Morogoro. Wakati Waislamu nchini na duniani wakisherehekea Sikukuu ya Eid el-Fitri kwa swala zilizofanyika jana na kuendelea leo, jumla ya watoto 12 wamezaliwa katika mkesha wa sikukuu hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Watoto hao wameongeza furaha ya Eid kwa familia zao, huku sita wakizaliwa kwa njia ya upasuaji baada ya mama zao kushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida kutokana na sababu mbalimbali zilizopelekea kujifungu kwa upasuaji.
Akizungumza na Mwananchi leo Machi 21, 2026 mjini hapa, Ofisa Muuguzi Msaidizi wa hospitali hiyo, Sarafina Mhiliwa amesema watoto wote pamoja na mama zao wanaendelea vizuri kiafya.
Sarafina amesema kati ya watoto hao, tisa walizaliwa usiku wa kuamkia jana, ambapo sita walizaliwa kwa upasuaji na watatu kwa njia ya kawaida.
“Katika watoto hao wa awali, sita ni wa kike na watatu wa kiume na katika mkesha wa kuamkia leo, watoto watatu wote wa kiume wamezaliwa kwa njia ya kawaida. Tunamshukuru Mungu watoto na mama zao wanaendelea vizuri,” amesema Sarafina.
Ameongeza kuwa baada ya uchunguzi wa madaktari, mama hao wataruhusiwa kurejea nyumbani kuendelea na malezi ya watoto wao.
Sarafina pia amesema hospitali hiyo inaendelea kutoa elimu kwa kina mama wanaojifungua kuhusu malezi bora ya watoto wachanga, ikiwemo kutambua dalili za hatari na umuhimu wa kuwahi hospitali pindi changamoto za kiafya zinapojitokeza.
Mkazi wa Kihonda, Flora Emilio (35) ni miongoni mwa waliopata watoto katika mkesha huo, akijifungua mtoto wa kike salama.
Flora amesema tukio hilo ni kumbukumbu ya kipekee kwake na familia yake, kwani limeambatana na Sikukuu ya Eid el-Fitri.
“Ninamshukuru Mungu kwa kujifungua salama. Hii ni zawadi kubwa ya Eid kwangu. Naomba Mungu amlinde mtoto wangu akue salama na mwenye afya njema,” amesema Flora.
