Simba yapanda nafasi ya pili ikiichapa TRA United

Klabu ya Simba imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo timu hiyo sasa imesogea hadi nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikifikisha pointi 31 ikiishusha Azam FC ambayo ina pointi 29 katika nafasi ya tatu.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Dimba la Major General Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam imeshuhudiwa Wekundu wa Msimbazi wakipata bao dakika ya 24 kupitia kwa mshambuliaji, Seleman Mwalimu ambaye amefunga kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa kushoto Nickson Kibabage kuchezewa faulo ndani ya eneo la hatari.

Mwalimu amefunga bao hilo baada ya kukosekana katika mechi tatu kutokana na adhabu ya kinidhamu iliyokuwa inamkabili ambapo alikosa michezo dhidi ya B19 FC, Singida Black Stars pamoja na Pamba Jiji.

Bao alilofunga limemfanya afikishe idadi ya mabao matano aliyopachika msimu huu katika Ligi Kuu.

Katika kipindi cha pili, Neo Maema aliongeza bao la pili kwa Wekundu hao katika dakika ya 67 akifunga kwa kupiga mpira wa adhabu uliovuka ukuta wa TRA na kuzama wavuni moja kwa moja.

Dakika moja kabla ya kukamilika 90 kiungo, Yusuph Kagoma alifunga karamu ya mabao kwa kuandika bao la tatu baada ya kumalizia kwa kichwa krosi iliyopigwa na Anicet Oura.

Simba sasa imesalia na mechi mbili kufikisha idadi sawa na watani zao wa jadi Yanga ambao wanaongoza ligi kwa pointi 38 huku wakiwa tayari wamecheza michezo 16 ya Ligi Kuu.