Wakati vita ya Marekani, Israel dhidi ya Iran ikiendelea kushika kasi kwa takribani wiki ya tatu sasa, moja ya changamoto kubwa ambayo iatajwa kuikumba dunia siku za usoni ni upatikanaji wa mbolea kwa wakulima.
Athari za vita hivyo, inatoa mwangwi kwa wakulima hapa nchini kujiweka mguu sawa ili kukabiliana na changamoto hiyo, ambapo Tanzania ni miongoni mwa wanufaika wa mbolea hiyo.
Mlango wa Bahari wa Hormuz, ambao kwa sasa umeathiriwa na hatua za Iran, hupitisha takribani asilimia 30 ya mbolea inayouzwa duniani.
Nchi za Ghuba ni wazalishaji wakubwa wa mbolea aina ya ammonia na urea.
Taarifa zinaonyesha kuwa vita hiyo inaweza kuhatarisha hadi asilimia 65 hadi 70 ya usambazaji wa urea duniani huku bei tayari zikiwa zimeongezeka kwa kati ya asilimia 30 hadi 40.
Mchumi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Maximo Torero, amesema hali hiyo itaathiri uzalishaji wa mazao, ikiwemo nafaka muhimu na chakula cha mifugo, jambo litakaloathiri pia bidhaa kama maziwa na nyama.
“Endapo hali itaendelea hata kwa wiki chache zijazo, uzalishaji wa chakula utapungua kwa kiasi kikubwa,” amesema Torero.
Iran imeshambulia kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Kuwait huku Israel ikimuua msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC), ikiwa ni mwendelezo wa vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran vinavyoonyesha kutokuwa na dalili ya kumalizika.
Wakati huohuo, Israel iliahidi kuepuka mashambulizi zaidi kwenye eneo la gesi la South Pars nchini Iran, siku moja baada ya Iran kulipiza kisasi kwa kushambulia miundombinu ya nishati nchini Qatar, tukio lililosababisha uharibifu mkubwa unaotarajiwa kuathiri upatikanaji wa gesi asilia duniani kwa miaka kadhaa.
Bei ya mafuta ghafi aina ya Brent ilisalia katika kiwango cha takribani dola 110 kwa pipa, baada ya kupanda kwa kasi siku iliyotangulia kutokana na hofu ya kuvurugika kwa kiwango kikubwa kwa usambazaji wa nishati duniani, hali inayoweza kusababisha mshtuko wa uchumi wa dunia.
Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa hata kama vita hiyo itamalizika hivi karibuni, athari zake hazitaondoka haraka kutokana na uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya anga pamoja na kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz, ambao hupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa duniani.
Rais wa Marekani, Donald Trump, alirudia wito wake kwa washirika wakuu wa nchi hiyo kusaidia kulinda usalama wa meli zinazopita katika mlango huo muhimu wa usafirishaji, akieleza kuwa hawakushirikishwa wala kupewa taarifa kabla ya kuanza kwa vita hiyo.
Katika hatua ya pamoja, nchi za Germany, Uingereza, Ufaransa, Italia, Uholanzi, Japan, na Canada zimeahidi kushiriki katika juhudi za kuhakikisha usalama wa usafirishaji kupitia mlango huo wa bahari.
Hata hivyo, Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz amesisitiza kuwa ushiriki huo unategemea kwanza kusitishwa kwa mapigano.
Msemaji wa IRGC, Jenerali Ali Mohammad Naeini ameuawa kufuatia shambulizi la anga lililofanyika usiku huku Israel ikidai kuhusika na operesheni hiyo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, Naeini aliyekuwa pia naibu wa kitengo cha uhusiano wa umma ndani ya IRGC, amefariki katika shambulizi hilo lililotokea jijini Tehran.
Kifo chake kinatajwa kuwa pigo jingine kwa uongozi wa kijeshi wa Iran katika vita vinavyoendelea kati ya Iran dhidi ya Marekani na Israel, ambavyo tayari vimesababisha vifo vya maofisa kadhaa waandamizi wa nchi hiyo.
Taarifa zinaeleza kuwa shambulizi hilo limetokea saa chache baada ya Naeini kutoa kauli kali akionya kuhusu uwezo wa Iran kuendelea kujibu mashambulizi, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa mvutano katika eneo la Mashariki ya Kati.
Tukio hilo linaongeza presha katika mzozo huo unaoendelea huku wachambuzi wakionya kuwa kuuliwa kwa viongozi wa juu wa kijeshi kunaweza kuchochea hatua za kulipiza kisasi na kuongeza hatari ya vita kupanuka zaidi katika ukanda huo.
Wakati huo huo, Israel na Iran zimeendeleza mashambulizi mapya ambapo Iran imeshambulia kiwanda cha kusafisha mafuta cha Israel na kufuatia onyo la Trump kwa Israel kuepuka mashambulizi zaidi kwenye eneo la gesi la Iran wanaloshirikiana na Qatar.
Jeshi la Israel limesema limefanya mashambulizi mjini Tehran likilenga “miundombinu ya utawala wa kigaidi wa Iran,” bila kutoa maelezo ya kina. Kwa upande wake, Iran imerusha makombora kadhaa kuelekea Israel, hali iliyosababisha ving’ora vya tahadhari kulia katika jiji la Tel Aviv huku milipuko ya mifumo ya ulinzi wa anga ikisikika angani.
Tangu kuanza kwa mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran Februari 28, vita hiyo imesababisha vifo vya maelfu ya watu, wengi wao wakiwa Iran na Lebanon, huku pia ikisambaa katika Mashariki ya Kati na kuathiri uchumi wa dunia.
Katika tukio jingine, Falme za Kiarabu (UAE) zimeripoti tishio la shambulizi la kombora mapema Ijumaa, wakati Waislamu wakianza kusherehekea Eid al-Fitr baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Nchi ya Kuwait nayo imesema kiwanda chake cha kusafisha mafuta kilishambuliwa kwa kutumia droni.
Mashambulizi hayo yanafuatia siku kadhaa za Iran kushambulia miundombinu ya nishati katika eneo hilo, hali iliyotikisa masoko ya dunia.
Bei za nishati zilipanda Alhamisi baada ya Iran kujibu shambulizi la Israel kwenye uwanja mkubwa wa gesi kwa kulenga mji wa viwanda wa Ras Laffan nchini Qatar, unaochakata takribani asilimia 20 ya gesi asilia iliyoyeyushwa duniani. Uharibifu uliotokea unatajwa kuhitaji miaka kadhaa kurekebishwa.
Bandari kuu ya Saudi Arabia katika Bahari ya Shamu, ambayo imekuwa ikitumika kama njia mbadala ya kusafirisha mafuta kufuatia kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz, nayo ilishambuliwa Alhamisi.
Hata hivyo, bei za mafuta zilishuka Ijumaa baada ya mataifa ya Magharibi na Japan kujitolea kusaidia kuhakikisha usalama wa meli katika mlango huo muhimu wa usafirishaji, unaopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta ya dunia huku Marekani ikitangaza hatua za kuongeza uzalishaji wa mafuta.
Mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati yanaonyesha uwezo wa Iran kuendelea kusababisha athari kubwa licha ya mashambulizi ya Marekani na Israel, pamoja na udhaifu wa mifumo ya ulinzi wa anga kulinda rasilimali muhimu za nishati katika Ghuba.
Rais Trump, ambaye anakabiliwa na shinikizo la kisiasa kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula mwezi Novemba, amewakosoa washirika wake kwa kuchukua tahadhari katika kusaidia kulinda njia hiyo muhimu ya usafirishaji.
Amesema pia kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, hatarudia mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati. “Nilimwambia, ‘Usifanye hivyo’ na hatofanya,” Trump amewaambia waandishi wa habari.
Hata hivyo, Netanyahu baadaye amesema Israel ilichukua hatua peke yake katika kushambulia kituo cha gesi cha South Pars nchini Iran.
Mbolea, chakula kupanda bei
Wakati huo huo, nchi zinazoendelea zinakabiliwa na hatari ya kupanda kwa bei ya chakula kutokana na usumbufu katika usafirishaji wa mbolea na kupanda kwa bei ya nishati kufuatia vita inayoendelea Iran.
Hali hiyo inakuja wakati nchi nyingi zilikuwa zimeanza kuimarika kiuchumi baada ya kukumbwa na misukosuko wakati wa janga la Uviko-19 na vita ya Ukraine na Russia, ambayo ilisababisha kuyumba kwa masoko ya chakula, mafuta, na fedha.
Sasa, mzozo wa Iran unatishia kufuta mafanikio hayo na kuziacha familia zikihangaika kujikimu kwa chakula, miongoni mwa athari nyingine zinazotarajiwa kujitokeza.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, Rais wa Benki ya Ulaya ya Ujenzi na Maendeleo (EBRD), Odile Renaud-Basso, amesema hali hiyo inaweza kuwa na athari kubwa kwa bei za chakula kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa ripoti ya Moody’s Ratings, katika nchi nyingi zilizoendelea, chakula na mafuta huchangia chini ya robo ya mfumuko wa bei, lakini katika nchi zinazoendelea hufikia kati ya asilimia 30 hadi 50. Hali hiyo huzifanya nchi hizo kuwa hatarini zaidi kwa mabadiliko ya bei yanayotokana na masoko ya nje.
Moja ya changamoto kubwa ni upatikanaji wa mbolea. Mlango wa Bahari wa Hormuz, ambao kwa sasa umeathiriwa na hatua za Iran, hupitisha takribani asilimia 30 ya mbolea inayouzwa duniani. Nchi za Ghuba ni wazalishaji wakubwa wa mbolea aina ya ammonia na urea.
Taarifa zinaonyesha kuwa vita hiyo inaweza kuhatarisha hadi asilimia 65 hadi 70 ya usambazaji wa urea duniani huku bei tayari zikiwa zimeongezeka kwa kati ya asilimia 30 hadi 40.
Mchumi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Maximo Torero, amesema hali hiyo itaathiri uzalishaji wa mazao, ikiwemo nafaka muhimu na chakula cha mifugo, jambo litakaloathiri pia bidhaa kama maziwa na nyama.
“Endapo hali itaendelea hata kwa wiki chache zijazo, uzalishaji wa chakula utapungua kwa kiasi kikubwa,” amesema Torero.
