Rais Samia atahadharisha uhuru wa kuabudu usivuke mipaka

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kulinda uhuru wa kila Mtanzania kuabudu kulingana na imani yake, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu mipaka ya uhuru huo ili kudumisha amani na mshikamano wa taifa.

Ameyasema hayo leo Jumamosi, Machi 21, 2026 wakati akishiriki Baraza la Idd El-Fitr lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia amesema Serikali inatambua na kuheshimu haki ya msingi ya uhuru wa kuabudu, lakini akaonya kuwa uhuru huo unapaswa kutumika kwa kuwajibika.

“Nataka niwahakikishie kuwa serikali yetu itaendelea kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kulinda uhuru wa kila Mtanzania kuabudu kulingana na imani yake. Pamoja na hayo, ni muhimu kwetu sote kuheshimu mipaka ya uhuru huo,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Hatuna budi kuheshimu sheria za nchi na haki za wengine ili uhuru huo usigeuke kuwa chanzo cha chuki, mgawanyiko au kuvuruga amani na mshikamano wa taifa letu.”

Amesema ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha kuwa matumizi ya uhuru huo hayakiuki sheria za nchi wala haki za wengine.

“Hatuna budi kuheshimu sheria za nchi na haki za wengine ili uhuru huo usigeuke kuwa chanzo cha chuki, mgawanyiko au kuvuruga amani na mshikamano wa taifa letu,” amesisitiza Rais Samia.

Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu, viongozi na wageni mbalimbali  kwenye Baraza la Eid El Fitr Kitaifa lililofanyika leo Machi 21, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.

Aidha, Rais Samia ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuenzi umoja, mshikamano na kuvumiliana kidini, akibainisha kuwa misingi hiyo ndiyo nguzo muhimu ya kudumisha amani na utulivu wa nchi.

Amekemea suala la matumizi ya akili mnemba kutumika vibaya kuwatukana viongozi wa serikali na wa dini huku akisema Watoto wakiona mambo hayo nchi haitakuwa salam.

“Nchi haitatulia maendeleo hayatakuwapoi kwa sababu kutakuwa na vurugu, viongozi wa dini endeleeni na jukumu hili muhimu kuwajenga wananchi na kuwaelekeza ili tuwe na taifa lenye amani, utulivu, ustahamilivu ili tuwe na kizazi bora cha sasa na kijacho,” amesema.

Amesema katika nyakati hizi ambazo tunashuhudia migogoro katik amaeneo mbalimbali duniani Tanzania inabaki salama na amani il ani muhimu kutambua kuwa si kila mtu anatamani kuiona katika umoja na utulivu.

Hivyo ni vyema kuhakikisha kuwa mshikamano unazidishwa na upendo kwa nchi na taifa.

Pia, alitumia nafasi hiyo kuitaka Baraza la Kiislamu Tanzania (Bakwata) kujiweka mguu sawa kuhakikisha kuwa uchaguzi wanaotarajia kuufanya mwaka huu uwe wa sawa na haki.

“Hakuna uchaguzi mdogo, hata uchaguzi wa monitor wa darasa una vishindo vyake, hivyo hata uchaguzi huu wa Bakwata utakuwa na vishindo vyake, niwaombe muwe watulivu, wastahamilivu, mchaguane kwa amani, watakaochaguliwa wakiendeleze chombo hiki na wasiochaguliwa waendeleze ushirikiano kuendeleza chombo hiki,” amesema Samia.

Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ali amesema kitendo cha kiongozi wa CCT kusoma aya ya kujenga umoja ni Dhahiri kuwa hakuna kitu kinachoweza kuwafanya watanzania wakafarakana.

“Kujenga umoja wa kidigi, dini mbalimbali na kitaifa ni jambo muhimu ambalo ametukumbusha askofu kutoka CCT katika aya aliyoisoma,” amesema.

Amesema katika mafunzo ya kiislamu kuna mafunzo yanayotaka kuaminiana na wasiokuwa waislamu, kutendeana na kuishi na kila mmoja anajua.

Amesema waislamu hawakatazwi kuhamiliana na wasiokuwa waislamu kama hawana ugomvi nao na anapenda watu waadilifu.

“Hivi karibuni kumeonekana kwenye vyombo vya Habari mbalimbali ambavyo vinaonyesha kuwa kuna watu wanausema vibaya uislamu, wanautukana kama ainanasibishwa na wakristo hivi, siyo kweli, hakuna hata Mkristo mmoja anaweza kuwafanyia fujo Waislamu.”

“Haijawahi kutokea tangu nyuma na mpaka leo haijawahi kutokea namna hiyo, tunaishi vizuri sana, ndiyo maana hata askofu amezungumza vizuri na tumefuahi.

Amesema watu wanaotaka kuweka uchokozi na kutaka Waislamu waamke na kufanya fujo na kudhani kuwa wakristo wamewafanyia fujo.

“Hakuna kila jambo ukaambiwa ukalishika, kila jambo likitokea lazima ulifanyie fikra na kuhakikisha kuwa jambo hilo ni sawa kwa kufanya upelelezi na si kufanya haraka kuzungumza mambo ambayo yanayopistishwa,” amesema.

Amesema katika zama hizi za Akili mnemba ni jambo la kuangalia kwani inatumika vibaya na inaweza kutumika kugombanisha Waislamu na Wakristo.