Global Publishers
March 22, 2026
0 Comments
Johannesburg: Naibu Waziri wa Uchukuzi, ambaye pia ni Rais wa Red Cross Tanzania, David Kihenzile, ametembelea ofisi za Red Cross jijini humo na kukutana na viongozi wakuu wa Southern African Red Cross Society, akiwemo rais na katibu mkuu.
Katika kikao hicho, viongozi hao walijadili namna bora ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na South Africa, hususan katika kuendeleza shughuli za kujitolea (volunteerism) pamoja na kuimarisha mahusiano ya kimataifa.

Majadiliano yaligusia maeneo muhimu ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo, usimamizi wa majanga, huduma za afya, maendeleo ya rasilimali watu pamoja na sheria za kibinadamu (Humanitarian Law).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, International Federation of Red Cross and Red Crescent Societies ndicho chombo kinachoongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wanavoluntia, wanaofanya kazi kupitia matawi takribani 200,000 katika nchi 191 duniani.
Aidha, imeelezwa kuwa Red Cross Tanzania ilikuwepo hata kabla ya uhuru wa nchi, na baada ya Tanzania kupata uhuru ilianzishwa rasmi kwa Sheria Na. 71 ya mwaka 1962, kufuatia pia azimio la United Nations la mwaka 1947. Kwa sasa, shirika hilo limeenea katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.

