Sababu Tanzania kuendelea kukumbwa na uhaba wa maji

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Maji Duniani leo Machi 22, 2026, wadau wa maendeleo na mazingira wameainisha sababu kadhaa zinazoendelea kuchangia uhaba wa maji nchini, huku upotevu wake ukitajwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa.

Mbali na upotevu huo, wadau wameeleza kuwa usambazaji duni wa maji, ukosefu wa miundombinu imara, mabadiliko ya tabianchi na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali hiyo, vinaongeza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya utendaji wa mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira kwa mwaka wa fedha 2024/25 iliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), kiwango cha upotevu wa maji kimeongezeka kutoka asilimia 36.8 mwaka wa fedha 2023/24 hadi asilimia 42.3 mwaka wa fedha 2024/25.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi bado ni mdogo, ukiwa kwa wastani wa saa 14 pekee kati ya 24.

Akizungumzia changamoto hiyo wakati wa uzinduzi wa taarifa hiyo Machi 19, 2026 mkoani Morogoro, Waziri wa Maji, Juma Aweso alisema Serikali imeanza kuchukua hatua za kudhibiti upotevu huo kwa kuweka mfumo wa kupima ufanisi wa wakurugenzi wa mamlaka za maji, kulingana na uwezo wao wa kupunguza upotevu.

Alisema baadhi ya watendaji ndani ya mamlaka za maji wanahusika na vitendo vya kuunganisha wateja nje ya mifumo rasmi, hali inayochangia upotevu unaoonekana kwenye takwimu.

Alitolea mfano baadhi ya taasisi –hoteli na viwanda, zinavyounganishwa kinyemela na huduma za maji, huku fedha zinazokusanywa zikichukuliwa na watendaji hao huku matumizi hayo yakionyeshwa kama kwenye ripoti rasmi maji yaliyopotea.

Licha ya masuala hayo, wataalamu wanasema Siku ya Maji Duniani huadhimishwa kila mwaka Machi 22 kwa lengo la kuhamasisha umuhimu wa maji safi na usimamizi endelevu wa rasilimali hiyo.

Siku hiyo ilianzishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1992 wakati wa mkutano wa kimataifa wa mazingira uliofanyika Rio de Janeiro, Brazil, maarufu kama Earth Summit. Maadhimisho ya kwanza ya siku hiyo yalianza mwaka 1993.

Kutokana na uhamasishaji huo, kwa Tanzania hali ya upatikanaji wa maji ikoje?

Jamila Hussein (35), mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam, ni miongoni mwa wananchi wanaokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama licha ya kuishi katika jiji kubwa.

Anasema hajawahi kuona maji yakitoka kwenye bomba la nyumbani kwake, hivyo hulazimika kutumia maji ya kisima na kununua ndoo ya lita 20 kwa Sh500.

“Bila kufanya hivyo siwezi kupata maji. Natumia fedha nyingi na wakati mwingine maji si salama. Ahadi zimekuwa nyingi lakini sioni mabadiliko,” anasema.

Changamoto hiyo haipo mijini pekee. Vijijini, hali ni mbaya zaidi, baadhi ya wananchi hupoteza maisha wakisaka maji. Mfano ni Corester Haule (25), mkazi wa Kijiji cha Kipingu mkoani Njombe, aliyefariki dunia mwaka 2025 baada ya kushambuliwa na mamba katika Mto Ruhuhu alipokuwa akichota maji.

Pamoja na changamoto nyingi, lakini takwimu zinaonyesha yapo mafanikio kwa kiasi fulani. Kwa mujibu wa Sera ya Maji Toleo la 2025, upatikanaji wa maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 50 mwaka 2002 hadi asilimia 83 mwaka 2024, huku mijini ukiongezeka kutoka asilimia 73 hadi asilimia 91.6 katika kipindi hicho.

Waziri wa Maji, Aweso anasema kati ya vijiji 12,333 nchini, vijiji 10,758 vimeunganishwa na huduma ya maji na vingine 1,575 vikiwa bado havijafikiwa.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, matarajio ya baadaye yanaibua wasiwasi.

Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 inaonya kuwa Tanzania inaweza kukumbwa na uhaba mkubwa wa maji kutokana na ongezeko la watu, shughuli za kiuchumi na mabadiliko ya tabianchi.

Serikali inalenga kufikia usalama wa maji kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ifikapo mwaka huo wa 205.

Akizungumzia hali hiyo, mchambuzi wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude anasema pamoja na Tanzania kuwa na vyanzo vingi vya maji, bado usambazaji wake haukidhi mahitaji, hata katika miji mikubwa kama Dar es Salaam.

Amesema ukuaji wa haraka wa miji, miundombinu duni na athari za mabadiliko ya tabianchi vinachangia upungufu huo. Pia amebainisha kuwa uchafuzi wa vyanzo vya maji na matumizi yasiyo endelevu vinaongeza tatizo.

“Ni lazima kuwe na matumizi endelevu ya maji nyumbani, viwandani na katika kilimo. Bila maji hakuna maisha wala uzalishaji,” amesema.

Mkude amependekeza kupunguza upotevu wa maji, kudhibiti wizi, kuboresha miundombinu na kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo ukaguzi wa matumizi ya maji katika viwanda. Aidha, ameshauri matumizi ya kilimo cha umwagiliaji wa matone ili kuokoa maji.

Kwa upande wake, mtaalamu wa mazingira, Aidan Msafiri anasema maji ni rasilimali adimu inayopungua kadri muda unavyokwenda, akionya kuwa ongezeko la joto duniani linaathiri upatikanaji wake.

Amesema kuna uzembe katika usimamizi wa miundombinu ya maji, hali inayosababisha upotevu mkubwa, huku uchimbaji holela wa visima na ukosefu wa upandaji miti ukihatarisha uendelevu wa rasilimali hiyo.

“Upotevu wa maji hata kwa asilimia 30 ni hasara kubwa. Pia kuna matumizi mabaya ya maji hata kwa watu walioelimika,” amesema.

Naye mchambuzi wa masuala ya kijamii, Magabilo Masambu amesisitiza umuhimu wa kuhimiza matumizi ya teknolojia nafuu za uvunaji wa maji ya mvua, hasa vijijini ambako huduma bado ni haba.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002, Toleo la 2025, inapendekeza uendelezaji wa miundombinu ya kuhifadhi maji inayostahimili mabadiliko ya tabianchi ili kupunguza athari za ukame na mafuriko.