Msimu huu namba za Yanga zinakataa, mtihani uko hapa!

NAMBA ambazo Yanga walizitengeneza msimu uliopita wa ligi 2024-2025, zinaonekana kuwakimbia msimu huu wa 2025-2026 na watatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kuzifikia  huku mambo yakionekana kutowaendea vizuri.

Yanga ambao wamemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara wakiwa kileleni, jana walianza mzunguko wa pili kwa kuambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo mkali wa ligi hiyo uliopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Deni ambalo wanalo Yanga linatokana na takwimu zilivyo hadi kufikia sasa kulinganisha na ilivyokuwa msimu uliopita ambao Yanga ilitetea taji lake ikibeba kwa mara ya nne mfululizo.

Wakati Yanga inabeba ubingwa huo, ilimaliza na pointi 82 baada ya kucheza jumla ya mechi 30, ikishinda 27, sare moja na kupoteza mbili, huku ikifunga mabao 83 yakiwa mengi zaidi kuliko timu nyingine na kuruhusu kumi, ambayo ni machache zaidi.

Hata hivyo, sare ya jana  inaonekana kuwaweka pabaya vijana hao wa Jangwani ambao kwenye mzunguko wa kwanza wenye pointi 45 walimaliza wakiwa na pointi 37 wakiwa wamedondosha pointi kumi baada ya kutoka sare michezo mitano kwenye ligi hadi sasa.

Yanga imetoka sare na Mbeya City, Simba, TRA, Azam na Mtibwa na hivyo kudondosha idadi hiyo ya pointi wakati msimu uliopita timu hiyo ilitoka sare mchezo mmoja pekee dhidi ya JKT Tanzania na ikapoteza michezo miwili dhidi ya Azam na Tabora ambayo kwa sasa inaitwa TRA.

Yanga inaonekana kuwa na mtihani kwenye maeneo yote matatu muhimu kwenye ligi msimu huu.

 Iko hivi, msimu uliopita Yanga ilimaliza ligi na pointi 82 kuanzia mchezo wa jana, hadi mingine 14 ijayo Yanga ilitakiwa kupata  pointi 45, kama ingefanikiwa kushinda michezo yote ina maana kuwa ingemaliza  msimu na pointi 82 sawa na zile ambazo ilimaliza nazo msimu uliopita, lakini kutokana na sare hiyo sasa Yanga imedondosha pointi kumi na hivyo ikishinda michezo iliyobaki yote itamaliza na pointi 80, mbili nyuma ya zile za msimu uliopita.

Sehemu nyingine ambayo Yanga inatakiwa kuifanyia kazi ni eneo la kufunga mabao ambalo msimu uliopita walikuwa na kasi nzuri ambapo walifanikiwa kufunga mabao 83 na kuwa timu ambayo iliyofunga mabao mengi kwenye ligi.

Sasa Yanga imefanikiwa kufunga mabao 32 kwenye ligi, hivyo wanalazimika kuhakikisha hadi mwisho wa msimu wanafunga mabao 51 ili kufikia rekodi yao, namba hizi zinaonekana kuwa mtihani mzito kwa kocha Pedro Concalves pamoja na vijana wake kutokana na mwenendo usioridhisha kwenye eneo la ushambuliaji.

Kuonyesha kuwa huu ni mtihani katika michezo minne ambayo Yanga imetoka sare iliambulia suluhu, hivyo washambuliaji wa timu hiyo wanatakiwa kubadilisha kasi yao uwanjani.Hata hivyo, kwenye takwimu za kuruhusu mabao haionekani kama kuna tatizo kubwa kwa Yanga kwa kuwa hadi sasa timu hiyo imeonekana kuwa na safu nzuri ya ulinzi ikiwa imeruhusu mabao matatu tu kwenye michezo 16, inachotakiwa kufanya ili kuwa na uwiano sawa na kutoruhusu zaidi ya mabao saba kwenye michezo iliyobaki.

Katika mchezo wa jana, Yanga ikiwa kwenye Uwanja wa Jamhuri ambao ulionekana kutokuwa kwenye hali nzuri kutokana na mvua, ilifanikiwa kujipatia bao lake lake kupitia kwa Pacome Zouzoua dakika ya 24 ambaye amefikisha mbao manne kwenye ligi msimu huu.

Hata hivyo Mtibwa walionekana kucheza kwa tahadhari kubwa na kufanikiwa kusawazisha bao hilo katika dakika ya 90 kupitia kwa Ismael Mhesa kwa mipra wa kona na kufanya matokeo kuwa 1-1.

Kwa upande wa Mtibwa haya yalikuwa matokeo yao mazuri wakiwa timu ya kwanza msimu huu kutoka sare na Simba na Yanga kwenye ligi.

Hata hivyo, baada ya mchezo kumalizika Djigue Diarra alimvaa mwamuzi na kuondolelea na viongozi wa benchi la ufundi la timu hiyo, lakini akawa anagoma.