Kibaha. Katika hatua inayolenga kuleta mapinduzi ya huduma za afya zinazozingatia faragha na heshima ya mgonjwa, Waislamu wa dhehebu la Ansar Sunnah mkoani Pwani wametangaza mpango wa kujenga hospitali ya kisasa itakayotoa huduma kwa kuzingatia jinsia ya mgonjwa.
Tangazo hilo limetolewa leo Ijumaa Machi 20, 2026, wakati wa swala ya Eid El Fitr iliyofanyika katika eneo la stendi ya zamani ya mabasi Kibaha, ambapo waumini walikusanyika kusherehekea sikukuu hiyo.
Akizungumza baada ya swala hiyo, kiongozi wa Darul Arqam Learning Centre, Mohammed Tundu Mshanaamesema hospitali hiyo itakuwa na mfumo maalum wa utoaji huduma unaolenga kulinda faragha ya wagonjwa kwa kuhakikisha wanawake wanahudumiwa na madaktari wa kike na wanaume wanahudumiwa na madaktari wa kiume.
Amesema utaratibu huo unalenga kuondoa aibu na changamoto ya kisaikolojia inayowakumba baadhi ya wagonjwa, hasa wanapolazimika kuelezea matatizo yao ya kiafya kwa madaktari wa jinsia tofauti.
“Tunataka kujenga mazingira rafiki ya matibabu ambapo kila mgonjwa atajisikia huru na salama. Mwanamke atahudumiwa na daktari mwanamke na mwanaume vivyo hivyo, jambo litakaloongeza faragha na kuimarisha uaminifu,” amesema Mshana.
Mbali na hospitali, mradi huo mkubwa wenye thamani ya Sh5.5 bilioni pia utahusisha ujenzi wa shule kuanzia ngazi ya awali hadi chuo kikuu, pamoja na msikiti mkubwa, hatua inayolenga kuimarisha sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Mshana, ujenzi wa miundombinu hiyo unatarajiwa kuanza Januari 2027 katika eneo la Boko, Kibaha, ambapo tayari eneo la zaidi ya ekari 11 limeshanunuliwa na taratibu za umiliki zimekamilika.
Baadhi ya waumini waliohudhuria swala hiyo wamepongeza mpango huo wakisema utaleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za afya, hasa kwa kuzingatia mahitaji ya kijinsia na kiimani.
Mkazi wa Kibaha, Swaumu Rashidi amesema mradi huo utawapa uhuru wagonjwa, hususan wanawake ambao mara nyingi hukumbana na changamoto ya kujieleza wanapopata huduma kutoka kwa madaktari wa jinsia tofauti.
Naye Sheila Mussa amesema uwekezaji huo ni wa mfano na unapaswa kuungwa mkono kwa kuwa unazingatia heshima ya mgonjwa pamoja na misingi ya dini na mila.
Kwa miaka ya hivi karibuni, Waislamu wa dhehebu la Ansar Sunnah wameendelea kujihusisha na miradi ya kijamii ikiwamo elimu na afya, wakilenga kuinua ustawi wa jamii na kuchochea maendeleo endelevu.
