Mkataba wa Nashoni, Simba upo hivi!

SIMBA imefanya umafia baada ya kumsajili kiungo wa Singida Black Stars, Kevin Nashon kwa mkataba wa miaka miwili zikiwa ni siku chache tangu walipogomewa saini yake.

Simba kabla ya kufanya maamuzi ya kumsainisha mkataba wa awali wa miaka miwili Nashon, ilishafanya utafiti wa kujua amebakiza muda gani Singida Black Stars.

Nashon alijiunga na Pamba 04/08/2025  kwa mkataba wa mwaka mmoja wa mkopo, mwishoni mwa msimu huu atakuwa anamalizana na SBS, jambo lililowashawishi Simba kumhitaji katika kikosi hicho.

Awali Simba ilimtaka kiungo huyo kwenye usajili wa Januari mwaka huu, lakini bei iliyopewa na Singida iliwafanya warudi nyuma na kujipanga upya, hata hivyo katika mahesabu yao waliona kuwa kiungo huyo amebakiza mkataba wa chini ya miezi sita kwenye kikosi hicho na kumuita Dar es Salaam fasta wakampa mkataba wa awali wa miaka miwili na kumrudisha Mwanza kwa mwewe.

Pamoja na kufanya mambo yote kwa siri kubwa, uongozi wa Pamba ulipata mkanda mzima na kukubaliana mchezo wa juzi kati ya Pamba na Simba kiungo huyo akae nje kabisa lakini atarudi kwenye michezo mingine.

“Ingawa mchezaji mwenyewe hajawa wazi, lakini tumefuatilia na kugundua alikwenda Dar es Salaam na kumalizana na Simba na kurudi kwa ndege haraka, sisi tunafahamu kwa kuwa tulipata taarifa, awali kulikuwa na dili hili lakini walishindwana na Singida kwenye bei, lakini hakuna kizuizi kwa kuwa amebakiza mkataba nafikiri wa miezi mitatu tu,” kilisema chanzo kutoka Pamba.

Simba wamekimbia haraka kukamilisha usajili huo kwa kuwa kuna taarifa kuwa kiungo wao wa shoka  Alassane Kante ataachana na na klabu hiyo mwishoni mwa msimu na kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Libya.

Kigogo mmoja wa Simba alisema kiwango cha Nashon aliyezaliwa 02/08/2000 (umri wa miaka 25) kimewavutia na wanaona kuna kitu atakiongeza katika klabu hiyo kama kila kitu kitakwenda sawa:

”Simba itafanya mabadiliko kwa baadhi ya wachezaji, kuna watakaoingia na kutoka katika usajili wa dirisha kubwa.

Alipotafutwa mkurugenzi wa utawala wa SBS, Muhibu Kanu alisema:

”Kwa sasa tunaweka nguvu zetu katika mechi tunazocheza baki tu baki, baada ya hapo ndipo tutarudi katika masuala ya usajili, hata hivyo hatujapokea barua yoyote kuhusiana na mchezaji huyo, kwa kifupi sina la kukujibu kuhusiana na hilo.”

Nashon ambaye yupo kwenye kikosi cha Taifa Stars amekuwa akitajwa mara kwa mara kwenye tetesi za usajili zikizihusu klabu ya Simba na Yanga lakini hakuna hata moja ambayo awali ilifikia hatua ya kumpa mkataba wa awali.