Dar es Salaam. Katika pilikapilika za maisha ya kila siku, kuna kazi nyingi ambazo wanawake huzifanya bila hata kuzitilia maanani kama ni fursa za kiuchumi.
Kazi hizo ni za kawaida za kila siku kama za kufua, kufuta vumbi, kufagia na hata kusafisha samani, zote hizi huonekana kama kazi za kawaida kabisa na za wajibu wa nyumbani.
Lakini ukiangalia kwa jicho la kibiashara, kazi hizi zinaweza kuwa chanzo cha kipato, hata kuzidi ajira rasmi na kumfanya mtu aendeshe maisha yake.
Ukweli ni kwamba, watu wanaohitaji msaada wa kazi hizi ni wengi kuliko inavyodhaniwa. Kasi ya maisha ya sasa imewafanya wengi kukosa muda wa kushughulikia usafi wa nyumba zao ipasavyo. Hapo ndipo soko linapojitokeza, la uhakika na linalokua kila siku.
Kazi hizi sasa ndizo zimemnyanyua Eveline Ulanga, mwanamke aliyebadili changamoto ya maisha yake kuwa fursa ya biashara yenye mafanikio.
Akiwa mwajiriwa katika moja ya kampuni za simu, Eveline alijikuta akibanwa na majukumu ya kazi, kiasi kwamba hakuwa na muda wa kufanya usafi wa nyumbani, ikiwemo kufua na kupanga mazingira ya nyumba yake.
Ili kukabiliana na hali hiyo, alilazimika kuajiri watu wa kumsaidia kila alipokuwa nyumbani. Hata hivyo, hali hiyo haikumletea tu unafuu, bali ilimfungua macho. Aligundua kuwa yeye si wa pekee, kuna watu wengi wenye uhitaji kama wake, lakini hawana muda wala mifumo ya kuwapata watu wa uhakika wa kufanya kazi hizo.
Kutokana na uelewa huo, mwaka 2021 Eveline alianza rasmi safari yake ya ujasiriamali, ingawa bado alikuwa ameajiriwa.
Mwanzo hakuwa na mbwembwe; hakuwa na ofisi wala mashine za kisasa. Alianza na vijana wawili waliokuwa wakifanya kazi za usafi majumbani kwa kutumia vifaa vya kawaida kama mifagio na mopa za kudekia.
Kupitia mitandao ya kijamii, alianza kujitangaza kwa marafiki na watu aliowafahamu kuwa anatoa huduma ya kazi hizo. Mwitikio ulikuwa mkubwa kuliko matarajio yake. Wateja waliongezeka kwa kasi na wengi walidhani tayari ana kampuni kubwa yenye mifumo kamili.
“Watu walipoona kazi yetu walifikiri tuna kampuni kubwa. Hapo ndipo nilipoona kuwa hii ni fursa ya kuikuza biashara hii kitaalamu zaidi,” anasimulia Eveline.
Akiwa na maono hayo, aliamua kumshirikisha mwenzake na kuingia naye ubia. Ndani ya miezi mitatu hadi minne ya kwanza, anasema waliendelea kufanya kazi bila kuwa na ofisi rasmi. Lakini kadri mahitaji yalivyoongezeka, walilazimika kuchukua hatua kubwa zaidi.
Hatimaye walifungua ofisi eneo la Makumbusho, Kinondoni jijini Dar es Salaam, wakiwa na mtaji wa Sh3 milioni. Fedha hizo zilitumika kununua baadhi ya mashine, kulipia fremu na gharama nyingine za uendeshaji. Ingawa mtaji haukutosha kikamilifu, waliendelea kukua taratibu.
Katika hatua ya mwanzo, anasema waliamua kujikita kwenye huduma ya kufua na kukausha nguo (dry cleaning), wakilenga kujenga ubora na kuaminika. Baada ya mwaka mmoja, walipanua huduma zao na kuanza kusafisha makochi na nyumba, baada ya kupata vifaa vya kisasa.
Leo, kampuni yao inatoa huduma mbalimbali ikiwamo ya usafi wa nyumba, makochi, mazulia, pamoja na kufua na kukausha nguo za aina zote.
Mbali na nyumba za kawaida, kampuni hiyo pia husafisha mazulia ya misikiti, makanisa na kumbi mbalimbali.
Eveline anasema wanao uwezo wa kusafisha kila sehemu ya nyumba, kuanzia madirisha, milango, feni, masinki, sakafu hadi kuta.
“Huduma hii inawasaidia sana hasa kwa watu waliomaliza ujenzi wa nyumba zao na wanaotarajia kuhamia kwenye nyumba mpya. Unajua kufanya usafi nako ni kipaji bwana,” anasema Eveline.
Hata hivyo, anasema hakuna mafanikio yanyopatikana kirahisi, anasema mwanzoni walikumbana na changamoto nyingi, ikiwemo ukosefu wa uzoefu katika biashara hiyo.
“Kabla ya kuwa na ofisi wateja wengi walikuwa wanaulizia tunapatikana wapi, wasipojibiwa kwa wakati, wanatuona kama wapiga porojo tu na hata tuliowahi kuwafanyia kazi zao wakawa wanapunguza imani wanatuhama,” anasema.
Anasema tatizo lingine ilikuwa ni changamoto ya usimamizi, hasa kutokana na Eveline kuendelea na ajira yake wakati huo.
“Kuwatumia vijana kwenda kwa wateja kulihitaji uangalizi mkubwa na wakati mwingine walishindwa kufika maeneo tuliyoitwa kufanya kazi kwa sababu ya kutoyafahamu vizuri,” anasema.
Hata hivyo, anasema baada ya kufungua ofisi, changamoto nyingine ilijitokeza katika ununuzi wa vifaa.
Eveline anasema kutokana na mtaji mdogo, walinunua mashine zilizotumika, baadhi zikiwa na hitilafu. Hali hiyo ilisababisha hasara na kuchelewesha maendeleo yao.
Anasema pia walikumbana na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara, hali iliyowalazimu kufuatilia huduma hiyo kwa karibu ili kuhakikisha kazi haziathiriki.
Changamoto nyingine ilikuwa ya kuchanganya nguo za wateja na nyingine kuziharibu.
“Kadri tulivyoendelea kujifunza na kupata uzoefu, tuliboresha huduma zetu,” anasema.
Leo, Eveline si tu msimamizi bali ni mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo na ameachana na ajira ili kujikita kikamilifu katika biashara, uamuzi uliomwezesha kusimamia kwa karibu ubora wa huduma.
Huduma wanazotoa zimekuwa msaada mkubwa kwa watu wengi, hasa wale wenye shughuli nyingi za kila siku. Wateja wanakiri kuwa uwepo wa kampuni kama hizi unarahisisha maisha na kusaidia nyumba kubaki katika hali ya usafi muda wote.
Angela Matiku, mkazi wa Tabata, anasema baadhi ya kazi za usafi zinahitaji utaalamu na muda ambao si rahisi kwa mtu mmoja kumudu.
“Kuna vitu kama sofa zenye rangi nyepesi, zikichafuka zinahitaji usafi wa hali ya juu. Huwezi kufanya mwenyewe kwa ufanisi ule ule, lakini hawa wanasaidia sana,” anasema.
Kwa upande wake, Said Mashaka anaeleza kuwa huduma hizi ni muhimu hasa kwa nyumba mpya.
“Ukimaliza kujenga, usafi unaohitajika kabla ya kuhamia si rahisi. Unahitaji watu wenye ujuzi na vifaa maalum ili kuondoa vumbi lote na kufanya nyumba iwe tayari kuishi,” anasema.
Hata hivyo, anasisitiza umuhimu wa ubora na uaminifu katika biashara hiyo. Anaonya kuwa wateja wanathamini huduma bora na kampuni zinazoshindwa kudumisha viwango hivyo hupoteza soko kwa haraka.
Anashauri watoa huduma kuhakikisha kila kazi wanayoifanya inakuwa fursa ya kujenga uhusiano wa kudumu na mteja.
