Global Publishers
March 22, 2026
0 Comments
Mabingwa mara 12 wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly SC, wameaga rasmi michuano ya CAF Champions League baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Espérance de Tunis katika mchezo wa robo fainali, na hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, Al Ahly walianza vyema kwa kupata bao la mapema dakika ya 10 kupitia kwa mshambuliaji wao Mahmoud Hassan Trezeguet, bao lililowapa matumaini ya kurejea kwenye mchezo huo muhimu.

Hata hivyo, Esperance walionyesha uimara na kurejea kwa nguvu, wakisawazisha dakika ya 68 kupitia kwa Danho kabla ya kuongeza bao la pili dakika ya 78 kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Mohamed Amine Tougai.
Licha ya Al Ahly kusawazisha tena dakika ya 84 kufuatia bao la kujifunga la Jelassi, juhudi zao hazikutosha kwani Esperance walipata bao la ushindi katika dakika za nyongeza (90+4) kupitia tena kwa Jelassi, akirekebisha makosa yake ya awali.
Matokeo hayo yanaihakikishia Esperance tiketi ya kutinga hatua ya nusu fainali, huku Al Ahly wakilazimika kuaga mashindano hayo kwa maumivu makubwa licha ya historia yao kubwa barani Afrika.
