MASHEKHE WAMPONGEZA MBUNGE LUTANDULA KUFUTURISHA WAISLAMU

Mbunge wa Jimbo la Chato Kusini,Pascal Lutandula

………….

MASHEKHE wa Bakwata Jimbo la Chato Kusini wamepongeza matendo ya huruma yaliyoonyeshwa na Mbunge wa Jimbo hilo Pascal Lukas Lutandula baada ya kuwafuturisha waislamu wasiojiweza katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti katika Sikukuu ya Eid El-Fitr na Mashekhe wa misikiti ya Bakwata Bwanga, Buseresere pamoja na Nyakayondwa.

Sherehe za Sikukuu ya Eid El-Fitr hufanyika kila mwaka baada ya waumini wa dini ya Kiislamu kumaliza funga ya siku 30 kama yalivyo mafundisho ya Mtume Muhammad.

Shekhe mkuu Bakwata Kata ya Bwanga, Alhaj Thabit Ally, amesema kitendo cha Mbunge wao kuamua kuwafuturisha waislamu katika mwezi mtukufu wa Ramadhan ni cha kiungwana sana na kwamba malipo ya wema huo yatajibiwa na Mwenyezi Mungu pekee na siyo wanadamu.

“Licha ya hivi karibuni kupokea swadaka ya Iftar kutoka kwa Mbunge Lutandula, nimeshangaa tena leo kupokea taarifa za kukabidhiwa swadaka kubwa zaidi ambayo ni ng’ombe, mchele, mafuta,soda, maji na juisi kwa lengo la kuhakikisha waislamu tunasherehekea sikukuu hii kwa furaha”.

“Ama hakika Mwenyezi Mungu amjazie Baraka nyingi na kumwepusha na mabalaa Mbunge wetu, tunamuahidi sisi waislamu tutaendelea kumwombea mema kwa Mwenyezi Mungu ili uongozi wake ukaendelee kugusa maisha ya wananchi hasa wenye uhitaji kama alivyotutendea sisi” amesema Shekhe Thabiti.

Shekhe Mkuu Bakwata Kata ya Buseresere, Alhaj Ibrahimu Mtambo, amesema kitendo kilichofanywa na Mbunge Lutandula kwa waumini wa Kiislamu ni cha kiungwana sana huku akidai moyo wa jinsi hiyo wamejaaliwa watu wachache.

Amewataka watu wengine kuiga mfano ulioonyeshwa na Mbunge huyo ili kujitwalia thawabu nyingi mbele ya Mwenyezi Mungu na kujiandalia kiama chema huko peponi.

“Ukweli ni kwamba licha ya kuwa Shekhe kwa muda mrefu bado sijawahi kuona Mbunge mwenye moyo wa kujitoa kama Lutandula, huyu amekuwa kiongozi wa kipekee sana kwetu, ametushika mkono katika funga yetu nasi tunamuahidi kumpa ushirikiano wa kila aina ili atimize ndoto zake na kuwatumikia kwa wema wananchi wa Jimbo la Chato Kusini”,

” Tunamshukuru sana kwa kutuletea ng’ombe, mchele na mahitaji mengine kwaajili ya kuwafanya waislamu wa Buseresere kusherehekea Eid El-Fitr kwa furaha na amani, tunakiri kupokea na Mwenyezi Mungu azidi kumfungulia ridhiki katika kazi zake na kumjazia afya njema siku zote” amesema Shekhe Mtambo.

Awali mwakilishi wa Mbunge wa Jimbo la Chato Kusini, Joseph James, amesema Mbunge Lutandula ameamua kuungana na waislamu wa Jimbo la Chato Kusini katika kusherehekea sikukuu ya Eid El-Fitr kwa kuwapatia ng’ombe wawili kwaajili ya chakula, mchele, mafuta ya kupikia, katoni za maji, soda pamoja na juisi.

James ambaye pia ni msaidizi wa Ofisi ya Mbunge huyo, amesema mbali na sadaka hiyo, Mbunge amewausia waislamu wote kuendelea kuyaishi matendo mema kama walivyojitakasa katika funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Kadhalika ameitaka jamii kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano pasipo kubaguana kwa itkadi za dini, vyama wala makabila, badala yake watambue kuwa wote tunaunganishwa na utanzania wetu.

Upo msemo usemao kuwa “Mtu mwenye busara haweki hazina kwaajili yake anavyotoa zaidi kwa wengine ndivyo anavyopata zaidi na zaidi”.