Mume alivyomuua mke wake, kumchuna na kutenganisha viungo vyake

Moshi. Hivi unaweza kuamini mume wa ndoa aliyependana na mkewe anaweza kufanya ukatili huu? Hii imetokea Kyerwa mkoani Kagera ambapo mume amemuua mkewe, kumkatakata na kutupa mguu wake kwenye choo cha shimo, mkono akauficha chini ya godoro, kisa wivu wa mapenzi.

Mwanamume huyo, Edson Wilson maarufu kwa jina la Rukuname, mkazi wa Kijiji cha Rugasha, hakuishia hapo, aliuchuna mwili huo ngozi na kuuzika nyuma ya nyumba.

Tukio hilo lilitokea Machi 30, 2024 katika Kitongoji cha Chankuba katika Kijiji cha Rugasha Wilaya ya Kyerwa, ambapo Wilson alimuua mkewe, Selina Nestory baada ya kumkuta na mwanamme mwingine.

Simulizi ya mauaji haya imo katika hukumu iliyotolewa Machi 18, 2026 na Jaji Lilian Itemba wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Bukoba na kuwekwa katika tovuti ya mahakama Machi 20, 2026, ambapo mshtakiwa amehukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Jaji anasema maelezo ya ungamo ya mshitakiwa na kupatikana kwa mwili wa marehemu kunafanya hitimisho kuwa ni mshitakiwa ambaye alimuua mkewe kutokana na wivu wa mapenzi na ushirikina.

Kulingana na ushahidi, usiku wa Machi 29, 2024, Selina Nestory (marehemu) alienda katika baa ya jirani na akachelewa kurudi nyumbani, ambapo mumewe, Rukumane aliamua kumfuta huko huko alipoenda, lakini akakuta baada imefungwa.

Alipokuwa anarudi, jirani na baa hiyo, alimsikia mkewe akizungumza na mtu mwingine kwenye simu wakiweka miadi ya kukutana eneo hilo alilokuwepo.

Mshitakiwa katika maelezo yake ya ungamo anaeleza kuwa “Nilikwenda hadi baa na nilipofika nilikuta baa ikiwa imefungwa, nikiwa nataka kurudi nikasikia sauti ya simu kwenye miti na baada ya kusogea nilisikia sauti ya mke wangu.

“Alikuwa akiongea na mtu kwenye simu akimwambia yupo palepale alipomwacha, hivyo basi afanye haraka. Punde si punde alitokea mwanamme, akamkamata mkono mke wangu nao wakaanza kuondoka,” alieleza.

Hicho inatajwa sababu ya mshitakiwa kumuua mkewe.

Ushahidi ulivyokuwa kortini

Katika kuthibitisha shitaka la mauaji ya kukusudia, upande wa mashitaka uliita mashahidi 11 na kuwasilisha vielelezo 11 huku mshitakiwa akiwa ni shahidi pekee wa upande wa utetezi na katika ushahidi wake hakuwasilisha kielelezo chochote.

Ilidaiwa awali marehemu alikuwa akiishi Wilaya ya Ngara ambapo alikuwa ameolewa na Donatus Wilson, ambaye ni kaka wa mshitakiwa. Baadaye wawili hao walitengana akahamia Kyerwa akaolewa na mshitakiwa kama mke wa pili.

Mmoja wa watoto wa marehemu, Amani Donatus aliyekuwa shahidi namba tano, alimfuata mama yake na kuishi kwa muda pamoja na mshitakiwa na baadaye alihamia kwake, jirani na kwa mama yake na alikuwa akimtembelea kila siku.

Ghafla, anasema mama yake akawa ametoweka na Aprili 2, 2024 alimkabili mshitakiwa na kumuuliza alipo mama yake, lakini hakuwa na majibu yanayoeleweka, kwani alidai amekimbilia Uganda kwa mtu anayeitwa Bouncer.

Shahidi wa pili, Stella Donatus naye ni mtoto wa marehemu aliyekuwa akiishi Ngara, alipopata taarifa za kutoweka kwa mama yake, alimpigia simu mshitakiwa ambaye alimpa hadithi kama aliyokuwa amempa shahidi wa tano wa Jamhuri.

Kulingana na shahidi huyo, simu ya mama yake alikuwa ameisajili yeye kwa jina lake, hivyo alijaribu kuipiga akashangaa inapokewa na mshitakiwa, hiyo ikamtia mashaka kwamba kama ameenda Uganda, ilikuwaje aache simu yake.

Kutokana na wasiwasi, alisafiri hadi Kyerwa ambapo yeye na ndugu yake walifungua taarifa polisi ambako waliwashauri wamtafute mama yao Uganda, walienda na kukutana na Bouncer, ambaye alikanusha kusafiri na mama yao.

Vipande vya mwili vinapatikana

Aprili 16,2024, Polisi na viongozi wa kitongoji wakaamua kufanya upekuzi katika nyumba aliyokuwa akiishi mshitakiwa ambaye wakati huo alikuwa mikononi mwa polisi, ambapo kundi moja liliingia katika chumba walichokuwa wakilala wawili hao.

Zoezi hilo lililoanza saa 8:00 mchana lilimshirikisha pia mshitakiwa, ambapo ndani ya chumba hicho walipata mfupa uliodhaniwa ni wa binadamu, ambao ulikuwa umefichwa chini ya foronya ya godoro na ulionekana kama uliunguzwa nusu.

Wakiwa katika mshituko, kundi hilo lilikwenda nyuma ya nyumba kwa ajili ya ukaguzi zaidi na nje ya nyumba hiyo kulikuwa na choo cha shimo, ambapo shahidi wa pili aliingia na kuona mkeka, ndipo aliamua kumulika tochi shimoni.

Ndani ya shimo hilo la choo, aliona baadhi nguo na walizitoa na zilitambuliwa na shahidi wa tano kuwa ni nguo za mama yake na hapo walianza kuhisi mchezo mchafu, wakaamua kubomoa choo kilifunikwa na saruji.

Baada ya kukibomoa walikutana na mguu wa kushoto wa binadamu, mkeka, sketi na nguo nyingine za jinsia ya kike ambazo zilitolewa mbele ya mshitakiwa na vitu vyote viliorodheshwa na kwa kuwa giza lilikuwa limeingia, polisi walirudi kituoni.

Waliondoka na vielelezo huku wakiacha ulinzi katika eneo hilo na waliporudi kituo cha polisi, mshitakiwa alikiri mbele ya shahidi wa 11 kuwa alimuua mkewe na kuuzika mwili wake nyuma ya nyumba waliyokuwa wakiishi na mkewe.

Mbali na mwili wa marehemu, pia alieleza kuwa alizika mabeseni mawili ambayo aliyatumia wakati wa mauaji hayo ya mkewe.

Siku iliyofuata, Aprili 17, 2024, utafutaji uliendelea kwa kundi lile lile la kwanza wakishirikiana na polisi wa Kyerwa na daktari ambapo katika chumba kilekile walichokuwa wakiishi, kulipatikana mfupa mwingine wa binadamu.

Hapo ndipo mshitakiwa aliwaongoza watafutaji hadi nyuma ya nyumba na kuwaonyesha alipofukia mabeseni mawili na mwili wa marehemu ulioopolewa kutoka choo cha zamani na uchunguzi ulithibitisha koromeo lilikuwa limekatwa.

Baadaye mifupa hiyo ilichukuliwa sampuli na baada ya kufanyiwa uchunguzi wa vinasaba (DNA) na shahidi wa sita, Anna Chuwa kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali aliileza mahakama kwamba mabaki hayo, ni ya marehemu Selina.

Katika utetezi wake kortini, mshitakiwa alikanusha mashitaka hayo lakini akakiri kumfahamu marehemu kama alikuwa mke wa pili na alikuwa anampenda sana na hangeweza kumuua na endapo angekuwa amemuua, asingebakia eneo la tukio.

Badala yake, angeweza kutorokea nje ya nchi na kuwa alitengenezewa kesi hiyo kwa kuwa alikuwa na chuki na watu watan, akiwamo kaka yake aitwaye Donatus William, kwa kuwa alipomuacha marehemu, yeye akamuoa.

Alijitetea kuwa choo kile ambacho mwili ulikutwa, kimekuwa kikitumiwa na watu wengi na kwamba aliteswa na polisi ili kukiri kutenda mauaji hayo.

Katika hukumu yake, Jaji Itemba alisema hakuna ubishi kuwa kesi hiyo imejengwa katika ushahidi wa mazingira na maelezo ya ungamo ya mshitakiwa mwenyewe.

Jaji alisema kwa kuegemea maelezo hayo ya ungamo, mshitakiwa anaeleza kwamba alimuua mkewe baada ya kumnyonga kwa waya, kisha kumkata mguu na mkono na kwenda kutupa mguu katika shimo la choo.

Aliuhifadhi mfupa wa mkono kwa mipango ya imani za kishirikina na kwamba inavyoonekana, kiini cha mauaji hayo ni imani za kishirikina, kwamba angetumia mifupa ya marehemu kusafisha nyota ndio maana aliihifadhi kwa kuichoma.

Pia Jaji akasema mashahidi namba 1, 2, 5, 9 na 11 wa Jamhuri wanathibitisha kuwa baada ya mshitakiwa kukiri kumuua mkewe, alibeba jukumu la kwenda kuwaonyesha wapelelezi mahali alipozika mwili na mabaki ya marehemu.

“Katika mazingira hayo niliyoyaeleza, ni mshitakiwa pekee aliyekuwa anajua mahali ulipo mwili wa mkewe na ukapatikana umezikwa pamoja na mabeseni mawili na mguu ambao uliutupwa ndani ya shimo la choo,”alisema Jaji.

“Ninaona kuwa hatua ya mshitakiwa kukiri kutenda kosa la mauaji mbele ya shahidi namba 11 wa Jamhuri, lilikuwa ni ungamo la kweli chini ya kifungu 31 cha sheria ya ushahdi sura ya 6 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023,” alieleza Jaji.

Kuhusu utetezi wa mshitakiwa kuwa aliteswa na polisi kukiri kutenda kosa, Jaji alisema kama hilo lingekuwa ni kweli, lakini mwisho wa siku ni yeye aliyekiri na kuelezea kwa kina mauaji hayo, taarifa ambayo hakuna mwingine aliyeifahamu.

Jaji alisema ingawa choo hicho kilikuwa kinatumiwa na watu wengine pia, ushahidi madhubuti wa Jamhuri haukuweza kutikiswa, hivyo mahakama inamtia hatiani mshitakiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.