Tsh 36,000 Kuingia Kariakoo? Taharuki Yazuka Kuhusu Tozo Zisizotangazwa Rasmi

 Waendesha bajaji na bodaboda wanaofanya kazi katika eneo la Kati ya Jiji la Dar es Salaam (CBD) wamedai kulazimishwa kulipa Tsh 36,000 kwa kibali cha kuingia katikati ya jiji, licha ya kutokuwepo kwa tangazo rasmi au kanuni zilizochapishwa kisheria (gazeti la Serikali) kutoka Halmashauri ya Jiji.

Taarifa hizo zimeibuka baada ya madereva kadhaa kulifikia gazeti hili wakilalamikia kutozwa faini papo kwa papo na kuzuiwa kuingia katika maeneo muhimu ya kibiashara ikiwemo Posta na Kariakoo. Mmoja wa madereva hao, aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa kuhofia hatua za kinidhamu, alionyesha risiti kuthibitisha malipo ya kibali alichodai ni cha lazima kuingia CBD. “Tunaambiwa bila kulipa hatuwezi kuingia. Ukikataa, unapigwa faini au unarudishwa,” alisema.

Eneo la CBD ndilo kitovu cha biashara cha Jiji la Dar es Salaam, likihudumia zaidi ya watu 300,000 kwa siku. Inakadiriwa kuwa asilimia 75 ya watu hao huelekea Kariakoo, ambako zaidi ya wafanyabiashara 9,000—kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) za mwaka 2022—wanategemea mzunguko huo wa wateja kujipatia kipato.

Bodaboda na bajaji zimekuwa mhimili wa usafiri wa “mwisho wa safari” hasa kwa wanunuzi wanaofanya manunuzi makubwa yasiyoweza kubebwa ndani ya daladala. Madereva wanasema tozo hizo zimeanza kupunguza mapato yao ya saa za asubuhi, ambazo ndizo huchangia sehemu kubwa ya kipato chao cha kila siku.

Wadau wa sekta ya usafiri wanaonya kuwa utozwaji wa gharama kwa ghafla, bila maelezo rasmi au msingi wa kisheria, unaweza kuvuruga mtiririko wa usafiri, kuongeza gharama kwa watumiaji na kutikisa mfumo wa biashara usio rasmi unaoendesha uchumi wa Kariakoo.

Hadi gazeti hili linaenda mitamboni, mamlaka za jiji hazikuwa zimetoa tamko rasmi kuhusiana na tuhuma hizo.