ONGEA NA ANTI BETTI: Mchumba wangu ‘kilaza’ wa teknolojia, nifanyeje?

Nina mchumba, hivi karibuni nilipata nafasi ya kumtembelea mahali akiwa na rafiki zake nilichojifunza hajui vitu vingi kwani hata vitu vya kawaida alikuwa akishangaa hasa kuhusu teknolojia.

Najiuliza hata simu yake ya mkononi huwa anaitumia kupiga tu au vipi. Kwani hajui hata vitu vinavyopatikana kwenye simu. Pia kingine rafiki zake wanamuelekeza kila mara kwa maana katika kundi lao wanamjua kama ni kilaza.

Pamoja na kuwa mfanyabiashara kuna vitu wakati huu wa sayansi na teknolojia unapaswa uvifahamu. Nifanyeje kumtoa katika ujima huu alionao?

Pole sana. Lakini jambo la kwanza muhimu ni kutambua kuwa kutokujua si ujinga, ni hatua ya mwanzo ya kujua, inawezekana hajapata mwongozo sahihi au mazingira ya kujifunza.

Kabla hujaanza kumsaidia, badili mtazamo wako. Ukianza kwa kumwona kama kilaza, hata bila kusema, atahisi dharau. Badala yake, muone kama mtu mwenye uwezo ambao haujafunguliwa, yaani ana uwezo ila hajui kama anao.

Kumbuka, kuna watu wana akili kubwa sana kwenye biashara au maisha ya vitendo lakini hawajawahi kupewa nafasi ya kujifunza teknolojia au mambo ya kidijitali.

Tafuta muda mzuri mkiwa wawili, kisha zungumza naye kwa upole.

Badala ya kumwambia hajui vitu, unaweza kumwonyesha kuna mambo ya teknolojia na maarifa ya kidijitali yanayoweza kumsaidia kwenye biashara zake, na ungependa mjifunze pamoja. Neno ‘pamoja’ lina nguvu sana, kwani atajiona anafundishwa kwa sababu ni dhaifu, bali kama mshirika katika safari ya ukuaji.

Una nafasi kubwa ya kumjenga kisaikolojia. Mwonyeshe mambo mazuri unayoona kwake, kama bidii yake kwenye biashara, uaminifu au juhudi zake za maisha. Mtu akijua ana thamani, huwa tayari kujifunza zaidi bila woga wa kuonekana hajui.

Katika kumsaidia kwa vitendo, anza na mambo madogomadogo yanayomuhusu moja kwa moja. Mfano, mfundishe jinsi ya kutumia simu yake zaidi, kama kutafuta taarifa kupitia Google, kuangalia mafunzo YouTube.

Unaweza pia kwa kutumia simu yake ikaielekeza Akili Unde (AI) imuandalie ripoti ya mapato na matumizi kwenye biashara zake, huku ukimueleza kuwa badala ya kumuajiri mtu aanze mwanzo kumpangia hesabu zake atafanya mwenyewe kwani teknolojia itakuwa imemrahisishia kazi.

Usimpe mambo mengi kwa wakati mmoja, kufanya hivyo kunaweza kumchanganya au kumkatisha tamaa. Hatua ndogo lakini za mara kwa mara huleta mabadiliko makubwa.

Kwa kuwa ni mfanyabiashara, muonyeshe jinsi teknolojia inavyoweza kuongeza wateja, faida na kurahisisha mawasiliano. Akiona manufaa ya moja kwa moja, atakuwa na hamasa ya kujifunza zaidi.

Zingatia na muhimu kutomfanya ajione mdogo mbele za watu au marafiki zake. Hata kama unaona mapungufu yake, muheshimu. Mtu anayehisi anaheshimiwa huwa na nguvu ya kubadilika.

Pia, kama marafiki zake yanamjengea taswira hasi, unaweza kumshauri awe karibu na watu wanaomchochea kukua na si wanaomdharau. Mazingira yana mchango mkubwa sana katika maendeleo ya mtu.

Hata hivyo, kuna swali la msingi la kujiuliza kwa utulivu moyoni mwako je, yeye yupo tayari kujifunza na kukua, au hana kabisa hamasa ya kubadilika? Tofauti ya maarifa inaweza kurekebishika kirahisi ikiwa mtu ana moyo wa kujifunza.

Kwa jumla, usimchukulie kama tatizo bali kama mtu aliye kwenye hatua tofauti ya kukua.