UNA mabao ya Yanga yapo nje kutokana na mitambo ya mabao kupata majeraha na kupewa muda wa kupumzika ili kutibiwa irejee kwenye ufiti. Kukosekana kwao kumechambuliwa na watalamu jinsi inavyoleta athari hasi.
Katika mechi 15 Yanga imeshinda 11, sare nne, inamiliki mabao 31, imefungwa mawili, ina pointi 37. Kati ya mabao hayo Prince Dube kafunga sita, Laurindo Dilson Depu sita, Dickson Job bao moja na Israel Mwenda asisti tatu. Mastaa hao wanasumbuliwa na majeraha.
Kwa ujumla wameshachangia mabao 13 na asisti tatu, jambo linalothibitisha mchango wao mkubwa katika kikosi hicho kwenye safari ya kutetea ubingwa baada ya kuchukua mara nne mfululizo.
Endapo Pacome Zouzoua asingerejea kikosini baada ya kukaa nje kuuguza majeraha basi jumla ya mabao 16 na asisti tano yangekuwa nje, lakini urejeo wake unakwenda kuongeza nguvu.
Ukiachana na rekodi ya msimu huu, ukimzungumzia mshambuliaji Clement Mzize wa misimu miwili iliyopita, ambapo 2024/25 alikuwa na mabao 14, asisti tano, 2023/24 alikuwa na mabao sita, asisti saba, kukosekana kwake kumeendelea kupunguza idadi ya mabao kikosini.
Katika hilo huwezi kumuweka kando beki wa kati wa klabu hiyo Ibrahim Abdulla ‘Bacca’, licha ya kufanya majukumu yake ya ulinzi kikamilifu. Ikumbukwe msimu uliopita alikuwa na mchango wa mabao matano kati ya 83 na Yanga ilikuwa bingwa kwa pointi 82.
Alivyoanza msimu huu Dube, kabla ya kupumzika nje kujisikilizia hali yake, uliopita alimaliza na mabao 13 na asisti nane. Pacome aliyerejea kikosini alikuwa na mabao 12, asisti 10, wakati Chadrack Boka alimaliza na asisti tatu. Hii inaonyesha umuhimu wao kikosini.
Kitendo cha Dube, Depu, Bacca, Job, Boka kupata jeraha kinaleta athari kama wanavyozungumza mastaa wa zamani wa klabu hiyo, huku wakiona ahueni kurejea kwa Pacome.
Staa wa zamani, Mohamed Hussein ‘Mma chinga’ alisema: “Kasi ya kufunga imepungua. Waki wepo Dube na Mzize unakuwa na uhakika wa kupata mabao kwani unajua yoyote anaweza kufunga wakati wowote.”
Mma chinga aliyeweka rekodi ya mabao 26 miaka 27 iliyopita, aliongeza: “Wachezaji hao ni muhimu hasa mzunguko wa pili unaoamua nani bingwa tena. Mbali na Dube na Mzize, Depu alianza kwa kasi kubwa na huenda angemaliza msimu huu akiwa na mabao zaidi ya 10. Ingawa sina wasiwasi na jumla ya mabao, naona yanaweza kuzidi ya msimu uliopita.”
Mchezaji mwingine wa zamani, beki Oscar Jashua, alisema: “Mchezaji anayetegemewa kikosi cha kwanza kuipa timu matunda, anapopata changamoto kuna namna kikosi kinayumba. Naamini wangekuwepo kwa mechi ambazo hawajacheza basi wangefunga.” Kipa wa zamani Benjamin Haule alisema: “Mchezaji anayecheza panga pangua kikosi cha kwanza, akipata changamoto ya jeraha kuna namna kikosi kinayumba kama hatatokea mchezaji kuziba pengo lake. Japokuwa Pacome atahitaji mechi tatu za kumrejeshea ufiti, uwepo wa Dube, Depu na Mzize uwanjani una mchango mkubwa pia kuumia kwa pamoja Job na Bacca kunakuwa changamoto.”
Mechi 15 za Ligi Kuu za Yanga za msimu 2024/25 zilikuwa na mabao 31 sawa na ya msimu huu, ilifungwa mabao sita ila sasa imeruhusu mawili, ilivuna pointi 36 tofauti na sasa ina alama 37.