Simiyu. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu kimepata pigo kufuatia kifo cha Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani humo, Mariam Manyangu, aliyefariki dunia leo Jumamosi Machi 21, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Simiyu, Lumen Ngunda, marehemu amefariki dunia akiwa jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa chama kimepokea kwa masikitiko makubwa kifo hicho, kikimtaja Manyangu kuwa kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha umoja wa wanawake ndani ya chama na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii mkoani humo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na wanachama wa UWT, akiwataka kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki cha maombolezo.
Baadhi ya wanachama wa UWT mkoa huo wameeleza kusikitishwa na kifo hicho, wakimtaja kuwa alikuwa kiungo muhimu katika kuwaunganisha wanawake na kuhamasisha maendeleo.
Rehema Magesa wa Bariadi amesema marehemu alikuwa karibu na wanachama na alisikiliza changamoto zao, huku Aneta Emanuel wa Maswa akimuelezea kama mfano wa uongozi bora kwa wanawake.
Kwa upande wake, Neema Nyambalya wa Itilima amesema wanawake wa Simiyu wamepoteza mlezi na mshauri aliyewahamasisha kushiriki shughuli za kijamii na kisiasa.
Kifo cha Manyangu kinakuja siku chache baada ya CCM kumpoteza aliyekuwa Mwenyekiti wa chama wilaya ya Itilima, Mhuli Ngeleja, aliyefariki dunia Machi 18, 2026.
Taarifa zaidi kuhusu taratibu za mazishi zitatolewa na familia pamoja na chama baada ya kukamilika kwa maandalizi.
