Vitisho vya Trump kwa Iran kuongeza makali ya vita Mashariki ya Kati

Tel Aviv. Rais wa Marekani, Donald Trump na Serikali ya Iran wametishia kuongeza makali ya vita yao kwa kulenga miundombinu ya nishati na mafuta katika Ukanda wa Ghuba, hatua inayoweza kuyumbisha tena masoko ya kimataifa ya nishati na fedha, hivyo kuzidisha mgogoro wa kikanda.

Jana, Jumamosi Machi 21, 2026, Trump alitishia kuangamiza kabisa mitambo ya kuzalisha umeme ya Iran iwapo Serikali ya nchi hiyo haitafungua kikamilifu Mlango Bahari wa Hormuz ndani ya saa 48, ikiwa ni ongezeko kubwa la mvutano siku moja tu baada ya kuzungumzia uwezekano wa kupunguza kasi ya vita hiyo ambayo sasa imeingia wiki ya nne.

Leo, Jumapili, Iran nayo imeonya kwamba italenga miundombinu ya Marekani, ikiwamo vituo vya nishati katika ghuba, iwapo Trump atatekeleza tishio lake alilolitoa wakati wanamaji wa Marekani na vyombo vizito vya kutua vikielekea katika eneo hilo.

Zaidi ya watu 2,000 wameuawa tangu vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran Februari 28, hali iliyoyumbisha masoko, kupandisha gharama za mafuta, kuchochea hofu ya mfumuko wa bei duniani na kuitikisa miungano ya Magharibi iliyoundwa baada ya vita.

Kwa mujibu wa Reuters, mchambuzi wa masoko ya hisa, Tony Sycamore amenukuliwa akisema, tishio la Trump limeweka hali ya sintofahamu ya saa 48 inayoweza kulipuka wakati wowote katika masoko.

“Iwapo kauli hiyo haitaondolewa, kuna uwezekano mkubwa wa kushuhudia Jumatatu Nyeusi ambapo masoko ya hisa duniani yataanguka kwa kasi huku bei za mafuta zikiongezeka kwa kiwango kikubwa,” amesema Sycamore.

Ameongeza kuwa, Tehran huenda ikalenga miundombinu ya nishati katika Saudi Arabia, United Arab Emirates na Qatar, jambo ambalo litakaloongeza na kurefusha maumivu ya kupanda kwa bei za nishati na kuupanua mgogoro kuwa wa kikanda.

Bei za mafuta zilipanda Ijumaa na kufikia kiwango cha juu zaidi katika karibu miaka minne baada ya Iraq kutangaza hali ya dharura (force majeure) katika visima vyake vyote vinavyoendeshwa na kampuni za kigeni, Israel kushambulia eneo kubwa la gesi nchini Iran na Iran kujibu kwa mashambulizi dhidi ya majirani zake, wakiwamo Saudi Arabia, Qatar na Kuwait.

Mashambulizi ya Iran yamesababisha kufungwa kwa kiasi kikubwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz, njia nyembamba inayobeba takriban theluthi moja ya tano ya mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa duniani na kusababisha hali mbaya zaidi ya mafuta tangu miaka ya 1970. Karibu kufungwa kwake kulisababisha bei za gesi barani Ulaya kupanda hadi asilimia 35 wiki iliyopita.

Kupitia mitandao ya kijamii, Trump alisema: “Iwapo Iran haitafungua kikamilifu, bila tishio, Mlango Bahari wa Hormuz ndani ya saa 48 kuanzia sasa, Marekani itashambulia na kuangamiza mitambo yao ya umeme, kuanzia na mkubwa zaidi!”

Saa chache baadaye, mwakilishi wa Iran katika wakala wa usafiri wa majini wa Umoja wa Mataifa, Ali Mousavi alisema mlango huo bado uko wazi kwa meli zote isipokuwa zile zinazohusishwa na maadui wa Iran.

Mousavi alisema usafiri katika njia hiyo unawezekana kwa kuratibu masuala ya usalama na Iran.

Taarifa za ufuatiliaji wa meli zinaonesha baadhi ya vyombo, ikiwamo meli zenye bendera ya India na Pakistan, zimefanikiwa kupita salama. Pakistan ina uhusiano mzuri na Iran huku pia ikidumisha uhusiano wa karibu na Marekani na Saudi Arabia.

Sycamore alisema mkakati wa Trump wa kulenga miundombinu ya Iran ni kufanya zuio la Hormuz kuwa lisilovumilika kiuchumi na kisiasa kwa Tehran, bila kuharibu visima vya mafuta vya Iran ambavyo vingesababisha uharibifu wa muda mrefu katika usambazaji wa kimataifa.

Makao makuu ya kijeshi ya Iran ya Khatam al-Anbiya yalisema iwapo Marekani itashambulia miundombinu ya mafuta na nishati ya Iran, basi Iran italenga miundombinu yote ya Marekani ya nishati, teknolojia ya habari na mitambo ya kuchuja maji katika eneo hilo.

Mtandao wa umeme wa Iran umeunganishwa kwa karibu na sekta yake ya nishati, hivyo mashambulizi dhidi ya mitambo mikubwa yanaweza kusababisha kukatika kwa umeme na kuathiri kila kitu kuanzia pampu, mitambo ya kusafisha mafuta hadi vituo vya kusafirisha nje na vituo vya kijeshi.

Mitambo mikubwa ya umeme ya Iran ni pamoja na Damavand karibu na Tehran, Kerman kusini mashariki na Ramin katika jimbo la Khuzestan, ambayo ina uwezo mkubwa zaidi wa uzalishaji kuliko kinu chake pekee cha nyuklia cha Bushehr.