KOCHA wa TMA FC, Mzanzibar Haji Ali Nuhu, amesema hadi sasa hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa kati yake na uongozi wa Yanga, kwa ajili ya kujiunga na kikosi cha timu za vijana, akiungana na Mohamed Badru, aliyewahi kufanya naye kazi.
Kocha, Badru ambaye kwa sasa anasimamia programu ya Yanga Soccer School, iliyozinduliwa rasmi tangu, Novemba 15, 2025, inaelezwa mabosi wa timu hiyo wanamtaka Haji Nuhu, ili akaungane naye, baada ya wote kufanya vizuri wakiwa na Azam FC.
Akizungumza na Mwanaspoti, Haji, alisema hadi sasa hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa juu ya suala hilo, japo, ikiwa itatokea itakuwa ni jambo nzuri kwake, kwa sababu ana ushirikiano mzuri na Kocha, Badru tangu wakifanya kazi Azam FC.
“Nadhani watu wanahusisha suala langu la kwenda Yanga na uhusiano mzuri niliokuwa nao na Kocha, Badru tangu tukiwa wote Azam FC, kwa sasa nipo Zanzibar kwa ajili ya mapumziko, ingawa, kukitokea jambo lolote nitaliweka wazi,” alisema Haji.
Aidha, Haji alisema malengo yake kwa sasa ni kupata changamoto mpya katika Ligi ya Championship anayoifundisha kwa mara ya kwanza maishani mwake, japo, ikitokea pia fursa nyingine atakaa na uongozi wake wa TMA ili wampe baraka za kuondoka.
Kocha huyo aliyezifundisha JKU SC na Mafunzo FC zote za Zanzibar na timu za vijana chini ya miaka 17 na 20 za Azam FC, amejiunga na kikosi hicho chenye maskani yake Arusha, akichukua nafasi ya mtangulizi wake, Habibu Kondo, aliyeondolewa.
Kondo aliyezifundisha timu za Mtibwa Sugar, Azam, Coastal Union, Majimaji na Mbeya Kwanza, aliondolewa katika benchi la ufundi na kocha msaidizi, Augustino Thomas, kocha wa makipa, Ally Mustapha ‘Barthez’ na kocha wa viungo, Kigi Makasi.
Baada ya kuondoka kwa Kondo, akapewa nafasi hiyo aliyekuwa mchezaji wa timu hiyo, Omary Matwiko ‘Tico Tico’, ambaye kwa sasa ameteuliwa kusaidiana na Haji anayewindwa na Yanga, licha ya kusaini mkataba na kikosi hicho hadi mwisho wa msimu.
TMA FC, iko nafasi ya 11 na pointi 21, katika msimamo wa Championship msimu huu wa 2025-2026, ambapo timu hiyo imeshinda mechi tano tu, sare sita na kupoteza 10, kati ya 21, huku, ikifunga mabao 14 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 19.