Alhaj Mavumbi akemea ukatili kwa watoto ataka wananchi kuchukua hatua

Tabora. Waumini wa Dini ya Kiislamu mkoani Tabora wametakiwa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kuwapa fursa ya kufikia ndoto zao na kuishi katika mazingira salama.

Wito huo umetolewa leo Jumamosi Machi 21, 2026 na Sheikh wa Mkoa wa Tabora, Alhajji Sheikh Ibrahim Mavumbi alipokuwa akitoa hotuba ya Idd El-Fitr baada ya swala iliyofanyika katika Msikiti wa Mabatini, Kata ya Mbugani, Manispaa ya Tabora.

Sheikh Mavumbi amesema ulinzi wa mtoto ni sehemu ya mafundisho ya dini ya Kiislam huku akisisitiza kuwa wazazi na walezi wanapaswa kuwajibika kikamilifu kuhakikisha watoto wanakuwa salama na wanalelewa katika misingi bora ya maadili.

“Ni maelekezo ya Mtume Muhammad (S.A.W) kwamba tusimamie maadili ya watoto wetu na tuwalinde dhidi ya ukatili. Hivi sasa tunashuhudia matukio mengi ya watoto kutupwa na kujeruhiwa, hali inayotokana na wazazi kupuuza wajibu wao,” amesema.

Amesema kila mzazi au mlezi anapaswa kusimama katika nafasi yake kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi, zikiwemo elimu, afya bora na malezi stahiki, badala ya kuwaacha katika mazingira hatarishi.

“Tunashuhudia watoto wakichomwa moto, kunyimwa chakula na kutelekezwa, hasa yatima. Haya ni matendo yasiyokubalika na ni dhambi kubwa kumuacha mtoto ateseke,” ameongeza.

Aidha, amewataka waumini hao na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuliombea Taifa ili kudumisha amani na utulivu, akieleza kuwa hali hiyo ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi.

“Amani na utulivu ni mzizi wa maendeleo ya taifa lolote. Huwezi kufanya kazi wala kuhifadhi mali kama hakuna amani. Tunapaswa kuilinda kama tunu yetu,” amesema.

Kwa upande wake, mkazi wa Tabora, Juma Maulidi amesema yuko tayari kutekeleza ushauri huo, akibainisha kuwa kwa sasa analea watoto watatu yatima na yuko tayari kuongeza wengine iwapo atapata uwezo.

“Ningekuwa na uwezo mkubwa zaidi ningependa kulea watoto wengi zaidi kwa sababu ni ibada. Nitaendelea kufanya hivyo kadiri nitakavyoweza,” amesema.

Naye Salma Shabani ameitaka Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wanaobainika kufanya ukatili kwa watoto, akisema adhabu kali inaweza kusaidia kupunguza vitendo hivyo.

“Ni muhimu Serikali iweke adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine. Kuna matukio ya kutupa watoto na hata unyanyasaji unaofanywa na baadhi ya wazazi wenyewe, hali inayotia hofu katika jamii,” amesema.