Daraja linalounganisha Bamba na Dege Kigamboni lakatika

Dar es Salaam. Wananchi wa Kigamboni wameeleza adha wanayopitia kutokana na kukatika kwa daraja linalounganisha eneo la Bamba na Dege, Kigamboni jijini Dar es Salaam kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Leo Jumapili, Machi 22, 2026, Mwananchi imefika eneo hilo na kushuhudia utepe wa njano ukiwa umezungushwa kuanzia mita kama 50 kutoka daraja lililokatika, ili kuzuia vyombo vya usafiri kupita.

Hata hivyo, watembea kwa miguu waliwekewa daraja la mbao lililokatika juu ya daraja kubwa linalojengwa ambalo bado halijaisha, ambalo pia si salama hasa kwa wazee, wagonjwa na watoto.

Wakati wa kuvuka, mmoja wa wananchi aiteleza na kudondoka kabla ya kupewa msaada na wananchi wenzake pamoja na polisi wachache waliokuwa eneo hilo.

Daraja linalounganisha eneo la Bamba na Dege, Kigamboni jijini Dar es Salaam limekatika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Wakizungumzia adha wanayopitia, baadhi ya wananchi wamesema, ukiachana na hofu ya usalama wao katika kuvuka daraja la muda lililojengwa kwa mbao, pia gharama za usafiri zimeongezeka.

“Badala ya kulipa mara moja, daladala zinafika hadi hapa (darajani) na kushusha abiria. Imekuwa wa huku wa huku na wa kule wa kule. Ukitaka kuvuka kwenda Dege, lazima utembee kwa miguu upande huu kidaraja cha mbao ambacho si salama, ndipo uvuke upande wa pili ili ukapande gari nyingine,” amesema Editha Luyembe.

Amesema, nauli awali ilikuwa Sh500, lakini sasa unaposhuka na kutembea kwenda kupanda gari nyingine inabidi ulipie tena Sh500, hivyo gharama imekuwa mara mbili.

Mwananchi mwingine, Jeremia Elisha, amesema kipande cha daraja kilichokatika kilipita gari la uzito mkubwa.

“Hii ni hatari, si salama kabisa. Tunashukuru hakujatokea madhara ya vifo, lakini kwa ujenzi huu daraja lilianza kutitia na hakuna kilichofanyika hadi sasa, limekatika kabisa,” amesema.

Mkazi mwingine ambaye ni ofisa usafirishaji kwenye eneo la Bamba, amesema daraja limekuwa kikwazo katika shughuli nyingi.

Amesema, kwa bodaboda unapopewa mzigo kupeleka eneo hilo, inabidi upaki pembeni na kubeba mzigo begani kuuvusha upande wa pili.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi.