Huu hapa mfupa wa Pedro Yanga

YANGA ina mechi ya nne mfululizo ugenini leo ikiwa mgeni wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini, Dodoma, ikiuanza mzunguko wa pili, lakini kuna tahadhari itatakiwa kuichukua kama inautaka ubingwa ikikaribia kuvunja rekodi yake ya msimu uliopita.

Yanga leo itakuwa inaanza mzunguko wa pili ambapo takwimu zinaonyesha timu hiyo imeshaangusha pointi nane ndani ya mechi 15 za mzunguko wa kwanza ambazo msimu uliopita iliziangusha kwenye msimu mzima.

Msimu uliopita Yanga ilikuwa bingwa lakini ndani ya mechi zake 30 iliangusha pointi nane tu ikipoteza michezo miwili na kutoa sare moja, kwenye msimu ambao timu hiyo ilifundishwa na makocha watatu tofauti.

Hadi Yanga inamaliza mzunguko wa kwanza ilikuwa imeshafundishwa na makocha wawili tofauti akianza Miguel Gamondi ambaye aliiacha Yanga imeshaangusha pointi sita baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo.

Yanga ilipoteza mechi ya kwanza dhidi ya Azam ikikubali kipigo cha bao 1-0 Novemba 2,2024 huku beki wa timu hiyo, Ibrahim Abdulla ‘Bacca’ akitolewa kwa kadi nyekundu, kisha ikapoteza tena mechi inayofuata dhidi ya Tabora United ambayo sasa ni TRA United kwa mabao 3-1, yote ikiwa nyumbani.

Mechi hizo mbili zikamfukuzisha Gamondi kisha kuletwa Sead Ramovic ambaye hadi anaondoka hakupoteza mchezo wowote akiongoza Yanga kwenye mechi sita na kushinda zote, kisha akitimkia CR Belouizdad ya Algeria.

Akafuata Hamdi Miloud ambaye aliiongoza Yanga kwenye mechi 14 lakini mechi yake ya kwanza tu akashtuliwa kwa kulazimishwa suluhu ya 0-0 ugenini dhidi ya wanajeshi wa JKT Tanzania huku zingine 13 akishinda na kuipa Yanga ubingwa.

Msimu huu Yanga iliuanza ikiwa chini Romain Folz ambaye hadi anaondoka hakuwahi kupoteza mechi yoyote kwenye ligi lakini aliangusha pointi mbili kwenye sare ya ugenini dhidi ya Mbeya City kwenye mechi ya pili tangu kaanza msimu.

Baada ya Folz kutimuliwa akiiongoza Yanga kwenye mechi mbili tu za kwanza, Pedro Goncalves akachukua timu akianza na Mtibwa Sugar nyumbani ambao atakutana nao leo na kuendeleza  rekodi hiyo ya kutopoteza lakini ikaangusha pointi hizo nane.

Yanga chini ya Pedro imeangusha pointi nane kwenye matokeo ya aina moja ikipata sare za 0-0 kwenye mechi tatu tofauti akianza na Simba  nyumbani Machi Mosi,2026, kisha Azam na TRA United  zote mbili ikiwa ugenini.

Licha ya kuangusha pointi hizo nane kwenye mechi 15 za kwanza Yanga bado ipo juu ya msimamo ikiongoza kwa kukusanya pointi 37, ikiwa haijapoteza lakini pia ikiwa imefunga mabao mengi 31, ikiruhusu mawili pekee.

Mtihani alionao, Pedro ni kuhakikisha Yanga haiendelei kuangusha pointi lakini pia akitakiwa kuipa makali safu yake ya ushambuliaji ambayo kwenye mechi tatu ilizoangusha pointi msimu huu, watangulizi wake walitoka salama kwa kufunga mabao na kushinda kasoro mechi moja tu dhidi ya Azam ambao timu hiyo ilishinda moja na nyingine ikipoteza.

Changamoto kubwa ambayo inamkumba Pedro ni kuumia kwa washambuliaji wake bora watatu kwenye kikosi ambao wote ni chaguo la kwanza ambao ni Clement Mzize atakayekosekana msimu huu mzima, Laurindo Aurelio ‘Depu’ akiumia nyama za paja na kuwa nje kwa wiki tatu.

 Mbali na Mzize na Depu, Pedro akapokea taarifa mbaya zingine baada ya Prince Dube naye akikosa mechi ya leo kufuatia kurudishwa jijini, Dar es Salaam kufuatia kuumia nyama za paja kwenye  mechi dhidi ya TRA United na sasa amebakia na mshambuliaji mmoja pekee, Emmanuel Mwanengo ambaye tangu atue kupitia usajili wa dirisha dogo la Januari 2026, akitokea TRA United hajafunga bao lolote kwenye Ligi Kuu Bara.

Akizungumzia hilo, Pedro alikiri kukutana na changamoto kwenye safu yake ya ushambuliaji ilitokana na baadhi ya washambuliaji kuandamwa na majeruhi huku akisema kwa sasa wako kwenye hesabu za kutafuta mpango B kuisuka upya safu hiyo.

“Ni kweli tumejikuta tunaangusha hizo pointi kuna mambo mengi yamechangia lakini kubwa ni kutokana na majeraha, unapokutana na mazingira ambayo washambuliaji wako watatu wanaumia kwa nyakati tofauti lazima mtapata shida kidogo.

“Hatujakata tamaa, unaona kama Dube aliumia kwenye mechi iliyopita tena ikiwa inaendelea, tukabaki na Mwanengo pekee, kwa sasa tunaendelea kumuimarisha ili asaidie timu, ni mchezaji mzuri lakini mbali na hilo tunataka kuwa na mpamgo B wa namna gani tunaweza kuwa timu inayoweza kutengeneza ushindi.”