MAKIPA Djigui Diarra wa Yanga, Aishi Manula (Azam) na Mahamadou Tanja Djibrilla Kassali Djibo (Simba), wameendelea kuonyesha ubora katika mechi mbalimbali hasa za Ligi Kuu Bara, huku viwango vyao vikiwa ni msaada kwa timu zao.
Kwa jumla makipa hawa wameokoa hatari 16 zilizodhaniwa zingewanyima cleansheet na kuwaacha waliojaribu kuwafunga wakishika vichwa kutokana na ufundi wao wa kuokoa.
Ikiongoza msimamo wa ligi hadi sasa na pointi 37 baada ya mechi 15, Yanga ndiyo inayoongoza kwa kuruhusu mabao machache (2), huku Azam yenye pointi 29 ikifuatia mabao manne na Simba yenye pointi 28 baada ya mechi 13 imeruhusu sita hadi sasa.
Wakati timu hizo zikiwa zinafukuzana katika nafasi tatu bora za Ligi Kuu Bara, makipa wao wamekuwa wakifanya kazi kubwa kulinda nyavu zisitikiswe kutokana na ubora wao wanapokuwa golini na kwa viwango vyao wameziokoa timu zao katika hatari ambazo zilidhaniwa ni mabao.
Diarra aliyejiunga na Yanga Agosti 8, 2021, akitokea Stade Malien ya kwao Mali, ameendelea kuonyesha kiwango bora, huku akiwa ni sehemu pia ya mafanikio ya kikosi hicho kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa misimu minne mfululizo.
Kipa huyo ambaye kwa sasa ana ‘Clean Sheets’ 10 za Ligi Kuu, akibakisha saba tu kufikia za msimu wa 2024-2025 na alikuwa nazo 17, ameendelea kuibuka shujaa, kutokana na michomo ya hatari ‘Saves’, ambazo amekuwa akizifanya msimu huu.
Uhodari wa nyota huyo, uliisaidia Yanga kupata suluhu (0-0) dhidi ya TRA United, katika mechi kali ya Ligi Kuu iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Machi 18, 2026, kutokana na kuokoa hatari ya dakika ya mwishoni.
Kipa huyo aliinyima TRA United kuondoka na pointi tatu, baada ya kuokoa mkwaju wa nyota wa kikosi hicho, Mganda Khassimuh Mugoya, dakika ya 90+3, hivyo, kuzifanya timu hizo kugawana pointi mojamoja, katika mechi hiyo ya Ligi Kuu.
Katika mechi ya ‘Dar es Salaam Derby’, kati ya Yanga dhidi ya Azam iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Machi 15, 2026 na kuisha kwa suluhu (0-0), Diarra aliokoa shuti la hatari lililopigwa na Zidane Sereri, dakika ya 15 na kuliweka salama lango lake.
Licha ya Yanga kushinda mabao 3-0 dhidi ya Singida Black Stars, kwenye Uwanja wa Airtel, mjini Singida, Machi 5, 2026, lakini Diarra, aliokoa shuti la hatari, lililopigwa na beki wa kushoto wa timu hiyo, Mghana, Ibrahim Imoro, dakika ya 89.
Katika mechi ya ‘Kariakoo Derby’, iliyopigwa, Machi 1, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan, Complex, Zanzibar, Diarra, aliibuka shujaa kwa kuokoa michomo ya hatari na kuisaidia Yanga kutoka suluhu (0-0) dhidi ya watani zao Simba.
Kipa huyo aliokoa shuti la hatari lililotokana na mpira wa kona uliopigwa na Libasse Gueye dakika ya tatu, kisha akaokoa tena mpira uliopigwa dakika hiyo hiyo na kiungo mshambuliaji nyota, Inno Jospin Loemba, akizidi kuonyesha kiwango bora.
Dakika ya 13, Diarra akaokoa mkwaju mwingine wa hatari uliopigwa na winga, Alain Anicet Oura, kwa shuti kali ambalo alilitema kisha kumkuta kiungo mshambuliaji, Inno Jospin Loemba, ambaye hata hivyo, wakati anaupiga alikuwa ameotea.
Wakati Simba ikiamini huenda ingeibuka na ushindi katika mechi hiyo iliyojawa na matukio mengi, Diarra aliiweka tena Yanga katika nafasi nzuri, baada ya kuokoa shuti la Elie Mpanzu, dakika ya 90+3 na mechi hiyo kumalizika kwa suluhu (0-0). – 7
Ukiachana na Diarra, Aishi Manula aliyerejea Azam FC msimu huu baada ya kuondoka Simba, ameendeleza kiwango kizuri, akishirikiana na Zuberi Foba, wanaobadilishana mara kwa mara katika kikosi hicho cha Kocha, Mkongomani, Florent Ibenge.
Manula aliyeondoka Azam FC mwaka 2017, kisha kujiunga na Simba, amerejea tena ndani ya kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, ambapo hadi sasa ana ‘Clean Sheets’ sita za Ligi Kuu Bara, huku akiokoa baadhi ya michomo ya hatari.
Katika mechi ya Azam dhidi ya Yanga iliyoisha kwa suluhu (0-0), ikichezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Machi 15, 2026, Manula aliokoa mpira uliopigwa kwa kichwa na Laurindo Dilson Maria ‘Depu’, dakika ya 83, akipokea pasi nzuri ya Israel Mwenda.
Kama haitoshi, katika mechi ya Azam FC iliyoisha suluhu (0-0) pia dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons, Machi 5, 2026, iliyopigwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Manula aliokoa mchomo wa hatari uliopigwa na Neva Kaboma dakika ya 90+5.
Licha ya Azam kuifunga TRA United mabao 2-0, katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, Januari 29, 2026, lakini Manula aliokoa mashuti mawili ya hatari, la Khassimuh Mugoya, dakika ya 51 na Nasry Kombo, dakika ya 87 ambayo kama yangetinga nyavuni, basi ingekuwa sare.
Katika mechi ya ushindi wa Azam FC wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union, iliyopigwa pia Uwanja wa Azam Complex, Januari 17, 2026, Manula aliokoa shambulizi la mpira wa hatari uliopigwa na Athumani Masumbuko ‘Makambo’, dakika ya 85. Akalinda clean sheet yake.
Licha ya Azam kutengeneza mashambulizi ya hatari dhidi ya Singida Black Stars, katika mechi iliyoisha kwa suluhu (0-0), Desemba 3, 2025, Manula aliokoa mchomo wa hatari wa dakika ya 53, uliopigwa na kiungo mshambuliaji, Marouf Tchakei. -6
Kwa upande wa kipa, Mahamadou Tanja Djibrilla Kassali Djibo, aliyejiunga na Simba katika dirisha dogo la usajili Januari 2026, akitokea AS FAN Niamey ya kwao Niger, ameendeleza kiwango kizuri na kikosi hicho, baada ya Moussa Camara, kuendelea kuuguza majeraha.
Camara, aliyejiunga na Simba, Agosti 1, 2024, akitokea Horoya AC ya kwao Guinea, msimu wa 2024-2025, ulikuwa ni mzuri kwake, baada ya kumaliza na ‘Clean Sheets’, 19, akiibuka kinara na kumpiku, Djigui Diarra wa Yanga aliyekuwa nazo 17 tu.
Hata hivyo, majeraha ya Camara, katika msimu wake wa pili na kikosi hicho, yaliilazimisha Simba kuingia sokoni dirisha dogo la Januari 2026 na kumsajili, Mahamadou Tanja Kassali, ambaye hadi sasa ameonyesha pia kiwango bora kikosini humo. Kipa huyo ana ‘Clean Sheets’, nne za Ligi Kuu Bara, huku akiokoa michomo ya hatari, ikiwemo pia ya Prince Dube wa Yanga dakika ya 46, katika mechi ya ‘Kariakoo Derby’, iliyopigwa New Amaan Complex, Zanzibar, Machi 1, 2026 na kuisha suluhu.
Michomo mingine ya hatari aliyookoa ni ya suluhu (0-0), pia ya kikosi hicho dhidi ya Dodoma Jiji, baada ya mshambuliaji nyota wa ‘Walima Zabibu’, Elias Maguri, kupiga shuti kali dakika ya 90+5, Kwenye Uwanja wa Jamhuri, Februari 25, 2026. Licha ya Simba kushinda mabao 2-0, dhidi ya Mashujaa, Kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni, Januari 29, 2026, ila Kassali, aliokoa mchomo wa hatari uliopigwa na Hassan Hadji ‘Cheda’, dakika ya 64, akipokea pasi ya Salum Kihimbwa.