Mtaalamu wa Lishe Afichua Matunda Yasilofaa Kula Asubuhi

Mtaalamu wa lishe, Nichola Ludlam-Raine, amefichua aina ya matunda ambayo hayapendekezwi kuliwa mara kwa mara wakati wa kifungua kinywa, akieleza kuwa baadhi ya matunda maarufu yana kiwango kikubwa cha sukari asilia kuliko watu wanavyofahamu.

Akizungumza na The Telegraph, Ludlam-Raine alifanya tathmini ya matunda 18 yanayopendwa nchini Uingereza, akiyapima kulingana na virutubisho kama vitamini na madini, kiwango cha nyuzinyuzi (fibre), pamoja na kiasi cha sukari asilia kilichopo katika kila tunda.

Kwa mujibu wake, ingawa matunda yana wanga katika mfumo wa sukari asilia kama fructose, nyuzinyuzi zilizomo husaidia kupunguza kasi ya mmeng’enyo wa chakula na kusaidia kuzuia kupanda kwa ghafla kwa sukari kwenye damu.

Alibainisha kuwa watu wenye changamoto za kisukari au upinzani wa insulini wanapaswa kuwa waangalifu zaidi na ukubwa wa sehemu wanazokula, akipendekeza kiasi cha takribani gramu 80 au konzi moja kama kipimo sahihi.

Licha ya matunda kuwa sehemu muhimu ya lishe bora, mtaalamu huyo alieleza kuwa si matunda yote yana faida sawa inapokuja katika matumizi ya kila siku, na baadhi yanapaswa kuzingatiwa zaidi kama “treat” badala ya kuwa chakula cha kawaida cha kila siku.

Katika tathmini hiyo, matunda ya jamii ya tikiti yamepata alama ya chini zaidi, yakishika nafasi ya mwisho kwa alama 1 kati ya 5. Hii inajumuisha Tikiti maji (Watermelon), Cantaloupe, Honeydew melon na Galia melon, ambayo yameelezwa kuwa na kiwango kikubwa cha sukari na nyuzinyuzi kidogo ukilinganisha na matunda mengine yaliyofanyiwa tathmini.

Matokeo hayo yanaashiria umuhimu wa kuchagua matunda kwa uangalifu, hasa kwa watu wanaotafuta kudhibiti viwango vya sukari mwilini au wanaopendelea kifungua kinywa chenye lishe bora na yenye uwiano mzuri wa virutubisho.

Kwa ujumla, wataalamu wa lishe wanasisitiza ulaji wa matunda kwa kiasi na kuchagua aina zenye nyuzinyuzi nyingi ili kusaidia afya bora ya mwili na udhibiti wa nishati kwa siku nzima.