MIRADI YA SHILINGI BILIONI 85 KUCHOCHEA USHIRIKIANO WA TANZANIA NA AUSTRIA

*****

Tanzania na Austria zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati yenye thamani ya Euro milioni 30 (takriban Shilingi bilioni 85), itakayolenga sekta za elimu, usalama na ufundi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Munde, Machi 23, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo na ujumbe kutoka Austria ulioongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria anayeshughulikia masuala ya kisiasa, Mhe. Balozi Dkt. Hannah Liko. Amesema ziara hiyo imekuja wakati muafaka ambapo Tanzania inahitimisha Dira ya Maendeleo ya 2025 na kuanza mchakato wa Dira mpya ya 2050.

Mhe. Munde amebainisha kuwa Austria imekuwa ikifadhili miradi muhimu kupitia mikopo nafuu inayochangia moja kwa moja maendeleo ya wananchi, ikiwemo mradi wa ukarabati na uwekaji wa mifumo ya kisasa katika Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Karume (KIST) Zanzibar pamoja na maboresho ya mfumo wa elimu visiwani humo. Miradi mingine ni ukarabati wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) pamoja na ununuzi na usambazaji wa magari ya kuzima moto na vifaa vya uokoaji Zanzibar.

Aidha, Mhe. Munde amewasilisha salamu za shukrani kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa Austria ni mshirika wa maendeleo anayeaminika na kwamba Tanzania iko tayari kuimarisha ushirikiano huo kwa lengo la kuinua hali ya kijamii na kiuchumi ya wananchi.

Kwa upande wake, Balozi Dkt. Liko amepongeza ushirikiano huo madhubuti na kuahidi kuwa Austria itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta za utalii na viwanda ili kuongeza tija ya kiuchumi kwa pande zote mbili.

Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili pia zimejadili utekelezaji wa Mkakati wa Austria na Afrika wa mwaka 2026–2029 unaolenga kuimarisha amani na usalama, kukuza uchumi wa kijani, kukabiliana na uhamiaji haramu huku ikiimarishwa mifumo ya uhamiaji wa kisheria na wenye tija, pamoja na kuendeleza sayansi na elimu.