Huu hapa utaratibu wa kupata mikopo ya Sh200 bilioni kwa vijana

Dar es Salaam. Wizara ya  Maendeleo ya Vijana, imeanika wazi mwongozo kwa vijana namna ya kuomba na kunufaika na mikopo ya Sh200 bilioni ambayo imekuwa ikitangazwa na Serikali kuwa lengo lake ni kuwawezesha kiuchumi.

Katika mwongozo huo uliotolewa leo Jumamosi Machi 21, 2026, serikali imeeleza kuwa waombaji ni mtu mmoja au kikundi na wanatakiwa kuwa na andiko la mradi au biashara, akaunti ya benki au namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mwombaji au kikundi hicho, pamoja na kuwasilisha barua rasmi ya maombi ikieleza aina ya mradi, kiasi cha mkopo na eneo la utekelezaji.

Aidha, nyaraka muhimu zimetajwa kuwa ni pamoja na kitambulisho cha Taifa (NIDA) au cha mpiga kura, TIN, leseni ya biashara kwa wanaoendesha shughuli tayari, barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa na picha mbili za mwombaji, huku maombi yote yakitakiwa kuwasilishwa kabla ya Aprili 3, 2026 kupitia barua pepe maalum ya [email protected]

Hatua hiyo imejibu malalamiko na mapendekezo ya vijana ambao kwa nyakati tofauti tangu kutolewa kwa taarifa ya fedha hizo wamekuwa wakijitokeza wakisema hakuna uwazi wa utaratibu wa upatikanaji wake na kushauri kuwepo kwa mfumo unaoeleweka na unaowafikia wote.

Vikundi mbalimbali vya vijana vikiwemo vya vyama vya siasa, wanaharakati na makundi ya kibiashara vimekuwa vikieleza sintofahamu yao kuhusu mgawanyo wa fedha hizo, vigezo vya utoaji na taasisi husika za usimamizi, huku baadhi yao wadai kuwa taarifa zinazotolewa hazijakamilika.

Licha ya lengo la fedha hizo kuwa ni kupunguza changamoto za ajira, mitaji na kukuza uchumi wa vijana, mjadala umeendelea kutawala juu ya namna bora ya kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa kwa haki na kwa ufanisi, jambo lililopelekea shinikizo la kutaka mwongozo rasmi wa kitaifa.

Miongoni mwa malalamiko makubwa yanayotolewa na vijana ni ukosefu wa uwazi wa namna ya kupata fedha hizo, huku wakidai kuwa taarifa zilizotolewa awali hazikujitosheleza.

“Mfumo wa utoaji hauko wazi, vijana wengi hawajui wapi pa kuanzia wala vigezo vinavyotumika,” alieleza Mwenyekiti wa ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo mbele ya wanahabari jijini Dar es Salaam.

Aidha, alihoji kukosekana kwa chombo chenye dhamana ya moja kwa moja ya kusimamia fedha hizo, wakisema hali hiyo inaweza kufungua mianya ya upendeleo na matumizi mabaya.

“Kukosekana kwa usimamizi wa wazi kunaweza kufungua mianya ya upendeleo na matumizi yasiyo sahihi,” walisisitiza.

Kwa upande mwingine, Kitengo cha Vijana wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Kivicha), walikosoa mgawanyo wa fedha hizo katika wizara mbalimbali wakisema hatua hiyo inaondoa uwajibikaji wa moja kwa moja na kuongeza urasimu.

“Kama fedha zilikuwa mahsusi kwa ajili ya vijana, kwa nini zisibaki chini ya Wizara ya Vijana?” alihoji mradi wa Taifa wa Kivicha, Masoud Mambo akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari hivi karibuni.

Nao Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Wananchi (Juvicuf), wamekuwa wakilalamika kuwa hadi sasa hakuna taarifa rasmi inayoonesha kiasi kilichopelekwa katika kila wizara, wakidai hali hiyo inafanya iwe vigumu kufuatilia matumizi ya fedha hizo.

“Ukosefu huu wa uwazi unatengeneza mazingira magumu ya kufanya tathmini na ufuatiliaji,” ilisema sehemu ya taarifa yao.

Mbali na malalamiko, vijana pia wamekuwa wakitoa mapendekezo mbalimbali wakitaka maboresho ya haraka ili fedha hizo ziwe na tija. Wamependekeza kuandaliwa kwa mwongozo mmoja wa kitaifa utakaoeleza kwa kina utaratibu mzima wa utoaji wa fedha hizo, vigezo, masharti ya urejeshaji na wizara zote zilizopokea fedha.

Hata hivyo, Serikali kupitia mwongozo wake imeweka wazi utaratibu wa maombi na vigezo vinavyotakiwa, ikisisitiza kuwa mchakato huo utakuwa wazi na unaoeleweka kwa vijana wote.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, “mwombaji atatakiwa kuwasilisha barua ya maombi ikibainisha jina, aina ya mradi, kiasi cha mkopo na eneo la utekelezaji pamoja na kuambatanisha nyaraka zote muhimu.”

Serikali pia imeeleza kuwa mfumo huo una lengo la kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa halisi na kuleta matokeo chanya katika uchumi wa vijana.

Hatua hiyo inaashiria mwanzo wa utekelezaji wa mpango huo ambao kwa muda umekuwa ukizua mjadala mpana, huku macho ya wengi yakielekezwa kuona kama mwongozo huo utatafsiriwa katika vitendo na kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa walengwa.