Iran Yakanusha Mazungumzo na Marekani, Yamjibu Trump Kuhusu Nishati

Global Publishers
March 23, 2026
0 Comments

Serikali ya Iran kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje imekanusha vikali madai ya Rais wa Marekani Donald Trump kwamba kuna mazungumzo yanayoendelea kati ya Washington na Tehran.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa shirika la habari la Mehr, Iran imesema kauli ya Trump ya kusitisha kwa muda mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ni mbinu ya kupunguza bei ya mafuta duniani, si ishara ya diplomasia.

Aidha, chanzo cha juu serikalini kimenukuliwa kikisema:

“Tunapinga madai ya Trump kuhusu mazungumzo, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitakubali mazungumzo yoyote hadi malengo yake katika vita yatakapofikiwa.”

Kauli hiyo inakuja wakati Trump akitoa onyo la saa 48 kwa Iran kufungua tena njia muhimu ya bahari ya Strait of Hormuz, ambayo imekuwa na usumbufu mkubwa baada ya kufungwa kwa kiasi, hali iliyosababisha kupanda kwa bei ya mafuta na gesi duniani huku meli za mafuta zikikwama kupita.

Mvutano huu unaendelea kuongeza hofu ya kuyumba kwa uchumi wa dunia, hasa katika sekta ya nishati.