Trump alaumiwa kwa kufurahia kifo cha bosi wa zamani wa FBI

Dar es Salaam. Rais wa Marekani, Donald Trump, amekumbana na wimbi la lawama baada ya kutoa kauli iliyotafsiriwa kuwa ya kikatili kutokana na kifo cha Robert Mueller, aliyekuwa mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).

Mueller, mkongwe wa vita vya Vietnam na mwanasheria aliyewahi kuongoza uchunguzi nyeti kuhusu madai ya Russia kuingilia uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2016, alifariki dunia Ijumaa akiwa na umri wa miaka 81.

Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump alinukuliwa akisema: “Robert Mueller amekufa. Vizuri, ninafurahi amekufa. Hawezi tena kuwaumiza watu wasio na hatia!” Kauli hiyo ilizua hasira kali kutoka kwa wanasiasa wa vyama vyote na wachambuzi wa masuala ya siasa.

Kwa mujibu wa The Guardian, miongoni mwa waliomkosoa ni Michael Steele, ambaye amemuita Trump “mtu wa kuchukiza,” huku Rick Wilson akimtaja Mueller kama “shujaa” na kumshambulia Trump kwa maneno makali.

Kwa upande wa Chama cha Democratic, sauti za ukosoaji pia zilikuwa kali. Seneta wa California, Adam Schiff, amesema kauli hiyo inaonesha “ukosefu wa maadili na kutofaa kwa uongozi,” wakati mbunge Dan Goldman akisema Trump anaadhimisha kifo cha mtu aliyefichua juhudi za kuathiri uchaguzi.

Wachambuzi wengine wameeleza mshangao wao kwa kulinganisha historia ya wawili hao, Mueller akiwa mwanajeshi aliyepigana Vietnam na kujeruhiwa, huku Trump akitajwa kupata msamaha mara kadhaa ili kuepuka kwenda vitani.

Kiongozi wa wachache katika Bunge la Seneti, Chuck Schumer, ameeleza kuwa kauli za aina hiyo ni sehemu ya mkakati wa kisiasa, akisema: “Ukali ndiyo lengo, ni njia ya kuwatoa watu kwenye masuala muhimu.”

Kauli ya Trump inaongeza orodha ya matukio aliyowahi kukosolewa kwa kutoa matamshi yanayoonekana kuwashambulia hata watu waliofariki, jambo linalozidi kuchochea mjadala kuhusu maadili ya uongozi nchini Marekani.

Hata hivyo, bado haijawekwa wazi sababu ya kifo cha bosi huyo wa zamani aliyehudumu kuiongoza FBI kuanzia mwaka 2001 hadi 2013, akiwa ameteuliwa siku chache kabla ya shambulizi la Septemba 11, 2001.

Katika uongozi wake, Mueller alifanya kazi na Rais George W. Bush na Barack Obama.