Na Mwandishi Wetu
Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
Tanzania (TPA) inaendelea kufungua fursa za uwekezaji katika sekta ya meli ili kuimarisha usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi.
Katika juhudi hizo, TPA ilipokea maombi kutoka kampuni ya Gold Voyage Logistics Limited, tanzu ya Zijin Mining Group Co. Ltd, ya kukodisha eneo katika Bandari ya Karema kwa ajili ya ujenzi wa meli nne kubwa za mizigo. Mradi huu unalenga kuongeza kipato cha wananchi wa mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma inayopitiwa na Ziwa Tanganyika pamoja na kukuza uchumi wa taifa.
Ujenzi wa meli hizo ulianza Aprili 2025 na unatarajiwa kukamilika Julai 2026. Hadi sasa, mradi umefikia zaidi ya asilimia 95, huku meli zote tayari zikiwa majini zikisubiri hatua za mwisho za uhakiki kabla ya kuanza kutoa huduma.
Akizungumza jijini Mwanza, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema meli hizo zitakapoanza kazi zitaimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Zambia. Pia zitachochea usafirishaji wa mizigo kupitia maeneo ya Manono, Bandari ya Kalemie, Kigoma, Dar es Salaam na Tanga.
Zaidi ya hayo, mradi huu utawanufaisha wakulima kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao yao, pamoja na kuleta ajira kwa Watanzania hususan mabaharia, ambapo kila meli itahitaji angalau wafanyakazi 15. Shughuli za upakiaji, upakuaji, huduma bandarini na biashara ndogondogo pia zinatarajiwa kuongezeka kwa kasi.
Msigwa ameongeza kuwa meli hizi zitafungua fursa zaidi za kiuchumi kwa kuimarisha usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya SGR, huku wamiliki wa malori wakinufaika kutokana na uwezo mkubwa wa kila meli kubeba tani kati ya 8,000 hadi 10,000 kwa safari moja.
.jpeg)
