Shinyanga. Wakati Tanzania ikielekea kuadhimisha Siku ya Misitu Duniani inayofanyika kila ifikapo Machi 21 kila mwaka imebainishwa ukanda wa Tanzania bara zaidi ya hekta 400,000 za misitu hupotea kutokana na uharibifu wa mazingira ikiwamo ya ukataji miti hovyo.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa Machi 20, 2026 na Ofisa Misitu Mwandamizi, Mkuu wa oparesheni Kanda ya Magharibi Shadrack Msilu.
Amesema kutokana na hilo, Wakala wa huduma za misitu Tanzania, Kanda ya Magharibi ambayo inahusisha mikoa ya Shinyanga, Tabora, Katavi na Kigoma, imeadhimisha siku hiyo leo kwa kupanda miti 350 katika Shule ya Sekondari ya wasichana Shinyanga.
“Kwa mwaka Tanzania Bara tunapoteza hekta 469,000 za misitu na hii inasabishwa na uharibifu wa mazingira kama ukataji miti kwa ajili ya kuni na uvunaji wa mkaa haramu,” amesema Msilu.
Hata hivyo, amesema serikali inaendelea kutoa elimu ya utunzaji misitu ili kupunguza kiwango cha kupoteza misitu na kulinda mazao yatokanayo na miti.
Naye Mkuu wa shule ya Sekondari ya wasichana Shinyanga, Nurat Kamuntu amesema awali shule hiyo ilikuwa na mti mmoja tu ambao ni wa asili, ulitumika kama sehemu ya kuegesha baiskeli na magari na muda mwingine kivuli chake kilitumika kupumzikia,
“Awali tulikuwa na miti mmoja tu wa asili ambao ulitumika kama sehemu ya kuegeshea magari na baiskeli pamoja na sehemu ya kupumzikia, nitoe shukrani kwa TFS wilaya kuifanya shule hii kuwa ya kijani, imekuwa ikileta miti kupandwa katika shule hii na sasa tuna miti ya kupandwa zaidi ya 3,000,” amesema Nurat.
Kiongozi wa klabu ya mazingira kutoka shule ya wasichana ya Sekondari Shinyanga, Kabula Bundala ametaja tatizo linaloikumba shule hiyo na kusababisha ustawi mbaya wa miti ni ardhi mbaya.
“Changamoto zilizopo ni pamoja na sehemu ya ardhi ya shule hairuhusu miti kustawi, pia kutokuwepo kwa uzio katika shule hii, kunasababisha mifugo kuvuka mipaka ya shule na kuharibu miti iliyopandwa sambamba na uhaba wa maji ya kumwagilia miti tunaomba tujengewe kisima cha maji” amesema Kabula.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga, Said Kitinga amesema tayari wameweka utaratibu wa upandaji miti kwa kila kaya.
“Changamoto mlizosema tumezichukua na tunakwenda kuzifanyia kazi, pia katika wilaya ya Shinyanga kuna utaratibu wa kila mwananchi anayepewa eneo la kujenga nyumba lazima apewe miti isiyopungua kumi kwa ajili ya kupanda katika eneo lake,” amesema Kitinga.
