Ugumu Simba v TRA United uko hapa!

KUNA dakika 90 muhimu leo zitapigwa pale Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni Jijini Dar es Salaam, Simba itakaporejea nyumbani kupambana na TRA United, kwenye mchezo ambao utakuwa wa ushindani mkubwa kila timu ikiwa inahitaji pointi tatu za jasho.

Huu utakuwa mchezo wa mwisho kwa timu hizo kabla ligi kuu haijasimama kwa wiki mbili kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambapo Taifa Stars itaondoka na kwenda Rwanda kwa ajili ya mashindano ya FIFA Series.

Simba itaingia kwenye mchezo huo ikitoka kwenye ziara ya mechi za ugenini, huku mchezo mmoja ukishindwa kuchezwa dhidi ya TRA United haohao uliokuwa upigwe pale Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha, kutokana na uwanja huo kujaa maji kufuatia mvua kubwa zilizonyesha Machi 14, 2026.

Baada ya mchezo huo, Simba ikaifuata Pamba Jiji Machi 19, 2026 mchezo uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ikakutana na sare ya kushtua, timu hizo zikimaliza dakika 90 kwa sare ya 1-1.

Simba itakuwa inaanza mechi zake za mzunguko wa pili ikitambua kwamba mchezo pekee ambao imefanya vibaya nyumbani ni pale ilipokubali kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Azam iliyokuwa Desemba 7, 2025. Hakuna mchezo mwingine ambao wekundu hao wameangusha pointi wakiwa kwao.

Habari njema kwa Simba ni kurejea kwa mshambuliaji wake na kinara wa ufungaji kwa sasa kwenye timu hiyo, Seleman Mwalimu, mwenye mabao manne, akitoka kutumikia adhabu ya kusimamishwa mechi tatu kufuatia kumpiga kiwiko beki wa Dodoma Jiji, Andy Bikoko, kwenye mechi kati ya timu hizo.

Kurejea kwa Mwalimu kutairudisha Simba kucheza na mshambuliaji halisi, ambapo tangu kusimamishwa kwake, kocha wa timu hiyo, Steve Barker, amekuwa akilazimika kumtumia mmoja kati ya viungo wake washambuliaji kucheza kama mshambuliaji halisi hjuku mchezo mmoja akianza Baraka Mwangosi.

Mbali na Mwalimu, nyota hatari wengine kwenye mchezo huo ni viungo Anicet Oura, Lebase Gueye, Clatous Chama na Elie Mpanzu ambao wakati wowote wanaweza kutengeneza shida kwenye lango la upinzani.

Takwimu zinaonyesha kwenye mechi tano zilizopita, Simba imeshinda mbili dhidi ya Tanzania Prisons (2-0) na Singida Black Stars (2-1), kisha imetoa sare tatu dhidi ya Dodoma Jiji (0-0), Yanga (0-0) na Pamba (1-1).

Kocha wa Simba Steve Barker akizungumzia mchezo huo alisema wanarudi nyumbani kutafuta ushindi, wakitaka kurekebisha matumizi ya nafasi wanazozitengeneza ili kujihakikishia ushindi.

“Tunakwenda kucheza dhidi ya TRA United, haitakuwa mechi rahisi ukiona wametoka kupata sare dhidi ya Yanga, ni timu ambayo inacheza kwa nidhamu kubwa, tunataka kurudi kwenye njia ya ushindi baada ya sare tuliyoipata kwenye mchezo wa mwisho,” alisema Barker.

TRA United imebadilishwa sana ikiwa chini ya kocha mzoefu, raia wa Burundi, Ettiene Ndayiragije, ambapo imeunda kikosi cha ushindani msimu huu.

Huu unakuwa mchezo wa kwanza baina ya timu hizo tangu ibadilishwe kutoka Tabora United na kuwa TRA United, ambapo kabla Simba ilikuwa inajipigia inavyotaka timu hiyo ambapo kwenye michezo miwili ya msimu uliopita ilishinda yote. Kwenye mechi zake tano zilizopita, TRA imepoteza mechi mbili, kisha ikashinda mbili na kutoa sare moja dhidi ya Yanga, ikionyesha kiwango kizuri kwenye mchezo wake huo wa mwisho kabla ya kwenda kukutana na Simba.

Simba inatakiwa kumchunga zaidi Ramadhani Chebwedo ambaye alionyesha kiwango cha juu kwenye mchezo dhidi ya Yanga na mwisho akaibuka mchezaji bora wa mchezo huo, pia wanatakiwa kuwa makini na mshambuliaji Mganda, Joseph Akandwanaho, anayeongoza kuwafungia mabao TRA United, lakini akiwa ni mmoja kati ya washambuliaji wasumbufu.