Mbeya. Serikali imeombwa kuongeza jitihada za kuwawezesha vijana kiuchumi ili kuwaondoa katika makundi yasiyofaa, huku jamii ikihimizwa kuendeleza matendo mema, mshikamano na kusameheana hata baada ya kumalizika kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Wito huo umetolewa leo Jumamosi Machi 21, 2026 na Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Alhaji Sheikh Msafiri Njalambaha wakati akizungumza na waumini kwenye Swala ya Sikukuu ya Idd El-Fitr, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza maadili mema yaliyojengwa kipindi cha mfungo.
Amesema hakuna maana ya kufunga kwa siku 30 na kujitahidi kutenda mema kama kusaidia wasiojiweza, endapo baada ya Ramadhan watu watarejea katika vitendo viovu, akiwataka waumini kuendelea kushikamana na kufanya yaliyo mema.
Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Alhaji Sheikh Msafiri Njalambaha.
“Ramadhan iwe sehemu ya kusameheana, kuombana radhi, kushirikiana na kusaidiana katika mema na siyo kwenye shari. Uislamu unaongoza watu kuishi katika upendo na amani,” amesema Sheikh Njalambaha.
Aidha, amesisitiza kuwa vijana ni nguvu kazi muhimu ya Taifa, hivyo wanapaswa kujengewa misingi ya uzalendo na kupewa fursa za kiuchumi ili waweze kujitegemea na kuepuka kushiriki katika vitendo visivyofaa.
Amesema maendeleo ya Taifa yanategemea kwa kiasi kikubwa mchango wa vijana, hivyo uwezeshaji wao kiuchumi utasaidia kujenga jamii yenye maadili na uzalendo.
“Taifa linawahitaji vijana. Wakiwezeshwa kimaendeleo wataondokana na mambo yasiyofaa na kujijenga kiuzalendo na kimaadili,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Sheikh Njalambaha amewataka Watanzania kutambua, kuthamini na kuheshimu mchango wa wanawake, akieleza kuwa wao ni nguzo muhimu katika maendeleo ya Taifa.
Waumini wa dini ya Kiislamu mkoani Mbeya wakiwa katika swala ya Idd-El-Fitr iliyofanyika katika misikiti mkuu wa Mkoa huo leo Jumamosi, Machi 21, 2026.
Amesema kuwapa wanawake nafasi na kuwashirikisha katika uamuzi kutasaidia kuondoa dhana potofu zinazowadunisha na kuimarisha maendeleo jumuishi.
“Wanawake ni nguzo kuu na wana uwezo mkubwa. Tuwape nafasi, tuwaheshimu, tuwathamini na kuwashirikisha katika maamuzi,” amesema.
Hata hivyo, amekemea vitendo vya kihalifu vinavyodaiwa kuongezeka katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Mbeya, akitoa wito kwa waamini wa Dini ya Kiislamu na Watanzania kwa ujumla, kutumia mafunzo ya Ramadhan kama msingi wa mabadiliko ya tabia na kuwa waongofu.
Akizungumza na Mwananchi, muumini Asfath Rashid amesema Mwezi wa Ramadhan ulikuwa na neema nyingi, akiwahimiza waumini kuendelea na moyo wa kusaidiana na kutenda mema hata baada ya mfungo.
“Tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuanza na kumaliza salama mwezi mtukufu. Tumeshuhudia wengi wakitenda mema, hivyo tuendelee na moyo huo ili funga zetu zipokelewe na tusamehewe madhambi,” amesema.
