Paskazia alivyopambania elimu ya mwanaye mwenye ulemavu

Tanga. Katika kijiji kidogo cha Mjesani wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga kuna simulizi inayogusa moyo na kutoa somo kubwa kuhusu nguvu ya upendo wa mama.

Ni hadithi ya mwanamke aliyepambana na changamoto za maisha, umaskini na maumivu ya kutelekezwa, lakini hakukata tamaa katika ndoto yake ya kuona mwanaye mwenye ulemavu akipata elimu bora.

Huyu ni Paskazia Yohana, mama jasiri ambaye kwa miaka mingi alipambana peke yake kumlea mwanaye mwenye ulemavu wa viungo hadi kufanikiwa kumfikisha chuo kikuu, ndoto ambayo wengi hawakuamini ingewezekana.

Safari yake ni ushuhuda kwamba, mapambano ya mama hayapimwi kwa mali aliyonayo, bali kwa moyo wake wa kutokata tamaa.

Paskazia ni mama aliyelazimika kulea mtoto mwenye ulemavu wa viungo Jonathan Kilenga katika mazingira magumu ya kiuchumi, hali iliyomlazimu kubeba jukumu la malezi peke yake bila msaada wa uhakika kutoka kwa familia wala jamii.
Hata hivyo, hakuruhusu hali hiyo imvunje moyo, bali aliigeuza kuwa sababu ya kupambana zaidi.

Akielezea mwanzo wa changamoto zake, anasema ndugu zake walitamani kumsaidia lakini hali yao ya kiuchumi haikuruhusu.

Kila mmoja alikuwa na majukumu yake ya kifamilia, jambo lililomfanya ajikute akibeba mzigo huo peke yake huku akijitahidi kuhakikisha mwanaye anapata maisha bora.

“Nilikuwa napambana mimi mwenyewe na akili yangu pamoja na Mungu. Ndugu zangu walitamani kunisaidia lakini kila mmoja alikuwa na hali yake,” anasema Paskazia kwa sauti ya utulivu lakini yenye msisitizo wa uzoefu alioupitia.

Anasema changamoto zake zilianza hata kabla ya mtoto kuzaliwa, pale mume wake alipokuwa akifanya kazi na kupangiwa kwenda Zanzibar wakati yeye akiwa mjamzito.

Anansema hali hiyo iliongeza sintofahamu katika maisha yake na kumfanya aanze kuhisi upweke mapema.

Baada ya kujifungua, mambo yalibadilika zaidi pale baba wa mtoto alipogundua kuwa mtoto ana ulemavu. Tukio hilo lilikuwa mwanzo wa kuvunjika kwa mahusiano yao, hali iliyomuacha Paskazia katika hali ya sintofahamu.

Paskazia Yohana Mkazi wa Kijiji cha Mjesani katika wilaya ya Mkinga akiwa amerejea nyumbani muda mfupi mara baada ya kurejea akitokea  kwenye shughuli zake za kilimo cha mazao ya chakula na mbogamboga.

“Nilivyojifungua na kumwonesha mtoto, ndipo mahusiano yetu yalipoanza kukatika,” anasimulia kwa huzuni, akionesha namna tukio hilo lilivyobadilisha maisha yake kwa ghafla.

Hatimaye, mwanamume huyo aliondoka kabisa na kumuacha Paskazia akilea mtoto peke yake, bila msaada wowote wa karibu. Huo ulikuwa mwanzo wa safari yake ya kweli ya mapambano.

Anasema kipindi hicho kilikuwa kigumu sana kisaikolojia, hadi kufikia hatua ya kukosa usingizi kwa muda mrefu akiwaza namna ya kumlea mtoto wake katika mazingira magumu aliyokuwa nayo.

Hata hivyo, hakukata tamaa aliamua kumkabidhi Mungu kila jambo na kuamini kuwa ipo siku hali itabadilika. Anasema imani hiyo ndiyo iliyompa nguvu ya kuendelea kupambana bila kuangalia nyuma.

Katika malezi, changamoto kubwa ilikuwa ni upatikanaji wa chakula na mahitaji muhimu, anasema mara nyingi alilazimika kufanya vibarua ili kupata kipato kidogo cha kujikimu.

Anasema alilima mashamba ya watu, akifanya kazi ngumu kwa ujira mdogo lakini kwa moyo wa matumaini, lengo lake lilikuwa kuhakikisha mwanaye hapati njaa na anaendelea kuishi katika mazingira salama.

Katika hatua za awali za makuzi ya mtoto, Paskazia hakumpeleka shule mara moja, badala yake, alianza kumfundisha nyumbani kwa kutumia vitabu vya “Soma kwa Hatua,” akitumia muda wake mwingi baada ya kazi kumlea na kumfundisha.

Hatua hiyo anasema ilimsaidia mtoto kuelewa masomo mapema na hata kufikia uwezo wa kusoma magazeti, jambo lililowashangaza watu wengi waliokuwa wakimfahamu.

Anasema alipoanza shule ya chekechea, walimu walibaini haraka uwezo wake mkubwa wa kuelewa na kushiriki darasani, jambo lililompa Paskazia matumaini makubwa kuhusu mustakabali wa mwanaye.

Anasema jamii haikumtenga moja kwa moja, lakini haikuwa na msaada wa kutosha kumwezesha. Hivyo, anasema aliendelea kujitegemea katika kila hatua ya maisha yake.

Mabadiliko makubwa yalianza kuonekana baada ya kuibuka Kituo cha YDCP jijini Tanga, kilichotoa mwanga mpya katika maisha yake na ya mwanaye.

Kupitia kituo hicho, anasema alihamasika zaidi kumuendeleza mwanaye kielimu na kuhakikisha anapata nafasi sawa na watoto wengine katika jamii.

Hata hivyo, safari haikuwa rahisi, anasema kulikuwa na nyakati za kukatisha tamaa, hasa pale mwanaye alipofeli kujiunga na kidato cha kwanza.

Anasema tukio hilo lilimuumiza sana lakini hakuruhusu limvunje moyo, aliendelea kumtia moyo mwanaye na kufanya jitihada zaidi hadi pale alipopata nafasi nyingine ya kuendelea na masomo.
Hatimaye, mwanaye alipata nafasi ya kujiunga na masomo ya sekondari na kuanza kufanya vizuri darasani, hatua iliyompa Paskazia nguvu mpya ya kuendelea na mapambano.

Katika maisha yake, anasema alifanya uamuzi mgumu kwa manufaa ya mwanaye, ikiwa ni pamoja na kuamua kutozaa mtoto mwingine ili aweze kumlea vizuri mtoto huyo mwenye uhitaji maalumu.

“Sikutaka kuzaa mtoto mwingine, niliona huyu anahitaji malezi ya karibu zaidi,” anasema kwa msisitizo, akionesha namna alivyokuwa tayari kujitoa kwa ajili ya mwanae.

Safari ya chuo kikuu ilipofika, anasema changamoto ziliongezeka zaidi kutokana na mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya ada na matumizi ya kila siku.

Paskazia anasema aliongeza juhudi kwa kujikita zaidi katika kilimo, akilima mazao mbalimbali na kuyauza ili kupata fedha za kumsaidia mwanaye.

“Nilikuwa nauza mazao na kumtumia fedha ya ada kwa awamu pamoja na matumizi yake ya kila siku,” anasema.
Kadiri mahitaji yalivyoongezeka, anasema alianzisha pia bustani ya mboga mboga ili kupata kipato cha haraka na kuendelea kumsaidia mwanae bila kukata tamaa.

Katika kipindi hicho, anasema wafadhili walijitokeza na kumsaidia mwanaye kulipiwa ada ya mwaka mzima, hatua iliyompa Paskazia nafuu kubwa na matumaini mapya.

Anasema hapo ndipo alipoona wazi kuwa, Mungu ameanza kujibu maombi yake ya muda mrefu aliyokuwa akifanya mchana na usiku.

Hatimaye, mwanaye ambaye anajulikana Jonathan alifanikiwa kuhitimu chuo kikuu, hatua iliyokuwa ndoto ya muda mrefu kwa familia hiyo.

Baada ya kuhitimu, alipata ajira katika halmashauri moja mkoani Mbeya, jambo lililobadilisha kabisa mwelekeo wa maisha yao.
Siku alipopata taarifa hiyo ilikuwa ya kipekee sana katika maisha ya Paskazia. Anasema alikuwa shambani akilinda mazao yake dhidi ya wanyama waharibifu alipopigiwa simu na mwanaye.

“Nilinyanyua mikono juu na kumshukuru Mungu, nililia kwa furaha nikikumbuka nilikotoka na yote niliyopitia,” anasimulia kwa hisia.
Leo hii, maisha ya Paskazia yamebadilika kwa kiasi kikubwa. Mwanaye ndiyo tegemeo lake kuu na anamhudumia kwa upendo mkubwa, akimheshimu kwa juhudi alizofanya.

Anasema hata nyumba ninayoishi kwa sasa ameijenga mwanaye huyo, jambo linaloonesha matunda ya uvumilivu na mapambano ya muda mrefu aliyopitia katika kipindi hicho.

Paskazia anasema safari yake ni ushindi wa imani, uvumilivu na jitihada za mwanamke asiyejua kukata tamaa.

Anatoa wito kwa jamii kuacha kuwanyanyapaa watoto wenye ulemavu na badala yake kuwapa nafasi ya kupata elimu na kujitegemea.

“Watoto hawa wana uwezo kama wengine, wanahitaji tu nafasi na malezi sahihi ili wafikie ndoto zao,” anasisitiza.
Simulizi yake inaacha funzo kubwa kuwa mwanamke anayeweza kufikia malengo yake bila kukata tamaa, hata katika mazingira magumu zaidi.

Ni hadithi ya ujasiri, matumaini na mafanikio inayopaswa kuwa mfano kwa jamii nzima.

Jamii inaelekezwa kuwekeza katika elimu, kuondoa unyanyapaa na kuwaunga mkono wazazi wanaolea watoto wenye ulemavu ili kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi sawa ya kufikia ndoto zake na kuchangia maendeleo ya Taifa.