Kanisa Katoliki, uteuzi na usimikaji wa askofu ni mchakato wa kina unaozingatia misingi ya kiroho, nidhamu ya kanisa na utaratibu wa kimamlaka. Hatua hizi huanzia ngazi ya chini kabisa ya dayosisi hadi kufikia mamlaka ya juu kabisa ya kanisa iliyoko Vatican City.
Mchakato huanza pale nafasi ya askofu inapokuwa wazi, iwe ni kutokana na kifo, kustaafu au uhamisho. Viongozi wa kanisa katika eneo husika huanza kukusanya taarifa na kupendekeza majina ya mapadri au maaskofu wanaoonekana kuwa na sifa stahiki. Katika hatua hii, maoni hukusanywa kwa siri kubwa kutoka kwa maaskofu, mapadri na hata baadhi ya waumini, ili kuhakikisha anayependekezwa ana maadili bora, elimu ya theolojia na uwezo wa uongozi wa kiroho.

Majina hayo hupelekwa Vatican City kupitia mwakilishi wa Papa anayejulikana kama Nuncio. Huko, huchambuliwa na idara maalum ya uteuzi wa maaskofu kabla ya kuwasilishwa kwa Papa, ambaye ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kumteua askofu.

Baada ya uteuzi kufanywa, jina la askofu mpya hutangazwa rasmi. Mteule hupaswa kukubali wito huo, kisha huanza maandalizi ya kiroho kama vile sala, mafungo na mafundisho maalum kabla ya kusimikwa.
Ibada ya kusimikwa hufanyika katika misa takatifu, ambapo maaskofu wengine huweka mikono juu ya kichwa cha mteule kama ishara ya kumpa mamlaka ya kiroho. Katika ibada hiyo, askofu mpya hupokea alama muhimu za uaskofu kama pete (ishara ya uaminifu kwa kanisa), fimbo ya kichungaji (crosier) na kofia maalum (mitre).
Anachokabidhiwa kutoka Vatican
Mbali na alama hizo za ibada, askofu mpya waKatoliki hukabidhiwa pia nyaraka rasmi kutoka Vatican City zinazoidhinisha uteuzi wake. Nyaraka hiyo huitwa “Apostolic Mandate” au “Bull” ya Papa, ambayo hubeba muhuri na mamlaka ya Papa.
Hati hii ni uthibitisho rasmi kwamba uteuzi wake umetolewa kwa mamlaka ya juu ya kanisa na inampa haki ya kuongoza dayosisi husika. Mara nyingi, hati hiyo husomwa hadharani wakati wa ibada ya kusimikwa ili kuonesha uhalali wa uteuzi huo mbele ya waumini.
Kwa baadhi ya maaskofu wakuu (Archbishops), pia hupokea Pallium vazi maalum la kitambaa cheupe chenye alama za misalaba, ambalo hutumwa moja kwa moja kutoka Vatican City kama ishara ya ushirika wao wa karibu na Papa na mamlaka yao juu ya majimbo ya kanisa.
Kwa ujumla, kuwa askofu katika Katoliki si tukio la ghafla, bali ni mchakato unaohusisha uchunguzi wa kina, maamuzi ya juu ya kanisa na maandalizi ya kiroho. Nyaraka na alama anazokabidhiwa kutoka Vatican City ndizo zinazothibitisha rasmi mamlaka yake na kuanza safari yake ya kuongoza waumini katika imani.