JOHANNESBURG: Naibu Waziri wa Uchukuzi, ambaye pia ni Rais wa Red Cross Tanzania David Kihenzile, ametembelea ofisi za Red Cross jijini Johannesburg, ambako alikutana na viongozi wakuu wa Southern African Red Cross Society akiwemo rais na katibu mkuu, na kujadili namna bora ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini, hususan katika kuendeleza shughuli za kujitolea (voluntia) na kuimarisha mahusiano ya kimataifa.
Majadiliano hayo yaligusia maeneo mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo, usimamizi wa majanga, huduma za afya, maendeleo ya rasilimali watu pamoja na sheria za kibinadamu (Humanitarian Law).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, International Federation of Red Cross and Red Crescent Societies ndicho chombo kinachoongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wanavoluntia, wanaofanya kazi kupitia matawi takribani 200,000 katika nchi 191 duniani.
Aidha, imeelezwa kuwa Red Cross Tanzania ilikuwepo hata kabla ya uhuru wa nchi, na baada ya Tanzania kupata uhuru ilianzishwa rasmi kwa Sheria Na. 71 ya mwaka 1962, kufuatia pia azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 1947. Kwa sasa, shirika hilo limeenea katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)