Arsenal Yakosa Tena Ubingwa, Guardiola Aandika Historia Atwaa Carabao

Global Publishers
March 23, 2026
0 Comments

Manchester City wameendelea kuthibitisha ubora wao katika soka la England baada ya kutwaa ubingwa wa Carabao Cup kwa mara ya tisa kihistoria, kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Arsenal katika dimba la Wembley Stadium.

Ubingwa huo unaifanya City kuongeza rekodi yao ya mafanikio katika michuano hiyo, wakiongeza taji la mwaka 2026 kwenye orodha yao ndefu ya ushindi walioupata miaka ya 1970, 1976, 2014, 2016, 2018, 2019, 2020 na 2021.

Nyota wa mchezo huo alikuwa Nico O’Reilly aliyefunga mabao mawili ya vichwa ndani ya dakika chache kipindi cha pili, mabao yaliyohitimisha kabisa ndoto za Arsenal kurejea kwenye mchezo.

Bao la kwanza lilitokana na kosa kubwa la mlinda mlango Kepa Arrizabalaga aliyeshindwa kuudhibiti mpira wa krosi uliopigwa na Rayan Cherki, na kumruhusu O’Reilly kufunga kwa urahisi.

Dakika chache baadaye, O’Reilly alifunga tena kwa kichwa na kuifanya City kuwa mbele kwa mabao mawili  hali iliyozima kabisa ushindani.

Kocha Pep Guardiola alipata taji lake la tano la Carabao Cup na kufikisha jumla ya mataji 32 makubwa katika taaluma yake ya ukocha, huku nusu yake akiwa ameyapata akiwa na Manchester City.

Ushindi huo pia ulikuwa ujumbe mzito kwa Mikel Arteta kuwa bado ana kazi kubwa ya kufanya ili kufikia mafanikio ya kiwango cha juu mbele ya mashabiki.

Licha ya kuanza mchezo kwa kasi, Arsenal walishindwa kutumia nafasi walizopata mapema. Kipa James Trafford aliokoa hatari tatu za haraka, akiwazuia Kai Havertz na Bukayo Saka kufungua ukurasa wa mabao.

Kwa upande wa City, Erling Haaland aliendelea kuwa na bahati mbaya katika dimba la Wembley, akishindwa kufunga kwa mechi ya saba mfululizo licha ya kupata nafasi kadhaa.