“Msimu huu mashindano hayo yatakuwa makubwa na yenye hadhi kwa mpira wa Tanzania na kutoa fursa na nafasi ya kukuza ligi zote mbili ya Zanzibar na Tanzania Bara,” alisema.
Katika hatua nyingine, Ahmada alisema kwa sasa vikao vya maandalizi ya mashindano hayo vinaendelea na wanajadili masuala mbalimbali ikiwamo upangaji wa makundi na ratiba inayotarajiwa kutolewa mwanzoni mwa mwezi Aprili.
Mashindano hayo yalirejea mwaka 2024 ambapo Simba ilibeba ubingwa kwa kuifunga Azam bao 1-0, katika fainali iliyochezwa Aprili 27, 2024 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja huku timu nne zikishiriki ambapo mbali na Simba na Azam kutoka Tanzania Bara, zilikuwepo KVZ na KMKM za Zanzibar.
Mwaka 2024, Yanga ilibeba ubingwa kwa kuifunga JKU bao 1-0 katika fainali iliyochezwa Mei Mosi, 2025 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.