Kiu ya ubingwa yaitesa KVZ

KATI ya timu za vikosi zinazoshiriki Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) ambazo hazijawahi kubeba ubingwa wa ligi hiyo, KVZ ni mojawapo tangu kuanza kwa ligi hiyo mwaka 1984. Nyingine ni Uhamiaji.

Akizungumza na Mwanaspoti, kiungo mshambuliaji wa KVZ, Seif Said Seif ‘Tiote’ amewasihi mshabiki kutochoka kuwasapoti kwani nao wanapambana kuhakikisha taji linapatikana.

“Tunajua mashabiki wa KVZ kiu yao ni ubingwa kama ilivyo kwetu wachezaji na viongozi wa timu, hivyo nawasihi tuendelee kushikamana, wasichoke kwa sababu hili ni letu kwa pamoja,” alisema Tiote.

Tiote alisema kutokana na uvumilivu wanaouonyesha mashabiki hawajakata tamaa na kuamini kuwa ipo siku KVZ itakuwa bingwa wa ZPL.

Alisema, kawaida furaha inatafutwa haijalishi itachukua muda gani kuipata, lakini lazima ipatikane ndio maana wachezaji wa timu hiyo wanajitahidi kujipambania ili kuwapa furaha mashabiki wake.

Pia, alisema mashabiki wa timu hiyo wamekuwa wahusika wa kutoa hamasa kwa wachezaji kufanya vizuri na hata ilivyomaliza nafasi ya pili msimu wa 2024-2025 mchango wao ulikuwepo.

Msimu uliopita 2024-2025, KVZ ilikosa ubingwa huo kwa tofauti ya mabao 23 dhidi ya Mlandege baada ya zote kumaliza na pointi 62. Mlandege ilifunga mabao 67 na kuruhusu 21, wakati KVZ ikifunga 35 na kuruhusu 12.

Kiungo huyo, alisema ingawa msimu uliopita KVZ ilimaliza nafasi ya pili, lakini ilimfanya ang’are zaidi na msimu huu umekuwa tofauti baada ya kupata majeraha.

Kwa sasa KVZ ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ZPL ikiwa na jumla ya alama 37, nyuma ya vinara wa ligi hiyo Fufuni yenye pointi 38 baada ya zote kucheza mechi 20 zikibaki 10 kukamilisha msimu.