Utalii wa kupanda Mlima Kilimanjaro kwa muda mfupi wavutia watalii

Moshi. Utalii wa kupanda Mlima Kilimanjaro kwa muda mfupi maarufu kwa jina la Ultra marathon, unatajwa kuzidi kukua na kuvutia idadi kubwa ya watalii kutoka nje na ndani ya nchi.

Makundi mbalimbali yamekuwa yakitumia aina hiyo ya utalii kupanda mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika ambao una urefu wa mita 5,895.

Akizungumza Jumamosi Machi 21, 2026 wakati wa kupokea watalii 21 kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Marekani na Nepal, waliokamilisha safari yao ya kupanda mlima huo kwa saa 24, Ofisa Uhifadhi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro (Kinapa), Vitus Mgaya amesema utalii huo unazidi kukua.

Amesema watalii hao walitumia saa 24 kupanda na kushuka Mlima Kilimanjaro kupitia lango la Marangu.

Ofisa Uhifadhi Mwandamizi kutoka Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), Vitus Mgaya, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea wageni 21 waliopanda Mlima huo kwa muda mfupi,saa 24.

“Kwa sasa hifadhi imekuwa ikipokea wageni wengi sana wanaotaka kufanya challenge za kupanda mlima mpaka kileleni kwa saa chache. Yuko yule mmoja ambaye anashikilia rekodi kwa kupanda kwa muda mfupi wa saa sita na dakika 45 lakini wako wengine waliotumia saa nane, 10 na zaidi.

“Tumekuwa tukipokea wageni wengi wanaotaka kupanda mlima kwa muda mfupi. Wapo waliowahi kufanya kwa saa sita na dakika 45, wengine saa nane, 10 na zaidi. Huu ni utalii unaokua kwa kasi na umekuwa kivutio kikubwa,” amesema Mgaya.

Ameongeza kuwa aina hiyo ya utalii pia ina faida kiafya na kusaidia kubadili mtazamo wa watu kuhusu mlima huo.

“Tunauhimiza utalii huu kwa sababu unasaidia kujenga afya na kuwafanya watu waone kuwa Kilimanjaro siyo ngumu kama wanavyodhani,” ameeleza.

Mgaya amesema watalii hao walitumia njia ya Marangu yenye umbali wa kilomita 34 kutoka lango la hifadhi hadi kileleni na kurejea ndani ya saa 24, huku akibainisha kuwa hata Watanzania wameanza kujitokeza pia.

Kwa upande wake, mwongoza watalii katika mlima huo, Mathayo Sanka amesema maandalizi ya safari hiyo yalihusisha awamu mbili, ambapo ya kwanza ilikuwa ni kupanda kwa siku nane kupitia njia ya Lemosho kabla ya kuanza safari hiyo ya saa 24.

“Awali, tulipanda kwa siku nane kupitia njia ya Lemosho, lakini baada ya kumaliza wakaamua kufanya awamu ya pili ya saa 24. Lengo lilikuwa kupanda na kushuka ndani ya muda huo, na tumefanikiwa kurudi salama bila madhara,” amesema.

Baadhi ya watalii na waongoza watalii, wakishuka kutoka Mlima Kilimanjaro, baada ya kupanda kwenye Mlima kwa muda mfupi “ultra marathon” ndani ya muda wa saa 24, kwa kupitia lango la Marangu.

Kiongozi wa msafara huo kutoka Uingereza, Dave Pickles amesema wamefanikiwa kukamilisha baada ya maandalizi ya muda mrefu.

Amesema mafanikio ya safari hiyo yamechangiwa na ushirikiano mkubwa kati ya wageni na waongozaji na kuwa wageni hao walifanya maandalizi makwao kabla ya kuja kupanda mlima huo.

Mmoja wa washiriki, Rory Birse kutoka Marekani, amesema safari hiyo ilikuwa ngumu lakini yenye mafanikio makubwa kwake binafsi.

“Nilikuja hapa kujipa changamoto japo ilikuwa ngumu sana, lakini pia ni uzoefu wa kipekee na nimefurahi kuweza kukamilisha ndani ya saa 22, najivunia mimi na timu yangu,”amesema.

Ameongeza kuwa maandalizi ya safari ya kawaida ya siku nane yaliwasaidia kuimarisha mshikamano wa timu na kujiandaa kwa challenge hiyo ya kupanda kwa saa 24.

Naye, Dk Jeff Chamberlain kutoka Marekani amesema pamoja na ugumu wa safari hiyo, uzoefu alioupata ulikuwa wa kipekee, hasa katika kujifunza maisha ya watu wa eneo hilo.

Amesisitiza kuwa, maandalizi ni jambo muhimu kwa yeyote anayetaka kushiriki upandaji wa mlima wa namna hiyo.

“Si salama kwa mtu ambaye hajajiandaa, lakini kwa aliyejiandaa inawezekana. Kuusukuma mwili ni muhimu, mimi nilitumia miaka kadhaa kujiandaa kiafya na miezi sita ya mwisho kujiandaa kwa ajili ya hili,” amesema.