Ruto, Gachagua wanavyotupiana maneno majukwaani, mbio za uchaguzi 2027

Joto la Uchaguzi Mkuu wa Kenya 2027 limeanza kupanda huku mijadala ikielekezwa zaidi kwenye majibizano ya majukwaani ya wanasiasa waandamizi, badala ya hoja za msingi zinazogusa maisha ya wananchi.

Rais William Ruto ameendelea kujikuta katika mvutano wa kisiasa na aliyekuwa mshirika wake wa karibu, Rigathi Gachagua. Wawili hao, waliowahi kushirikiana katika uongozi wa juu wa nchi hiyo, sasa ni mahasimu wakubwa, wakitumia majukwaa ya hadhara kurushiana maneno makali.

Katika mikutano yao inayofanyika maeneo mbalimbali nchini humo, mijadala imechukua mkondo wa kushambulia maisha binafsi badala ya kuwasilisha dira na sera mpya kuhusu watakavyowahudumia wananchi iwapo watapata madaraka.

Hali hiyo imeibua wasiwasi miongoni mwa wachambuzi wa siasa za ukanda wa Afrika Mashariki wanaofuatilia kwa karibu, wakihofia kuwa mwelekeo huo unaweza kupotosha mjadala wa kitaifa na kupunguza ubora wa ushindani wa kisiasa.

Kwa kawaida, kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu hutumika kama jukwaa la wagombea kueleza mikakati yao ya kuboresha uchumi, ajira, elimu na huduma za kijamii.

Hata hivyo, hali inayoonekana sasa nchini Kenya inaashiria kupungua kwa uzito wa hoja za maendeleo na kuongezeka kwa siasa za mvutano binafsi huku kila upande ukimshambulia mwenzake.

Wapo wanaoamini kuwa majibizano hayo, yakidumu katika miezi 15 ijayo kabla ya uchaguzi, yanaweza kuathiri namna wananchi watakavyofanya uamuzi wao. Badala ya kuchagua viongozi kwa misingi ya sera, kuna hatari ya uchaguzi kugeuka kuwa mashindano ya hisia na ushawishi wa kisiasa.

Taswira ya siasa za Kenya ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikifuatiliwa kwa karibu katika ukanda wa Afrika Mashariki, inaweza kubadilika na kuathiri imani ya wananchi katika mifumo ya kidemokrasia.

Katika mikutano ya mwanzoni mwa juma hili, chombo cha habari cha Citizen TV kilimnukuu Gachagua akisema anakuja na kaulimbiu: “Fagia Kasongo (Ruto) na kundi lake,” akidai kuwa uongozi huo umejikita katika kujilimbikizia mali za umma badala ya kuwanufaisha wananchi wote.

“Hatuwezi kumuacha Ruto apumzike katika miezi 15 iliyobaki. Tutaendelea kumuanika; na vijana wangu hawa mnaona jinsi alivyokonda hadi masikio yanapanda, na bado tutaendelea kumuanika,” amesema Gachagua, ambaye ni kiongozi mkuu wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP).

Hata hivyo, Ruto alimjibu kwa kudai kuwa mtu mwenye chuki na kisirani hawezi kuwa na ujumbe wa maana kwa wananchi, akiongeza kuwa wapinzani wake wamekula kupita kiasi.

“Nawaambia waende wakajiangalie kwanza kwenye kioo jinsi walivyokaa, vichwa vimevimba, na matumbo yamejaa hadi yanararua mashati. Punguzeni kula chakula kingi na muache kulala kwenye mikutano,” amesema.

Ruto, ambaye pia ni kiongozi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), ameongeza kuwa kutokana na miili yao mikubwa, wakati mwingine wamekuwa wakichafua hali ya hewa wanapolala, huku akijisifia kuwa anajua wakati wa kupunguza uzito ili aweze kushughulikia matatizo ya wananchi kwa ufanisi.

Mchambuzi wa siasa za Afrika Mashariki, Lugete Mussa amesema siasa zinazoendelea Kenya kwa sasa hazilengi maslahi ya wananchi bali zimejikita katika ukabila, ukanda na kulinda maslahi ya vigogo.

Amesema eneo la Mlima Kenya lina wapigakura wengi, hivyo Ruto alimchagua Gachagua kuwa Naibu wa Rais, si kwa sababu ya mapenzi ya kisiasa, bali kwa mvuto wake wa kupata kura.

Amesema baada ya kuingia madarakani, Gachagua alianza kujenga mtandao wa kisiasa uliolenga kumdhoofisha Ruto akijipanga na mwaka 2027 lakini bahati mbaya mpango wake ulifichuka na akang’olewa kisheria baada ya miaka miwili tu.

Kwa mujibu wa mchambuzi huyo, Gachagua anaamini kuwa kutokana na asili yake ya Mlima Kenya ana nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi ujao, hivyo analazimika kujijengea mtandao wa kisiasa ili kumchafua mpinzani wake.

Amesema juhudi hizo zimeambatana na jitihada za kukivuruga Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), ambacho kwa sasa kina mgawanyiko wa ndani wapo wanaomuunga mkono Ruto na wengine wanapinga msimamo huo.

“Ukiangalia mvutano unaoendelea, hauhusiani na masilahi ya Wakenya wala masuala muhimu kama sheria ya ardhi au gharama za maisha. Badala yake, kila upande unamshutumu mwenzake kwa ufisadi huku ukijiandaa kwa uchaguzi wa 2027,” amesema.

Amesema hali hiyo inaathiri wananchi kwa kuwa, muda mwingi unatumika katika kujibu propaganda badala ya kushughulikia changamoto halisi.

Amesema Kenya bado haijatulia kufuatia vuguvugu la vijana, na uchaguzi ujao unatarajiwa kuwa na ushindani mkali. Hali hiyo, amesema, ndiyo inayomfanya Ruto kujipanga kimkakati kulinda nafasi yake.