Rungwe. Wimbi la wizi wa parachichi shambani limeibua taharuki kwa wakulima wa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, huku baadhi yao wakitishia kukata miti ya zao hilo na kuachana na kilimo hicho endapo Serikali haitachukua hatua za haraka kudhibiti hali hiyo.
Wakulima hao wamesema wamechoshwa na ongezeko la wizi pamoja na kile wanachodai kuwa utoaji holela wa vibali vya uchumaji na ununuzi wa parachichi, hali inayowalazimu kukesha shambani kulinda matunda yao kwa kutumia silaha za jadi kama mapanga na mawe.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Machi 22, 2026, mkulima wa Kijiji cha Mpandapanda, Kata ya Kiwira, Frank Mwankenja amesema wakulima wamekuwa katika sintofahamu kutokana na hali hiyo huku wakihofia kupoteza kabisa matumaini ya kunufaika na zao hilo.
Amesema baada ya kuibuka kwa matukio ya wizi, walilalamikia uongozi wa wilaya na kuahidiwa kuchukuliwa hatua, ikiwamo kusitishwa kwa utoaji wa vibali vya uchumaji.
Mkulima wa zao la Parachichi Ipyana Mwalukasa akionyesha sehemu ya matunda yanayo chumwa na kuuzwa kwa wanunuzi. Picha na Hawa Mathias
“Serikali ilisema itasitisha utoaji wa vibali ili kudhibiti wizi, lakini bado tunaona hali haijabadilika. Sisi wakulima tunafanya kazi ngumu kuzalisha, lakini sasa tumelazimika kukesha shambani kulinda mazao yetu dhidi ya wahalifu,” amesema Mwankenja.
Amesema endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa, hali inaweza kusababisha migogoro na hata kuhatarisha usalama wa wakulima.
Mkulima wa Kijiji cha Kyomo, Kayusi Msigwa amesema mwaka huu umekuwa tofauti na miaka mingine kutokana na changamoto hizo ambazo zimeathiri hata hali ya kiuchumi kwa wakulima.
“Huu utoaji wa vibali kiholela umetukatisha tamaa sana. Wakulima wengine wanafikiria kukata miti ya parachichi na kugeukia shughuli nyingine za kiuchumi,” amesema.
Msigwa amesema badala ya kujikita katika uzalishaji, wakulima wengi wamejikuta wakikesha shambani wakilinda matunda yao, jambo ambalo linaathiri shughuli nyingine za uzalishaji.
Muonekano wa matunda ya parachichi yakiwa yamehifadhiwa kwenye vifungashio kwa ajili ya kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali nchini. Picha na Hawa Mathias.
“Sisi tunaiomba Serikali iingilie kati haraka, kwa sababu kilimo hiki ndicho chanzo kikuu cha kipato kwa familia nyingi hapa Rungwe,” amesema.
Mkulima wa Kata ya Nkuga, Maria Mzungu amesema hali imekuwa ngumu kwa wakulima kutokana na wizi pamoja na changamoto za bei katika mizani.
“Tunaibiwa mashambani, halafu tukipeleka mazao sokoni tunapigwa kwenye mizani. Tunaomba Serikali ituangalie kwa jicho lingine ili kunusuru maisha yetu,” amesema.
Mkulima mwingine, Ipyana Mwalukasa amesema utoaji wa vibali vya ununuzi wa parachichi daraja la pili umechangia kuongeza wizi mashambani.
“Matunda mengi bado hayajakomaa, lakini watu wanaingia mashambani kuyaiba na kuyauza. Hili limekuwa tatizo kubwa kwa wakulima,” amesema.
Mbali na wakulima, wanunuzi wa zao hilo pia wameeleza wasiwasi wao kufuatia agizo la Serikali kusitisha ununuzi wa parachichi tangu Machi 17 mwaka huu.
Mnunuzi wa parachichi kutoka Kata ya Kyimo, Josia Katende amesema hatua hiyo imeathiri biashara yao kwa kuwa bado kuna matunda mengi shambani huku baadhi ya mizigo ikiwa imekwama kutokana na zuio hilo.
“Tunaomba Serikali itukutanishe wadau wote ili kujadili changamoto hizi. Kuweka zuio pekee haitoi suluhisho, hasa kwa wafanyabiashara ambao tayari wamewekeza fedha nyingi,” amesema.
Ameongeza kuwa changamoto nyingine ni ushuru mkubwa wa Sh1,600 kwa kila gunia la parachichi, jambo ambalo linaongeza gharama za biashara hiyo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kwanza Fresh ya Wilaya ya Rungwe, Onesmo Mwasongwe amesema kusimamishwa kwa msimu wa ununuzi kunaweza kuathiri vibaya biashara ya parachichi, hasa kwenye masoko ya nje ya nchi.
Amesema tayari amewekeza mtaji wa Sh11 bilioni katika biashara hiyo na kati ya fedha hizo, Sh9 bilioni tayari zimetumika kununua matunda kutoka kwa wakulima.
Baadhi ya wakulima wanaolalamikia kuibuka kwa wimbi la wizi wa zao hilo jambo ambalo wametishia kukata miti .Picha na Hawa Mathias
“Suluhisho la tatizo hili si kusimamisha msimu wa ununuzi. Hatua hiyo inaweza kuathiri hata masoko ya nje ambayo tayari tumeyafungua,” amesema.
Akizungumzia malalamiko hayo, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Rungwe, Salum Adam amesema halmashauri imekuwa ikitoa vibali vya uchumaji wa parachichi tangu Novemba mwaka jana katika kanda tatu zenye hali tofauti za hewa.
Amesema kutokana na tofauti hizo za hali ya hewa, matunda hukomaa kwa nyakati tofauti, hivyo vibali hutolewa kwa wanunuzi kwa kuzingatia madaraja ya kwanza na pili.
“Zipo kanda tatu zenye hali ya hewa tofauti, hivyo matunda hukomaa kwa nyakati tofauti. Ndiyo maana tumekuwa tukitoa vibali kwa wanunuzi kwa madaraja hayo,” amesema.
Kuhusu malalamiko ya wakulima, Adam amesema baadhi yao bado hawajakubaliana na mfumo mpya wa biashara ya parachichi ambao, kwa mujibu wake, umechangia kuimarisha bei ya zao hilo sokoni.
Amesema suala la wizi mashambani linahitaji pia ushiriki wa wakulima wenyewe kwa kuweka mifumo ya ulinzi katika mashamba yao.
“Ulinzi wa mashamba ni jukumu la wakulima wenyewe pia, siyo Serikali pekee,” amesema.
Hata hivyo, amesema baada ya maelekezo ya Mkuu wa Wilaya, halmashauri ilitoa tangazo la kuwataka wafanyabiashara kuondoa mizigo ya parachichi iliyokwisha nunuliwa kati ya Machi 17 na 19 mwaka huu, ingawa baadhi yao wameeleza kukumbwa na changamoto za usafirishaji.
