Kwa muda mrefu, ndoa imekuwa ikitazamwa kama jambo la hisia, bahati au mapenzi yasiyo na maelezo.
Watu wengi huamini kuwa ndoa ikianza vizuri, basi itaendelea kuwa nzuri, au ikianza kwa shida, basi ni mkosi wa maisha.
Lakini utafiti wa kisayansi umeanza kubadilisha mtazamo huu.
Leo, sayansi inaonesha kuwa ndoa yenye furaha si bahati nasibu, bali ni matokeo ya tabia, mawasiliano na uamuzi yanayoweza kujifunzwa na kufanyiwa kazi.
Miongoni mwa wataalamu waliobadili kabisa namna dunia inavyoelewa ndoa ni Dk John Gottman, mwanasaikolojia wa Marekani ambaye amefanya utafiti wa zaidi ya miaka 40 juu ya uhusiano wa ndoa.
Kupitia kazi zake za kitafiti, ameweza kutabiri kwa usahihi mkubwa kama ndoa itadumu au itavunjika, kwa kuchunguza mawasiliano ya wenza kwa muda mfupi tu.
Matokeo yake yameweka msingi wa kile anachokiita “sayansi ya ndoa.”
Kwa mujibu wa Dk Gottman, ndoa yenye furaha haimaanishi kutokuwepo kwa migogoro.
Badala yake, ndoa yenye afya ni ile inayoweza kusimamia migogoro kwa njia salama na yenye heshima. Anaandika kwa uwazi: “Ndoa zenye mafanikio si zile zisizo na migogoro, bali ni zile zinazojua jinsi ya kusimamia migogoro.” Kauli hii inavunja dhana ya kuwa wanandoa wenye furaha hawagombani.
Ukweli ni kuwa wanagombana, lakini kwa njia inayojenga badala ya kubomoa.
Misingi ya kisayansi ya ndoa
Kupitia utafiti wake maarufu katika maabara ya uhusiano, Dk Gottman alibaini kuwa kuna tabia fulani zinazoharibu ndoa kwa kasi kubwa.
Aliita tabia hizi “Wapanda farasi wanne wa ndoa,” ambazo ni dharau, lawama, kujitetea kupita kiasi na kujitenga kihisia. Kati ya zote, dharau ndiyo hatari zaidi. Kuhusu hili, anaandika: “Dharau ni sumu kali zaidi katika ndoa.”
Kauli hii inaonyesha kuwa kejeli, matusi na kudharau hisia za mwenza huua polepole mapenzi na heshima.
Kinyume chake, ndoa zinazodumu zina sifa ya msingi mmoja muhimu sana: urafiki.
Kwa Dk Gottman, urafiki si jambo la pembeni katika ndoa, bali ni kiini chake. Anaeleza kuwa wanandoa wenye furaha wanajuana kwa undani, wanaheshimiana, na wanafurahia uwepo wa kila mmoja.
Katika maandiko yake anaandika: “Siri ya ndoa yenye furaha iko katika urafiki wa kina kati ya wanandoa.”
Hii inaonyesha kuwa mapenzi pekee hayatoshi; urafiki unaojengwa kila siku ndio unaobeba ndoa kwa muda mrefu.
Urafiki huu hujengwa kupitia mambo madogo madogo: kusikiliza mwenza, kujali hisia zake, kucheka pamoja, na kujibu maombi madogo ya ukaribu. Anabainisha kuwa wanandoa wenye ndoa imara hujibu maombi haya mara nyingi, hata kama ni kwa ishara ndogo. Anaandika: “Ndoa hudhoofika pale wenza wanapopuuzia maombi madogo ya kuunganishwa kihisia.”
Hii inaweka wazi kuwa kumpuuza mwenza mara kwa mara, hata bila ugomvi, kunaweza kuharibu ndoa.
Katika mtazamo wa kisayansi, ndoa ni kama akaunti ya benki ya kihisia. Kila tendo la wema, kusikiliza au kuthamini huongeza akiba, na kila tusi au dharau hupunguza.
Dk Gottman anaeleza kuwa ndoa imara huwa na uwiano mzuri wa hisia chanya dhidi ya hasi. Kwa maneno yake: “Katika ndoa zenye afya, mwingiliano chanya unapaswa kuzidi hasi kwa kiwango kikubwa.”
Hii inaonyesha kuwa si lazima ndoa iwe kamilifu, bali iwe na wingi wa mambo mazuri yanayozidi changamoto.
Kwa mujibu wa Dk Gottman, kufurahia ndoa ni matokeo ya juhudi za makusudi, si hisia za muda mfupi. Anasisitiza umuhimu wa kujenga maana ya pamoja katika ndoa.
“Ndoa hudumu pale wanandoa wanapojenga maana ya pamoja ya maisha, ” anaeleza.
Kauli yake inaonyesha kuwa ndoa si tu kuishi pamoja, bali ni kusafiri pamoja kimaono na kimaisha.
Anapinga wazo la kuwa lazima migogoro yote itatuliwe. Anabainisha kuwa asilimia kubwa ya migogoro katika ndoa ni ya kudumu, ikitokana na tofauti za tabia na maadili.
Badala ya kujaribu kubadilisha mwenza, anashauri wanandoa wajifunze kuishi na tofauti hizo kwa heshima. Anasema: “Migogoro mingi ya ndoa haiwezi kutatuliwa, bali inaweza kusimamiwa.” Kauli hii inawapa wanandoa uhuru wa kuacha vita visivyo na mwisho na badala yake kujenga uelewano.
Katika kufurahia ndoa, anaweka mkazo mkubwa kwenye lugha ya mawasiliano. Anashauri wanandoa waanze mazungumzo magumu kwa upole badala ya lawama.
“Mazungumzo yanayoanza kwa ukali mara nyingi huisha vibaya, anasema na kusisitiza kuwa namna ya kuanza mazungumzo ni muhimu kuliko hoja yenyewe. Kauli laini hujenga nafasi ya kusikilizana na kuelewana.
Sayansi ya Dk Gottman pia inaonyesha umuhimu wa heshima na shukrani. Wanandoa wanaodumisha ndoa zao huonyesha kuthaminiana hata katika mambo madogo.
Anaandika: “Shukrani ni chanjo ya ndoa dhidi ya kudharau.” Hii inaonyesha kuwa kusema asante, kuona juhudi za mwenza, na kuthamini mchango wake huimarisha ndoa dhidi ya sumu ya dharau.
Usalama wa kihisia na mradi wa maisha
Dk Gottman anasisitiza kuwa ndoa yenye furaha ni ile inayotoa usalama wa kihisia.
Mwenza anapaswa kuwa mahali salama pa kurudi, si chanzo cha hofu. Anaandika: “Ndoa yenye afya ni ile ambayo mwenzi wako anajua yuko salama kwako.”
Kauli yake inaweka wazi kuwa furaha ya ndoa haipimwi kwa picha nzuri au zawadi kubwa, bali kwa hisia ya kuaminiana na kukubaliana.
Kwa mtazamo wa kisayansi wa Dk Gottman, ndoa si fumbo lisiloeleweka, bali ni mfumo unaoweza kujengwa na kuboreshwa.
Furaha ya ndoa haitokani na kutokuwepo kwa matatizo, bali na uwezo wa wanandoa kushughulikia changamoto kwa heshima, urafiki na ufahamu.
Ndoa inayodumu ni ile inayolindwa kila siku kupitia maneno, matendo na uchaguzi mdogo mdogo.
Katika jamii inayokumbwa na ongezeko la migogoro ya ndoa, sayansi ya Gottman inatoa matumaini mapya. Inaonyesha kuwa upendo unaweza kufundishwa, mawasiliano yanaweza kuboreshwa, na ndoa inaweza kufurahiwa kwa makusudi.
Kwa wanandoa, ujumbe ni mmoja: ndoa yako si bahati, ni mradi wa maisha unaohitaji uelewa, juhudi na sayansi ya mapenzi.
Makala haya kwa hisani ya vyanzo mbalimbali vya kimtandao.
