Dosari za kisheria zamnusuru kifungo cha miaka 30 jela

Arusha. Mahakama ya Rufani imebatilisha hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela alichokuwa amehukumiwa Lemindea Lesira baada ya kukutwa na kosa la ubakaji.

Makosa mengine aliyokutwa nayo na hatia na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka mitano na faini kwa mwathirika wa tukio hilo ni kusababisha madhara makubwa kinyume na kifungu cha 225 na kosa la ukatili kwa watoto kinyume na kifungu cha 169A (1) na (2) cha Kanjni ya Adhabu.

Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kubaini dosari za kisheria katika upokeaji wa ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo kuwa, haukuzingatia matakwa ya sheria, hakula kiapo wala kuthibitisha kabla ya kuanza kutoa ushahidi wake.

Uamuzi uliobatilisha adhabu hiyo umetolewa Machi 20, 2026 na jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo ambao ni Winfrida Korosso, Lilian Mashaka na Paul Ngwembe, waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo ya jinai namba 601/2023.

Mahakama imesema kulikuwa na upungufu mkubwa katika mwenendo wa kesi hiyo, hususan namna ushahidi wa mwathiriwa ulivyopokelewa mahakamani.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Mahakama ilibaini kuwa ushahidi wa mwathiriwa, ambaye alikuwa na umri wa miaka 16 wakati wa kutoa ushahidi, haukuzingatia matakwa ya kisheria kwani hakula kiapo wala kuthibitisha kabla ya kuanza kutoa ushahidi wake.

Badala yake, mwathiriwa alitoa ahadi ya kusema ukweli, utaratibu ambao kisheria unaruhusiwa tu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 14. Kutokana na kasoro hiyo, Mahakama iliamua kuondoa ushahidi wake wote kwenye rekodi ya kesi.

“Baada ya kuondolewa kwa ushahidi huo muhimu, hakuna ushahidi uliobaki unaoweza kuthibitisha kosa la ubakaji bila shaka yoyote,” inaeleza sehemu ya hukumu hiyo.

Lemindea na Kulasa Mandeu (siyo mrufani), walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakikabiliwa na makosa matatu ambayo ni madhara makubwa kinyume na kifungu cha 225 na ukatili kwa mtoto kinyume na kifungu cha 169A (1) (2) cha Kanuni ya Adhabu.

Pia, mrufani alishtakiwa kwa kosa la ubakaji kinyume na kifungu cha 130(1) (2) (e) na 131 cha Kanuni ya Adhabu, alidaiwa kumuoa kwa ndoa ya kitamaduni msichana aliyekuwa na umri wa miaka 14 mwaka 2020.

Mwathiriwa wa tukio hilo alidai siku ya tukio Septemba 14, 2022 akiwa amebeba chupa yenye dawa ya kuua wadudu,   mumewe (mrufani) alikasirika akamshambulia.

Alidai kukimbia na kwenda kwa shemeji yake (Kulasa Mandeu) ili amsaidie ila badala yake Kulasa aliungana na mrufani na kumfunga kwenye mti na kuanza kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na baada ya kumshambulia kwa muda walimfunga mikono na miguu na kumtelekeza msituni.

Kumbukumbu za rufaa hiyo zinaonesha siku nne,kuanzia Septemba 14 hadi 18,2022 mwathirika wa tukio hilo alibaki katika hali ya udhaifu, alipoteza fahamu kutokana na majeraha hayo.

Alidai kila alipokuwa akipata fahamu alijaribu kusogea kutoka msituni ili apate msaada.

Septemba 18, 2022 shahidi wa pili alikutana naye alipokuwa akichunga mifugo, alimpeleka nyumbani kwake na kumpa huduma ya kwanza kwa kutumia mafuta ya kondoo kama tiba ya kitamaduni.

Baadaye alitoa taarifa kwa baba yake, shahidi wa tatu ambaye alienda na kumchukua binti yake kisha kumpeleka hospitali kwa ajili ya matibabu.

Shahidi wa nne, Dk Wilbert Kessy, aliyemchunguza mwathirika wa tukio hilo alidai kuwa sehemu za siri za mwathirika wa tukio ziliashiria kuingiliwa kingono mara kwa mara.

Mrufani na mwenzake walikana kuhusika na makosa hayo ambapo alidai mkewe (mwathirika wa tukio hilo) alitoroka na kurudi kwa wazazi wake na kwamba majeraha hayo aliyapata akiwa kwa wazazi wake.

Kuhusu ubakaji alidai mwaka 2020 baada ya kukamilisha taratibu zote za kitamaduni zinazohitajika na mila za kimasai na alikuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa hiari yake kama mkewe.

Mahakama baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote iliwahukumu kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la kwanza na pili na kuamuru kila mmoja kumlipa mwathirika wa tukio hilo faini ya Sh milioni mbili.

Mrufani alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la ubakaji,hukumu ambazo zilienda sambamba.

Katika rufaa ya kwanza Mahakama Kuu,iliunga mkono hatia na hukumu isipokuwa faini katika makosa mawili ya awali ambayo ilipunguza na kuwa Sh300,000.

Katika rufaa ya pili, mrufani alikuwa na sababu tisa ambazo ziligawanywa na Mahakama hiyo katika misingi mitatu ambayo ni Mahakama mbili, zilifanya makosa kumtia hatiani kwa kosa la ubakaji na kumhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela  akiwa na umri wa miaka 18,kinyume na kifungu cha 131 (2) (a) cha Kanuni ya Adhabu.

Nyingine ni tofauti kati ya shtaka na ushahidi wa upande wa mashtaka pamoja na kesi dhidi yake haikuthibitishwa pasipo kuacha shaka.

Katika rufaa hiyo,mrufani alijiwakilisha mwenyewe bila kuwa na wakili ambapo awali  alionyesha kutoweza kufuatilia kesi mahakamani kwa sababu ya kikwazo cha lugha kwani hakuwa anaelewa wala kuweza kuzungumza lugha ya Mahakama ambayo ni Kiswahili na Kiingereza isipokuwa kimasai pekee.

Mahakama ilitafuta mkalimani anayejua lugha ya Kiswahili na kimasai, alipatikana Kirema Kivuyo ambaye aliapishwa na kuwa mkalimani katika kesi hiyo.

Kwa ufupi ni kuwa mrufani alilalamika kuwa mwaka 2020 alikuwa na umri wa miaka 18 huku mwathirika wa tukio hilo akiwa na umri wa miaka 14, hivyo adhabu dhidi yake ilipaswa viboko tu.

Aidha alitoa hoja kadhaa, ikiwamo madai kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa na upungufu, kulikuwa na tofauti kati ya shtaka na ushahidi uliotolewa kwamba kesi haikuthibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.

Aidha, alijitetea kuwa alikuwa katika ndoa ya kimila na mwathiriwa tangu mwaka 2020, akidai kuwa uhusiano wao ulikuwa wa hiari kwa mujibu wa mila za jamii yao.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufaa haikujikita sana katika hoja hiyo ya ndoa ya kimila, badala yake ikaweka mkazo katika kasoro ya msingi ya ushahidi wa mwathiriwa.

Katika uchambuzi wake, Mahakama ilieleza kuwa, kwa mujibu wa sheria za ushahidi na mwenendo wa makosa ya jinai, shahidi yeyote mwenye umri zaidi ya miaka 14 anatakiwa kula kiapo au kuthibitisha kabla ya kutoa ushahidi mahakamani.

Jaji Ngwembe amesema kuwa kushindwa kufuata utaratibu huo ni kosa la kisheria linalofanya ushahidi huo kuwa batili na usioweza kutumika katika kuamua hatia ya mtuhumiwa.

Kutokana na hali hiyo, ushahidi wa mwathiriwa uliokuwa nguzo kuu ya kesi ya ubakaji uliondolewa na kuiacha kesi hiyo bila msingi imara wa kuthibitisha kosa hilo.

Mahakama ilisisitiza kuwa katika kesi za ubakaji, ushahidi wa mwathiriwa ni muhimu sana, kwani ndiye anayeelezea tukio lenyewe moja kwa moja. Bila ushahidi huo, ushahidi mwingine hubaki kuwa wa ziada tu na hauwezi kuthibitisha kosa hilo kwa kiwango kinachohitajika.

Jaji amesema katika kesi hiyo ingawa daktari aliyemchunguza mwathiriwa alithibitisha kuwepo kwa dalili za kuingiliwa kingono, Mahakama ilieleza kuwa, ushahidi huo hauwezi kusimama peke yake bila kuungwa mkono na ushahidi wa moja kwa moja kutoka kwa mwathiriwa.

Mashahidi wengine waliotoa ushahidi walieleza hali waliyomkuta nayo mwathiriwa baada ya tukio, lakini hawakushuhudia tukio lenyewe, hivyo ushahidi wao haukuweza kuthibitisha hatia ya mrufani bila shaka yoyote.

Kwa upande wa Jamhuri uliokuwa unapinga rufaa hiyo mwanzoni, ulijikuta ukibadilisha msimamo na kuunga mkono rufaa baada ya kubaini kasoro hiyo ya kisheria.

Mahakama ya Rufaa ilikubaliana na hoja hiyo ya Jamhuri, ikieleza kuwa Mahakama za chini zilifanya makosa kwa kupokea ushahidi usiozingatia sheria na kuutegemea katika kutoa hukumu.

Kutokana na sababu hizo, Mahakama iliamua kubatilisha hukumu ya awali na kuamuru mrufani aachiliwe huru mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine za kisheria.